03. Sababu ya kutunga “Swifatu Swalaat-in-Nabiy”

Nilipoona kuwa hakuna kitabu kilichoenea juu ya maudhui haya, ndipo nikaona ni wajibu kwangu kuandika kitabu kwa ajili ya ndugu zangu waislamu (ambao wanajali kuabudu kama Mtume wao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), chenye kukusanya yale yote yaliyofungamana na namna ya swalah ya Mtume (ambao wanajali kuabudu kama Mtume wao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuanzia katika Takbiyr mpaka kwenye Tasliym. Lengo ni ili wale wanaompenda Mtume (ambao wanajali kuabudu kama Mtume wao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mapenzi ya kweli iweze kuwa sahali kwao kutekeleza maamrisho yake katika Hadiyth iliyotangulia:

“Swalini kama mlivyoniona nikiswali.”

Kwa ajili hiyo nikajibidisha kuvipitia vitabu mbalimbali na kuzifuatilia Hadiyth zinazozungumzia kile ninachokiendea katika vitabu mbalimbali. Natija yake ikawa ni kitabu hiki kilicho mbele yako. Nilijiwekea sharti ya kutoweka Hadiyth yoyote isipokuwa tu ambayo kumethibiti[1] cheni ya wapokezi wake, zengine zote zimepuuzwa, pasi na kujali inahusiana na kitu gani katika swalah. Kwa sababu naamini kuwa zile Hadiyth zilizothibiti zinatosheleza vyema kwa mtu kutohitajia kutendea kazi zile dhaifu. Hapana tofauti kwamba Hadiyth dhaifu hazifidishi chochote zaidi ya dhana iliyoshindwa nguvu. Ni kama alivosema Allaah (Ta´ala):

وَإِنَّ الظَّنَّ لَا يُغْنِي مِنَ الْحَقِّ شَيْئًا

“Hakika dhana haitoshelezi chochote mbele ya haki.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Tahadharini na dhana! Kwani hakika dhana ni mazungumzo ya uongo.”[3]

Allaah (Ta´ala) hakutuamrisha kumuabudu kwa kutumia Hadiyth kama hizi, bali uhakika ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametukataza na jambo hilo na akasema:

“Jiepusheni kuelezea kuhusu mimi isipokuwa mliyoyajua.”[4]

Ikiwa kumekatazwa kusimulia mapokezi dhaifu, basi kuzitendea kazi ni jambo lina haki zaidi ya kukatazwa.

[1] Hadiyth iliyothibiti kunaingia ndani yake Swahiyh na ilio nzuri: Swahiyh kwa dhati yake, Swahiyh kupitia zengine, nzuri kwa dhati yake na nzuri kupitia zengine.

[2] 53:28

[3] al-Bukhaariy na Muslim. Imetajwa katika ”Ghaayat-ul-Maraam fiy Takhrij ‘al-Halaal wal-Haraam’” (412).

[4] Swahiyh. Ameipokea at-Tirmidhiy, Ahmad na Ibn Abiy Shaybah. Shaykh Muhammad Sa´iyd al-Halabiy ameinasibisha kwa al-Bukhaariy katika ”al-Musalsalaat” (2/1) yake na amekosea.

Halafu baadaye ikanibainikia kuwa Hadiyth hiyo ni dhaifu. Hapo kabla nilikuwa nikitegemea usahihishaji wa cheni ya wapokezi ya al-Munaawiy kwa Ibn Abiy Shaybah. Muda ulivyokwenda nikapata na kuona kuwa ni dhaifu. Cheni ya wapokezi hiyohiyo inatumiwa na at-Tirmidhiy na wengineo. Rejea katika kitabu changu ”Silsilat-ul-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah” (1783). Kunaweza kusimama mahala pake maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kusimulia kutoka kwangu ilihali anaona kuwa ni uongo basi yeye ni mwongo pia.”

Ameipokea Muslim na wengineo. Rejea utangulizi wa ”Silsilat-ul-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah”.

Vilevile inatoshelezwa na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Tahadharini kusimulia kwa wingi kutoka kwangu. Mwenye kuelezea kutoka kwangu basi asiseme isipokuwa haki tu au ukweli. Mwenye kusema juu yangu kitu ambacho sikukisema basi ajiandalie makazi yake Motoni.”

Ameipokea Ibn Abiy Shaybah (8/760), Ahmad na wengineo. Ipo katika ”as-Swahiyhah” (1753).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 36
  • Imechapishwa: 16/01/2019