06. Nuuh alitumwa kwa watu ambao walikuwa wamechupa mipaka kwa watu wema

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah alimtuma kwa watu wake walipopetuka mipaka watu wema; Wadd, Suwaa´, Yaghuuth, Ya´uuq na Nasr.

MAELEZO

Allaah alimtuma Nuuh (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa watu wake pindi walipotumbukia katika upetukaji mipaka kwa watu wema. Mtunzi (Rahimahu Allaah) ameweka mlango katika “Kitaab-ut-Tawhiyd” juu ya maudhui hii “Sababu ya kukufuru kwa mwanaadamu na kuacha dini yake ni kupetuka mipaka kwa watu wema.”

Kupetuka mipaka maana yake ni kule kuvuka mipaka katika ´ibaadah, matendo na kusifu, ni sawa kwa njia nzuri au mbaya. Kuna aina nne ya upetukaji mipaka:

1 – Kupetuka mipaka katika ´Aqiydah. Ni kama mfano wa upetukaji mipaka wa wanafalsafa inapokuja katika sifa. Imewafikisha katika kiwango cha wao kuzifananisha sifa za Allaah na sifa za viumbe au kuzikanusha.

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ndio wako kati kwa kati. Wanathibitisha yale majina na sifa ambazo Allaah amejithibitishia nazo Mwenyewe na ambazo zimemthibitishia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanafanya hivo pasi na upotoshaji, ukanushaji, kuziwekea namna na kuzifananisha.

2 – Kupetukaji mipaka katika ´ibaadah. Mfano wa hilo ni kama uvukaji mipaka wa Khawaarij. Wanaonelea kuwa mwenye kufanya dhambi kubwa ni kafiri. Mfano mwingine ni kama Mu´tazilah. Wanaonelea kuwa anayefanya dhambi kubwa yuko baina ya imani na ukafiri. Huku ni kuvuka mipaka. Wanakabiliwa na usahilishaji wa Murji-ah ambao wanasema kuwa imani haidhuriki kwa madhambi.

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wako kati kwa kati. Wanasema kuwa madhambi yanaipunguza imani kwa kiwango cha dhambi itavyokuwa.

3 – Kupetuka mipaka katika mambo ya miamala. Baadhi wanaharamisha kila kitu wakati wengine wanahalalisha kila kitu chenye kukuza pesa na uchumi. Wamefikia kiasi cha kuhalalisha mpaka ribaa na ghushi.

Msimamo wa kati na kati ni kusema kwamba miamala iliojengeka juu ya uadilifu ambao unaafikiana na dalili za Qur-aan na Sunnah ndio halali.

4 – Kupetuka mipaka katika mambo ya ada na desturi. Kuna ambao wameng´ang´ania kushikilia zile ada za zamani na hawataki kuzibadilisha na zile ambazo ni bora zaidi. Ama ada hizo zikiwa zinalingana katika manufaa, kule mtu kubaki katika hali aliyomo ni bora kuliko kuchukua desturi zenye kutoka nje.

Mtu mwema ni yule mwenye kutimiza haki ya Allaah na haki za waja wa Allaah.

Waad, Suwaa´, Yaghuuth, Ya´uuq na Nasr ni masanamu yaliokuweko wakati wa Nuuh (´alayhis-Salaam). Walikuwa ni waja wema. Imepokelewa katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy ya kwamba Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Haya ni majina ya watu wema kutoka katika watu wa Nuuh. Walipokufa, shaytwaan akawafanya watu wao kutengeneza masanamu, wakayaweka mahala walipokuwa wakikaa na wakayapa majina yao. Matokeo yake wakafanya hivo na hayakuabudiwa mpaka walipokufa na elimu ikasahaulika. Hapo ndipo wakaanza kuabudiwa.”[1]

Katika tafsiri hii kuna utatizi, nao ni maneno yake (Radhiya Allaahu ´anh):

“Haya ni majina ya watu wema kutoka katika watu wa Nuuh.”

Udhahiri wa Qur-aan ni kwamba waliishi kabla ya Nuuh. Allaah (Ta´ala) amesema:

قَالَ نُوحٌ رَّبِّ إِنَّهُمْ عَصَوْنِي وَاتَّبَعُوا مَن لَّمْ يَزِدْهُ مَالُهُ وَوَلَدُهُ إِلَّا خَسَارًا وَمَكَرُوا مَكْرًا كُبَّارًا وَقَالُوا لَا تَذَرُنَّ آلِهَتَكُمْ وَلَا تَذَرُنَّ وَدًّا وَلَا سُوَاعًا وَلَا يَغُوثَ وَيَعُوقَ وَنَسْرًا

“Nuuh akasema: “Mola wangu! Hakika wao wameniasi na wakafuata yule ambaye mali yake na wanawe hawakumzidishia isipokuwa khasara. Na wakapanga njama kubwa. Wakasema: “Msiwaache miungu yenu – na wala msimwache Wadd na wala Suwaa´ na wala Yaghuuth na Ya’uuq na Nasr!” (71:21-23)

Udhahiri wa Aayah unafahamisha kuwa watu wa Nuuh walikuwa wakiyaabudu na kwamba aliwakataza. Muundo wa Aayah unafahamisha aliyotaja Ibn ´Abbaas. Hata hivyo mtiririko wa Aayah unadhihirisha kuwa watu hawa wema waliishi kabla ya Nuuh (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – na Allaah ndiye anajua zaidi.

[1] al-Bukhaariy (4636).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Utaymiyn
  • Mfasiri: Fitqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 17
  • Imechapishwa: 23/04/2022