Kuhusu maneno yake katika Hadiyth ya Abu Twalhah na Sahl bin Haniyf:

“Isipokuwa iliyotandazwa kwenye nguo.”

Hapa kunabaguliwa aina ya picha zinazozuia kuingia kwa Malaika nyumbani na si picha yenyewe. Hayo yako wazi mtu akitazama mtiririko wa Hadiyth. Kinachokusudiwa ni pale ambapo michoro ya picha inakuwa kwenye nguo ambayo inadharauliwa na kutwezwa. Vivyo hivyo kuhusu mto unaotwezwa. Hivo ndivo inavyofahamisha Hadiyth ya ´Aaishah iliotangulia ambapo aliikata pazia na kuifanya kuwa mto mmoja au mito miwili.

Hadiyth ya Abu Hurayrah:

“Amrisha kichwa cha kinyago hicho kikatwe kiwe na umbile kama la mti. Amrisha pazia ikatwe na kufanywe mito miwili inayokanyagwa chini. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akafanya hivo.”[1]

Haijuzu ubaguaji huu kuufasiri juu ya picha katika nguo iliyoning´inizwa, iliowekwa kwenye mlango, ukuta na mfano wake. Hadiyth ya ´Aaishah iko wazi katika kukataza pazia kama hii na ulazima wa kuindosha au kuiharibu, kama ilivyotangulia kutajwa kwa matamshi yake.

Hadiyth ya Abu Hurayrah inaonyesha wazi juu ya kwamba mfano wa pazia kama hii inazuia kuingia kwa Malaika mpaka itandazwe chini au kikatwe kichwa cha kinyago kilicho na picha hiyo na kiwe kama na umbile la mti. Hadiyth zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hazigongani. Bali zinasadikishana. Vovyote zitakavyowezekana kuoanishwa kwa njia inayofaa ambayo haina dhuluma, basi italazimika na kutanguliza jambo hilo juu ya mfumo wa kuyapa nguvu na kufuta [moja kati ya maoni mawili], kama ilivyothibitishwa katika elimu ya Usuwl na Mustwalah-ul-Hadiyth. Imewezekana kuoanisha kati ya Hadiyth hizo mbili kwa yale tuliyoyataja. Himdi zote njema anastahiki Yeye. Haafidhw [Ibn Hajar] amerajihisha kuoanisha kati ya Hadiyth kwa yale tuliyoyataja punde na akasema:

“al-Khattwaabiy amesema: “Picha ambayo inawazuia Malaika kuingia nyumbani ni ile aina ya picha ambayo ni haramu kuimiliki. Nayo ni ile picha ambayo iko na roho ambayo haikukatwa kichwa au haikutwezwa.”[2]

[1] at-Tirmidhiy (2806) na Abu Daawuud (4158).

[2] Fath-ul-Baariy.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Jawaab al-Mufiyd fiy Hukm-it-Taswwiyr kutoka katika Majmuu´-ul-Fataawaa (04/215-216)
  • Imechapishwa: 28/03/2022