04. Kitabu “Swifatu Swalaat-in-Nabiy” kilivyojengeka

Nimekigawanya kitabu sehemu mbili, sehemu ya juu na sehemu ya chini. Sehemu ya juu ni zile Hadiyth zenyewe au jumla zenye kulazimiana nayo. Nimeziweka sehemu yake stahiki na kuzikamatisha kwa njia ya kwamba kitabu kionekane kimekamatana kuanzia mwanzo wake mpaka mwisho wake. Nimejibidisha kuchunga maandiko na matamshi ya Hadiyth kama yalivyotajwa katika Sunnah. Inaweza kutokea Hadiyth ikawa na matamshi mbalimbali ambapo nikachagua tamshi linaloendana na mazingira au kitu kingine. Wakati mwingine huweka tamshi lingine na kuzindua juu ya hilo. Ni mara chache nitashirikisha upokezi kwa wapokezi wake ambao ni Maswahabah. Wala sibainishit ni maimamu wepi walioipokea kwa ajili ya kumfanyia wepesi msomaji na kurejea.

Ama sehemu ya pili ni kama maelezo ya yaliyo juu yake. Sehemu hiyo nimetaja vyanzo na viwango vya Hadiyth zilizo katika sehemu ya juu. Hutaja matamshi na njia zake. Nazungumzia cheni za wapokezi wake na mapokezi yanayoyatolea ushahidi ambayo ima nimeyasifia au nimeyakosoa, nimeyasahihisha au nimeyadhoofisha kwa mujibu wa elimu na kanuni za Hadiyth. Mara nyingi baadhi ya njia zina matamshi na nyongeza zisizopatikana katika njia zengine ambapo yanaweka katika Hadiyth husika katika ile sehemu ya juu. Ikiwa inawezekana basi huziweka vilevile pamoja na asili yake. Hubainisha hilo kwa kuyaweka katikati ya [ ]. Hata hivyo sitaji ni nani aliyepwekeka kupokea asili ikiwa chanzo cha Hadiyth kinatokamana na imepokelewa na Swahabah mmoja. Vinginevyo huiandika kwa kuitenganisha. Hayo utayaona kwa mfano katika zile du´aa za kufungulia swalah. Hilo ni jambo lenye faida na la kipekee ambalo unakaribia kutolipata katika kitabu kingine.

Hutaja vilevile uelewa wa wanachuoni mbalimbali juu ya Hadiyth husika tuliyoitaja, uelewa wa kila dalili na baada ya hapo kuujadili. Baada ya hapo hufupiza maoni yenye nguvu ambayo huyataja katika ile sehemu ya juu. Huenda wakati mwingine nikataja baadhi ya mambo yasiyokuwa na dalili ambayo ni Ijtihaad tu za wanachuoni, lakini hayako katika kitabu chetu hiki.

Kwa vile sehemu mbili zote za kitabu hiki hazijachapishwa, basi natosheka na ile sehemu ya juu na nakipa jina ”Swifatu Swalaat-in-Nabiy (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) minat-Takbiyr ilaat-Tasliym ka-annak taraah”.

Namuomba Allaah (Ta´ala) akifanye kiwe kwa ajili ya uso Wake mtukufu na awanufaishe kwacho ndugu zangu waumini. Kwani hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuitikia.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 37-38
  • Imechapishwa: 16/01/2019