al-Khattwaabiy (Rahimahu Allaah) amesema tena:

“Hakika si venginevyo adhabu ya mtengeneza picha imefanywa kubwa kwa sababu picha ilikuwa inaabudiwa badala ya Allaah. Ukiongezea kuwa kunamtia mtu katika mtihani kule kuitazama na baadhi ya nafsi humili kwayo.”

an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mlango unaoharamisha kutengeneza picha za wanyama na uharamu wa kuchukua vitu vyenye picha zisizotwezwa katika magodoro na kwenginepo na kwamba Malaika (´alayhimus-Salaam) hawaingii nyumba ilio na picha au mbwa. Maswahiba zetu na wanazuoni wengine wamesema:

“Kutengeneza picha za wanyama ni haramu na uharamu wake ni mkubwa. Ni miongoni mwa madhambi makubwa. Kwa sababu mtu ametishiwa kwa matishio haya makali yaliyotajwa katika Hadiyth mbalimbali. Ni mamoja mtu ameitengeneza kwa lengo itwezwe au sababu nyingine. Kazi aliyoifanya ni haramu kwa hali yoyote. Kwa sababu kufanya hivo ni kuiga maumbile ya Allaah (Ta´ala). Ni mamoja picha inayokuwa kwenye nguo, zulia, pesa, senti, jengo, ukuta au maeneo mengine.

Kuhusu kutengeneza picha ya miti, ngamia, magoti ya ngamia na venginevyo ambavo havina picha ya wanyama sio haramu. Hii ni hukumu ya picha yenyewe kama yenyewe. Lakini mtengeneza picha kufanya picha ya mnyama, ikiwa imetundikwa ukutani, nguo inayovaliwa, kilemba na mfano wake katika vitu ambavo havitwezwi basi ni haramu. Ikiwa katika zulia linalokanyagwa, mto na mfano wake katika vitu vinavyotwezwa basi sio haramu… mpaka aliposema: Hapana tofauti katika yote haya kati ya zile zenye kivuli na zisizokuwa na kivuli.

Huu ndio ufupisho wa madhehebu yetu katika suala hili. Kikosi cha wanazuoni wengi katika Maswahabah, wanafunzi wa Maswahabah na wengineo waliokuja baada yao wamesema maneno yenye maana kama hayo. Vilevile ndio madhehebu ya ath-Thawriy, Maalik, Abu Haniyfah na wengineo.

Baadhi ya Salaf wamesema:

“Zilizokatazwa ni zile zilizokuwa na kivuli na picha zenye kivuli hazina neno. Haya ni madhehebu batili. Hakuna yeyote anayeshuku kusemwa vibaya kwa pazia aliyoikemea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) iliokuwa na picha. Picha yake haikuwa na kivuli. Ukiongezea kwamba Hadiyth zilizosalia zilizosema kwa njia ya kuachia kuhusu kila picha.”[1]

Haafidhw [Ibn Hajar] amesema baada ya kutaja mukhtaswari wa maneno haya ya an-Nawawiy:

“Kinachotilia nguvu kuenea [kwa uharamu] kwa picha zilizo na kivuli na zisizokuwa na kivuli ni yale aliyopokea Ahmad kupitia kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ni nani miongoni mwenu atakayeondoka kwenda Madiynah na asiache sanamu lolote isipokuwa ahakikishe amelivunja wala picha isipokuwa ahakikishe anaifuta?”[2]

Bi maana akaipasue.

Ndani yake imekuja:

“Yeyote atakayerejea kutengeneza kitu katika haya basi amekufuru yale aliyoteremshiwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[3]

Yule atakayezingatia Hadiyth zilizotangulia, basi majulisho yake yatamdhihirikia kuenea kwa uharamu na kutokuwa na tofauti kati ya zile zenye kivuli na nyenginezo, kama yalivyotangulia hayo kuwekwa wazi.

[1] Sharh Muslim.

[2] Muslim (969), at-Tirmidhiy (1049), an-Nasaa´iy (2031), Abu Daawuud (3218) na Ahmad (01/87).

[3] Ahmad (01/87).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Jawaab al-Mufiyd fiy Hukm-it-Taswwiyr kutoka katika Majmuu´-ul-Fataawaa (04/216-217)
  • Imechapishwa: 28/03/2022