07. Hitimisho – mukhtaswari wa yaliyotangulia

Inatubainikia sisi kutokana na yaliyotangulia yafuatayo:

Wakati fulani Sujuud ya kusahau inakuwa kabla ya kutoa salamu na mara nyingine inakuwa baada ya kutoa salamu. Sujuud ya kusahua inakuwa kabla ya kutoa salamu katika sehemu mbili:

1 – Ikiwa kumetokea upungufu katika swalah. Hili ni kutokana na Hadiyth ya ´Abdullaah bin Buhaynah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisujudu Sujuud ya kusahau kabla ya salamu wakati alipoacha Tashahhud ya kwanza. Hadiyth hii imeshatajwa hapo juu kwa tamko lake.

2 – Ikiwa mtu atakuwa na shaka na wala asibainikiwe na moja kati ya mambo mawili. Hili ni kutokana na Hadiyth ya Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliamrisha yule ambaye amepatwa na shaka katika swalah yake na akawa hajui ameswali Rak´ah ngani, tatu au nne, atachukua ile idadi ya chini na kusujudu Sujuud ya kusahau kabla ya kutoa salamu. Hadiyth hii imeshatajwa hapo juu kwa tamko lake.

Sujuud ya kusahua inakuwa baada ya kutoa salamu katika sehemu mbili:

1 – Ikiwa mtu amezidisha katika swalah yake. Hili ni kutokana na Hadiyth ya ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) pale ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswali Dhuhr Rak´ah tano. Walipomkumbusha hili baada ya kutoa salamu akasujudu Sujuud mbili za kusahau kisha akatoa salamu. Wala hakubainisha ya kwamba Sujuud ni baada ya kutoa salamu kwa kuwa hakujua kwamba amezidisha isipokuwa baada ya kutoa salamu. Hili linafahamisha juu ya kuenea kwa hukumu vilevile. Aidha inajulisha pia ya kwamba kule mtu kusujudu kwa sababu ya kuzidisha inakuwa baada ya kutoa salamu, ni mamoja ikiwa alijua kule kuzidisha kabla ya kutoa salamu au baada ya kutoa salamu.

Miongoni mwa yanayohusiana na hayo ni pale ambapo mtu atatoa salamu kabla ya kumaliza swalah yake kwa kusahau, kisha baadaye akakumbuka na akaikamilisha swalah yake. Hapo atakuwa amezidisha salamu katikati ya swalah. Atatakikana kusujudu Sujuud ya kusahau baada ya kutoa salamu. Hili ni kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoa salamu katika swalah ya Dhuhr au ´Aswr baada ya Rak´ah mbili. Wakati walipomkumbusha akakamilisha swalah yake kisha akatoa salamu. Halafu akasujudu Sujuud ya kusahau kisha akatoa salamu.

2 – Ikiwa mtu amepatwa na shaka halafu ikambainikia moja kati ya mambo mawili. Hili ni kutokana na Hadiyth ya Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliamrisha kwa yule aliyepatwa na shaka katika swalah yake ajitahidi kutafuta usawa na hivyo ajengee juu ya hilo kisha atoe salamu halafu asujudu Sujuud ya kusahau kisha atoe salamu. Hadiyth hii imeshatajwa hapo juu kwa tamko lake.

Pale ambapo mtu atakosea kwa kusahau mara mbili katika swalah; sehemu moja ikamlazimikia yeye kusujudu Sujuud ya kusahau kabla ya kutoa salamu na sehemu ya pili ikamlazimikia yeye kusujudu Sujuud ya kusahau baada ya kutoa salamu. Wanazuoni wanasema ile ya kabla ya kutoa salamu ndio itatangulizwa, hivyo atasujudu Sujuud ya kusahau kabla yake.

Mfano wa hilo:

Mtu anaswali Dhuhr, akasimama katika Rak´ah ya tatu. Lakini hakukaa katika Tashahhud ya kwanza na badala yake akakaa katika Tashahhud katika Rak´ah ya tatu, akifikiria ya kwamba ndio Rak´ah ya pili. Kisha baadaye akakumbuka ya kwamba ni Rak´ah ya tatu, hivyo atasimama na kuswali Rak´ah moja. Kisha atasujudu Sujuud ya kusahau halafu atatoa salamu.

Mtu huyu ameacha Tashahhud ya kwanza, ambapo hukumu yake Sujuud inakuwa kabla ya kutoa salamu. Akazidisha kukaa katika Rak´ah ya tatu, ambapo Sujuud inakuwa baada ya kutoa salamu. Hivyo ile Sujuud ya kusahau kabla ya kutoa salamu ndio itatangulizwa juu ya ile ya baada ya salamu – na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

Ninamuomba Allaah atuwafikishe sisi na ndugu zetu waislamu kukifahamu Kitabu Chake na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuvifanyia kazi, kwa nje na kwa ndani, katika ´Aqiydah, ´ibaadah, mambo ya mua´alama na atupe mwisho mwema sote. Hakika Yeye ni Mwingi wa kutoa, Mkarimu.

Himdi zote njmea ni stahiki Yake Allaah. Swalah na amani zimwendee Mtume Wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sujuud-us-Sahw, uk. 151-153
  • Imechapishwa: 07/04/2022