05. Mfumo katika “Swifatu Swalaat-in-Nabiy”

Pale ilipokuwa kitabu kinazungumzia ni vipi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivoswali, ikawa pasi na shaka sifuati madhehebu maalum. Nataja tu yale yaliyothibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kama yalivyo madhehebu ya Muhaddithuun[1] siku zote[2]. Amepatia mshairi aliyesema:

Ahl-ul-Hadiyth ndio watu wa Mtume

Hata kama hawakutangamana naye

lakini wametangamana na nyendo zake[3]

Kwa ajili hiyo kitabu hiki kitakusanya maudhui kusudiwa ambayo kuna tofauti katika vitabu vya madhehebu. Hakuna kitabu wala madhehebu yoyote ambayo yamepatia katika kila kitu. Yule ambaye atakitendea kazi kitabu hiki basi atakuwa – Allaah akitaka – miongoni mwa wale ambao Allaah amesema juu yao:

 لِمَا اخْتَلَفُوا فِيهِ مِنَ الْحَقِّ بِإِذْنِهِ ۗ وَاللَّـهُ يَهْدِي مَن يَشَاءُ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ

“… katika yale waliyotofautiana kwa idhini Yake na Allaah humwongoza amtakaye kuelekea njia iliyonyooka.”[4]

Jengine ni kwamba pinid nilipoamulia kujiwekea mfumo huu katika kitabu hiki, nao ni kushikamana na Sunnah Swahiyh, na kuandika vitabu vyangu kutokanaa na mfumo huo, nikatambua kuwa sintoyaridhisha makundi na mapote yote. Nilijua kuwa baadhi yao au wengi wao wataniponda. Hakuna ubaya kwa upande wangu. Najua kuwa kuwaridhisha watu wote ni jambo lisilowezekana. Najua pia kwamba yule ambaye atawaridhisha watu kwa kitu kinachomkasirisha Allaah basi Allaah atamtegemezea watu, kama alivosema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[5]. Kwangu inatosha kutambua kuwa hii ndio njia iliyonyooka ambayo Allaah kawaamrisha waumini kushikmana nayo na ambayo imebainishwa na Mtume wetu Muhamad  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye ndiye bwana wa Mitume. Njia hii ndio ambayo ilifuatwa na wema waliotangulia katika Maswahabah, Taabi´uun na wale waliokuja baada yao wakiwemo wale maimamu wane ambao waislamu wengi hii leo wanajinasibisha nao. Wote ni wenye kukubaliana juu ya kushikamana barabara na Sunnah na kurejea kwayo na kuacha yale yote yanayokwenda kinyume nayo bila kujali ni ukubwa kiasi gani mwenye kwenda kinyume huyo atavyokuwa. Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni mkubwa zaidi na njia yake ndio bora zaidi. Kwa ajili hiyo mimi nimechagua kuiga mwongozo na maamrisho yao ya kushikamana barabara na Sunnah japokuwa yatakuwa yanaenda kinyume na maoni yao. Maamrisho yao yalikuwa na athari kubwa kwangu juu ya kushika njia hii iliyonyooka na kupuuzilia mbali kufuata kichwa mchunga. Allaah (Ta´ala) awajaze kheri kwa yale waliyofanya kwangu.

[1] Abul-Hasanaat al-Luknawiy amesema:

“Yule mwenye kutazama kwa jicho la inswafu Fiqh na misingi atajua kiyakini kabisa kwamba Muhaddithuun siku zote ndio wenye maoni yaliyo na nguvu kuliko wengine katika mambo ambayo wanachuoni wametofautiana juu yake. Kila ninapoingia katika mambo yaliyo na tofauti basi huona kuwa Muhaddithuun ndio walio karibu zaidi na uadilifu. Uzuri ulioje walivo! Wanastahiki kushukuriwa. Ni vipi isiwe hivo ilihali wao ndio warithi wa kweli wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mabalozi wake? Allaah atufufue pamoja na kundi lao na atujaalie kuwapenda.” (Imaam-ul-Kalaam fiymaa yata´allaq bil-Qiraa-ati khalf-al-Imaam, uk. 156)

[2] as-Subkiy amesema:

“Swalah ni jambo muhimu kwa waislamu. Hivyo ni wajibu kwa kila muislamu kuitilia umuhimu, kuihifadhi na kusimamisha nembo zake. Baadhi ya mambo ya swalah kuna maafikiano juu yake. Ni lazima kuyatekeleza. Kuna mambo mengine ambayo wanachuoni wametofautiana juu ya uwajibu wake. Njia nyoofu katika hayo ni mambo mawili:

1- Mtu afanye vyema kiasi anachoweza ili kuepuka tofauti.

2- Kujibiidisha na yale yaliyosihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ayatendee kazi. Mwenye kufanya hivo basi swalah yake itakuwa ya sawa na salama yenye kuingia ndani ya maneno Yake (Ta´ala):

فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا

“Basi yule anayetaraji kukutana na Mola wake, atende matendo mema na wala asimshirikishe yeyote katika ‘ibaadah za Mola wake.” (18:110) (al-Fataawaa (1/148))

Hilo jambo la pili sio bora tu, bali wajibu. Jambo la pili, pamoja na kwamba linakaribia kutowezekana katika mambo mengi, halihakikishi maamrisho yake Mtume (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam):

“Swalini kama mlivyoniona nikiswali.

Katika hali hii swalah yake pasi na shaka itakuwa ni yenye kutofautiana na swalah yake yeye (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam). Zingatia.

[3] Shairi la al-Hasan bin Muhammad al-Nasawiy. Ameipokea Haafidhw Dhwiyaa’-ud-Diyn al-Maqdisiy katika ”Fadhwl-ul-Hadiyth wa Ahlih”.

[4] 02:213

[5] at-Tirmidhiy, al-Qadhwaa´iy, Ibn Bishraan na wengineo. Nimeitaja Hadiyth hii na njia zake katika ”Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah” kisha katika ”as-Swahiyhah” (2311). Ikanibainikia kuwa Hadiyth haidhuriki kitu na wale wenye kuonelea kuwa hayo ni maneno ya Swahabah na kwamba Ibn Hibbaan vilevile ameisahihisha.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 38-41
  • Imechapishwa: 16/01/2019