06. Hupewi udhuru kuacha maneno ya Mtume na kufuata ya Shaykh lako

Ikiwa mtu atauliza kuhusu yale yaliyotangulia katika Hadiyth ya Zayd bin Khaalid, kutoka kwa Abu Twalhah ya kwamba Bisr bin Sa´iyd ambaye amesimulia kutoka kwa Zayd kwa kusema: “Kisha Zayd akalalamika ambapo tukarudi. Tahamaki mlangoni mwake kulikuwa na pazia lililokuwa na picha… Udhahiri wa haya yanafahamisha kuwa Zayd anaona kufaa kutundika mapazia yalio na picha.

Jibu ni kuwa Hadiyth za ´Aaishah ni zenye kutangulia na nyenginezo zilizo na maana kama hiyo zinafahamisha kuhusu uharamu wa kuning´iniza mapazia yalio na picha, kuhusu ulazima wa kuyavunja na kwamba yanazuia Malaika kuingia ndani. Zinaposihi Hadiyth kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi haitojuzu kupingana nazo kwa maneno wala matendo ya yeyote katika watu. Haijalishi kitu ni nani. Katika hali hiyo italazimika kwa muumini kuzifata na kushikamana na yale zinajulisha na kutupilia mbali yale yanayokwenda kinyume nazo. Amesema (Ta´ala):

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا

”Kile alichokupeni Mtume basi kichukueni na kile alichokukatazeni basi kiacheni.”[1]

قُلْ أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ ۖ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْهِ مَا حُمِّلَ وَعَلَيْكُم مَّا حُمِّلْتُمْ ۖ وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا ۚ وَمَا عَلَى الرَّسُولِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ

”Sema: ”Mtiini Allaah na mtiini Mtume, mkigeukilia basi hakika jukumu lake ni lile alilobebeshwa nanyi ni juu yenu yale mliyobebeshwa; na mkimtii mtaongoka na hapana juu ya Mtume isipokuwa ufikishaji wa wazi.”[2]

Allaah katika Aayah hii amempa dhamana ya kuongoka kwa yule anayemtii Mtume.

Amesema (Ta´ala):

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Basi watahadhari wale wanaokwenda kinyume amri yake; isije kuwapata fitina au ikawapata adhabu iumizayo.”[3]

Pengine Zayd (Radhiya Allaahu ´anh) hakujua pazia iliyokusudiwa au hakufikiwa na Hadiyth zinazojulisha uharamu wa kutundika mapazia yalio na picha. Hivyo akachukua udhahiri wa maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Isipokuwa iliyotandazwa kwenye nguo.”

Kwa hivyo atakuwa ni mwenye udhuru kwa kutozijua.

Lakini yule atakayezijua Hadiyth ambazo ni Swahiyh zinazofahamisha juu ya uharamu wa kusimamisha mapazia yalio na picha hapewi udhuru kwa kwenda kinyume nazo.

[1] 59:07

[2] 24:54

[3] 24:63

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Jawaab al-Mufiyd fiy Hukm-it-Taswwiyr kutoka katika Majmuu´-ul-Fataawaa (04/217-218)
  • Imechapishwa: 28/03/2022