06. Msimamo sahihi kuhusu kutengeneza picha na wachoraji

Suala la nne: Je, jambo hili ni katika yale yanayopaswa kukemewa au hapana?

Imethibiti kwa dalili za Qur-aan na Sunnah kwamba kukemea maovu ni katika wajibu mkubwa sana, bali zimekuja Hadiyth zinazoonyesha kuwa hili ni katika misingi mikubwa ya dini, nguzo zake zenye nguvu na msingi wake madhubuti. Ummah huu utaendelea kuwa katika kheri muda wa kuwa unaamrisha mema na unakataza maovu. Ukiacha hilo, basi utapatwa na adhabu inayojulikana. Waislamu hawakutofautiana kuhusu wajibu wa kuamrisha mema na kukataza maovu, ingawa wametofautiana katika baadhi ya maelezo yake, masharti yake na namna yake. Vipi wasiafikiane juu yake ilihali Qur-aan imelieleza kwa wingi katika maeneo mengi! Sunnah imekuja na dalili nyingi juu ya mada hiyo ambazo kama zingekusanywa basi zingekuwa kitabu kikubwa.

Tumeeleza hapo awali kuwa kutengeneza picha za wanyama ni haramu. Na pia imethibiti kwa dalili za kuamrisha mema na kukemea maovu kwamba kila lililoharamishwa ni lazima likemewe. Hivyo kutengeneza picha ni haramu na kila haramu ni maovu. Kwa hiyo kutengeneza picha ni maovu na kila maovu ni lazima yakemewe. Kwa maana nyingine kitendo cha kutengeneza picha ni lazima kikaripiwe. Dalili za hoja hizi zimetajwa hapo awali. Hazina shaka kwa mwenye kuelewa hoja za Kishari´ah.

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin ´Aliy ash-Shawkaaniy (afk. 1250)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Hukm-ut-Taswwiyr, uk. 28-31
  • Imechapishwa: 07/05/2026