Ikiwa mtu atakuwa na shaka katika swalah yake akafanyia kazi yakini au kulingana na itakavyokuwa imembainikia – kutokana na upambanuzi tuliyoutaja – baadaye ikambainikia ya kwamba alilofanya ndio sawa na kwamba yeye hakuzidisha katika swalah yake na wala hakupunguza. Basi hapo itamdondokea kusujudu Sujuud ya kusahau kutokana na kauli iliyotangaa kutoka katika madhehebu [ya Hanaabilah]. Hili ni kwa kule kuondoka lile jambo linalowajibisha kusujudu, ambalo ni shaka. Inasemekana vilevile ya kwamba haitomdondokea ili amfedheheshe shaytwaan. Hili ni kutokana na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Na ikiwa atakuwa ameswali swalah kikamilifu nne, basi hio itakuwa ni fedheha kwa shaytwaan.”

Aidha ni kwa sababu atakuwa ameswali sehemu katika swalah hali ya kuwa ni mwenye shaka, na hii ndio kauli yenye nguvu zaidi.

Mfano wa hilo:

Mtu anaswali, kisha akawa na shaka katika Rak´ah kama ni ya pili au ya tatu na asibainikiwe na kitu kati ya hayo mawili. Hivyo akaifanya Rak´ah hiyo kuwa ya pili na akajengea swalah yake juu yake. Kisha baadaye ikambainikia ya kwamba kweli ilikuwa ni Rak´ah ya pili, basi Sujuud ya kusahau haimlazimu. Hii ndio kauli iliyotangaa katika madhehebu [ya Hanaabilah]. Na kauli ya pili tuliyotaja ni kwamba inamlazimu yeye kusujudu Sujuud ya kusahau kabla ya kutoa salamu kwa mujibu wa ile kauli tuliyoipa nguvu.

Sujuud ya kusahau kwa maamuma:

Pale imamu atakaposahau basi italazimika kwa maamuma kumfuata imamu katika Sujuud ya kusahau. Kutokana na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika si venginevyo imamu amewekwa ili afuatwe. Hivyo basi, msende kinyume naye.” mpaka pale aliposema “… na iwapo atasujudu, basi nanyi sujudini.”[1]

Ni mamoja ikiwa imamu atasujudu Sujuud ya kusahau kabla ya kutoa salamu au baada ya kutoa salamu, itakuwa ni wajibu kwa maamuma kumfuata. Isipokuwa tu ikiwa huyo mswaliji huyo amepitwa na baadhi ya Rak´ah. Katika hali hiyo hatomfuata katika Sujuud ya kusahau kutokana na udhuru utakaokuwa umetokea kwa yule ambaye amepitwa na Rak´ah kwa sababu haiwezekani kwake kutoa salamu na imamu wake. Kwa ajili hiyo yule maamuma atakamilisha yaliyompita kisha atoe salamu, halafu atasujudu Sujuud ya kusahau na kutoa salamu.

Mfano wa hilo:

Mtu amejiunga na imamu katika Rak´ah ya mwisho na imamu analazimika kusujudu Sujuud ya kusahau baada ya kutoa salamu. Hivyo pale ambapo imamu atatoa salamu, basi huyu ambaye amepitwa na Rak´ah atasimama ili kukamilisha na kulipa yaliyompita na wala hatosujudu pamoja na imamu. Pale atakapokamilisha swalah yake, atasujudu Sujuud ya kusahau baada ya kutoa salamu.

Pale ambapo maamuma – na si imamu – atasahau, hali ya kuwa hakupitwa na kitu chochote katika swalah, katika hali hii hana Sujuud ya kusahau juu yake. Kwa sababu kusujudu kwake katika hali hii kutampelekea kwenda kwake kinyume na imamu na kutakuwa kumepatikana upungufu katika kumfuata. Isitoshe Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) waliacha Tashahhud ya kwanza pale ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ameisahau na hawakukaa chini. Wakasimama pamoja na yeye na hawakukaa katika Tashahhud kwa sababu ya kuchunga kule kumfuata imamu na kutoenda naye kinyume.

Ikiwa amepitwa na kitu katika swalah na akawa amesahau kitu pamoja na imamu wake wakati anaswali pamoja naye au katika zile Rak´ah ambazo analipa baada yake. Katika hali hii haitomdondokea Sujuud ya kusahau. Itamlazimu kusujudu Sujuud ya kusahau baada ya yeye kulipa zile Rak´ah ambazo zitakuwa zimempita aidha kabla ya kutoa salamu au baada ya kutoa salamu kutokana na upambanuzi uliyotangulia.

Mfano wa hilo:

Maamuma amesahau kusema:

سبحان ربي العظيم

“Ametakasika Mola wangu aliyetukuka.”

katika Rukuu´ na hakupitwa na kitu chochote katika swalah, basi hatolazimika kusujudu Sujuud ya kusahau. Endapo atakuwa amepitwa na Rak´ah moja au zaidi,  basi atailipa halafu atasujudu Sujuud ya kusahau kabla ya kutoa salamu.

Mfano mwingine:

Maamuma anaswali Dhuhr na imamu wake. Wakati imamu aliposimama katika Rak´ah ya nne, basi yule maamuma alikaa chini akidhani ya kwamba ile ni Rak´ah ya mwisho. Lakini pale alipojua ya kwamba imamu amesimama na yeye akasimama. Ikiwa hakupitwa na kitu chochote katika swalah, basi itakuwa sio lazima kwake Sujuud ya kusahau. Na ikiwa alikuwa amepitwa na Rak´ah moja au zaidi, basi atazilipa na kutoa salamu, kisha atasujudu Sujuud ya kusahau kisha atatoa salamu.

[1] al-Bukhaariy na Muslim kutoka katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sujuud-us-Sahw, uk. 148-151
  • Imechapishwa: 07/04/2022