06. Maamrisho ya Abu Haniyfah ya kushikamana na Sunnah

Hapa inaweza kuwa jambo lenye faida kutaja maneno ya maimamu wenye kufuatwa kuhusu kufuata Sunnah na kujiepusha na maoni yao pale yanapokwenda kinyume na Sunnah. Huenda ndani yake kukawa kuna mazingatio na ukumbusho kwa wale wenye kuwafuata wao na walio chini yao kichwa mchunga[1] na kushikamana barabara na madhehebu yao kama kwamba yameteremshwa kutoka mbinguni. Allaah (´Azza wa Jall) anasema:

اتَّبِعُوا مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُمْ وَلَا تَتَّبِعُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ ۗ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ

“Fuateni yale mliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wenu na wala msifuate badala Yake walinzi – ni machache mnayoyakumbuka.”[2]

1- Abu Haniyfah (Rahimahu Allaah)

Wa mwanzo wao ni Imaam Abu Haniyfah an-Nu´maan bin Thaabit (Rahimahu Allaah). Marafiki zake wamepokea ibara na maneno mbalimbali kutoka kwake. Yote yanaelekeza sehemu moja; uwajibu wa kuzitendea kazi Hadiyth na kuacha kufuata kichwa mchunga maoni ya maimamu yanayokwenda kinyume nazo. Kwa mfano amesema:

1- “Hadiyth ikisihi basi hayo ndio madhehebu yangu.”[3]

2- “Haifai kwa yeyote kuchukua maoni yetu muda wa kuwa hajui ni wapi tumeyatoa.”[4]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Ni haramu yule asiyejua dalili yangu kutufu maoni yangu.”

Katika upokezi wa tatu amezidisha kwa kusema:

“Kwa sababu sisi ni watu; tunasema neno leo na tunajirudi kesho.”

Katika upokezi wa nne imekuja:

“Maangamivu ni kwako ee Ya´quub (Abu Yuusuf)! Usiandike kila unachosikia kutoka kwangu. Mimi naweza kuonelea maoni leo na nikaachana nayo kesho na nikaonelea maoni kesho na nikaachana nayo baada ya kesho.”[5]

3- “Nikisema kitu kinachoenda kinyume na Kitabu cha Allaah (Ta´ala) na maelezo ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi yaache maneno yangu.”[6]

[1] Ufuataji wa kipofu huu ndio ule ambao Imaam at-Twahaawiy alikuwa akimaanisha pale aliposema:

“Hakuna ambaye anakuwa shabiki isipokuwa mpumbavu au mfuataji kichwa mchunga.”

Ameyanukuu Ibn ´Aabidiyn katika ”Rasm-ul-Muftiy” kutoka katika ”Majmuu´-ur-Rasaa-il” (1/32).

[2] 07:03

[3] Ibn ´Aabidiyn katika ”al-Haashiyah” (1/63) na ”Rasm-ul-Muftiy” kutoka ”Majmuu´-ur-Rasaa-il” (¼) na Shaykh Swaalih al-Fulaaniy katika ”Iyqaadhw-ul-Himam”, uk. 62. Ibn ´Aabidiyn ameyanukuu yafuatayo kutoka kwenye ”Sharh-ul-Hidaayah” ya Ibn Shahnah:

“Hadiyth ikisihi na wakati huohuo madhehebu yakawa yanasema kitu kingine, basi Hadiyth ndio itayotakiwa kutendewa kazi na hayo ndio yanakuwa madhehebu yake. Haina maana kwamba yule mwenye kuiendea kazi anaacha kuwa Hanafiy! Kwani imesihi kwamba Abu Haniyfah amesema:

“Itaposihi Hadiyth basi hayo ndio madhehebu yangu.”

Ameyanukuu hayo Imaam ´Abdil-Barr kutoka kwa Abu Haniyfah na maimamu wengine.”

Haya yanaonyesha ukamilifu wa dini na uchaji wao. Kwani hayo yanaashiria kwamba elimu yao haikuizunguka Sunnah yote. Hayo yamesemwa wazi na Imaam ash-Shaafi´iy. Ilikuwa inaweza kutokea wanafanya kitu kinachopingana na Sunnah kwa sababu hakijawafikia. Hivyo wanatuamrisha kushikamana barabara na Sunnah na kukifanya ni katika madhehebu yao. Allaah awarehemu wote!

[4] Ibn ´Abdil-Barr katika ”al-Intiqaa’ fiy Fadhwaa-il-il-A-immah al-Fuqahaa’”, uk. 145, Ibn-ul-Qayyim katika ”I´laam-ul-Muwaqqi´iyn” (2/309), Ibn ´Aabidiyn katika taaliki yake ya ”al-Bahr al-Raa-iq” (6/293) na ”Rasm-ul-Muftiy”, uk. 29 na 32, na ash-Sha´raaniy katika ”al-Miyzaan” (1/55) pamoja na ule upokezi wa pili.

Upokezi wa tatu ameupokea ´Abbaas ad-Duuriy katika ”at-Taariykh” (1/77/6) ya Ibn Ma´iyn kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kutoka kwa Zufar. Maneno kama hayo yamepokelewa vilevile kutoka kwa maswahiba zake kama Zufar, Abu Yuusuf na ´Aafiyah bin Yaziyd, kama yalivyotajwa katika ”al-Iyqaadhw”, uk. 65, kupitia akiwemo vilevile Ibn ´Abdil-Barr na Ibn-ul-Qayyim.

Ikiwa wamesema hivo juu ya yule asiyejua dalili yao, najiuliza wanachosema juu ya yule ambaye atajua kuwa dalili yao imepingana na maoni yao licha ya hivo akaitanguliza. Zingatia hilo. Hilo tu linatoshab kusambaratisha kufuata kichwa mchunga. Hilo ni kwa sababu siku moja nilimkemea mmoja wa watu hawa wenye kufuata kichwa mchunga ambaye alitoa fatwa kwa mujibu wa maoni ya Abu Haniyfah ambayo hakutambua dalili yake, akapinga kwamba Abu Haniyfah ndiye ambaye kasema hivo!

[5] Hilo linatokana na kwamba imamu mara nyingi hujenga maoni yake juu ya kipimo (Qiyaas). Baada ya hapo anabainikiwa na  kipimo kingine kilicho na nguvu zaidi kuliko au Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo anayaacha maoni yake ya zamani. ash-Sha´raaniy amesema:

“Vile ninavyoamini mimi na kila ambaye ana inswafu ni kwamba iwapo Abu Haniyfah (Rahimahu Allaah) angeliishi mpaka ikaandikwa Shari´ah yote na kukusanywa, angeichukua na kuachana na kila kipimo. Vipimo vingelikuwa vichache katika madhehebu yake kama ambavo vilevile vingelikuwa vichache katika madhehebu ya wengine. Lakini ilipokuwa kwamba dalili za Shari´ah ni zenye kutofautiana katika wakati wake pamoja na Taabi´uun na waliokuja baada ya Taabi´uun katika miji, vijiji na mipaka ya nchi, bila shaka ndipo kipimo kikawa ni chenye kutumika zaidi katika madhehebu yake ukilinganisha na madhehebu mengine. Kwa sababu madhebeu yake hayakuwa na dalili kutoka katika Qur-aa na Sunnah juu ya yale mambo ambayo yalitumia kipimo juu yake. Tofauti na ilivyokuwa katika madhehebu mengine. Wanachuoni walikuwa wamesafiri kwenda katika miji na vijiji kwa ajili ya kutafuta, kukusanya na kuziandika Hadiyth. Kwa njia hiyo ikawa Hadiyth za Shari´ah zinajazana zenyewe kwa zenyewe. Kwa hiyo hii ndio ilikuwa sababu ya kipimo kuwepo kwa wingi katika madhehebu yake na uchache katika madhehebu mengine.” (al-Miyzaan (1/62))

Sehemu yake kubwa imenakiliwa na Abul-Hasanaat katika ”an-Naafiy´ al-Kabiyr”, uk. 135, ambapo pia kaandika taaliki yenye kuisapoti na kuyaweka wazi zaidi. Arejee huko yule anayetaka.

Ikiwa huu ndio udhuru wa Abu Haniyfah kutokana na yale maoni yanayopingana na Hadiyth Swahiyh pasi na kukusudia (na bila shaka ni udhuru wenye kukubalika kwa sababu Allaah (Ta ´ala) haikalifishi nafsi zaidi ya vile inavyoweza), hivyo itakuwa haijuzu kumtukana kama wanavofanya baadhi ya wajinga. Ni wajibu kuwa na adabu naye. Kwa sababu ni mmoja katika maimamu wa waislamu ambao wameihifadhi dini hii na kuyasambaza mataga yake. Ni mwenye kulipwa thawabu kwa hali yoyote, ni mamoja amepatia au amekosea. Kama ambavyo haijuzu kwa wale wenye kumuadhimisha kushikamana na maoni yake yanayotofautiana na Hadiyth. Kwani Hadiyth ndio madhehebu yake, kama ulivyojionea mwenyewe akisema. Hawa wamoja wako mashariki na hawa wengine wako magharibi. Haki iko baina ya hawa wawili:

رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Ee Mola wetu! Tusamehe sisi na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo juu ya wale walioamini. Ee Mola wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma, Mwenye kurehemu.” (59:10)

[6] al-Fulaaniy katika ”al-Iyqaadhw”, uk. 50, amemnasibishia Imaam Muhammad maneno kama hayo. Kisha akasema:

“Haya na mfano wake hayamuhusu Mujtahid kwa sababu si mwenye kuhitajia jambo hilo – haya yanamuhusu yule mwenye kufuata upofu.”

Kutokana na haya ash-Sha´raaniy amesema:

“Iwapo utauliza ni kipi cha kufanya juu ya zile Hadiyth zilizosihi baada ya kufariki kwa imamu wako na wala hakuzitendea kazi, unachotakiwa kujua ni kwamba ni lazima kwako kuzitendea kazi. Endapo imamu wako angezitambua na akaona kuwa ni Swahiyh basi bila shaka angekuamrisha kuzitendea kazi. Maimamu wote ni wametekwa na mkono wa Shari´ah. Mwenye kufanya hivo basi kwa hakika ameishika kheri kwa mikono yake yote. Yule asiyezitendea kazi Hadiyth mpaka pale zitapokuwa zimefanyiwa kazi na imamu wake, basi hakika atapitwa na kheri nyingi. Hiyo ndio hali ya watu wengi ambao wanawafuata kichwa mchunga maimamu wa madhehebu. Ingelikuwa bora kwao kutendea kazi kila Hadiyth iliyosihi baada ya maimamu wao na hivyo kutekeleza wasia wa imamu. Tunaamini kwamba lau wangeishi muda mrefu na kuzishika Hadiyth hizo zilizosihi baada yao, basi wangezichukua, kuzitendea kazi na kuachana na kila kipimo walichopima hapo kabla.” (al-Miyzaan (1/26))

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 41-43
  • Imechapishwa: 16/01/2019