05. Sababu ya tatu ambayo ni kuingiwa na shaka

03 – Kutilia shaka

Kuwa na shaka ni kutokuwa na uhakika kati ya mambo mawili ni lipi lililotokea. Shaka haizingatiwi katika ´ibaadah katika hali tatu:

1 – Ikiwa ni dhana tu na hana uhakika wa jambo hilo, kama vile wasiwasi.

2 – Ikiwa shaka hiyo itakithiri kwa mtu kwa kiasi ambacho hawezi kufanya ´ibaadah yoyote isipokuwa anapatwa na shaka.

3 – Ikiwa shaka hiyo inamjia baada ya kumaliza ile ´ibaadah. Shaka hiyo haizingatiwi muda wa kuwa hajakuwa na yakini juu ya hilo. Hivyo mtu atatendea kazi kwa mujibu wa vile inavopelekea yakini yake.

Mfano wa hilo:

Mtu ameswali Dhuhr. Wakati amepomaliza kuswali swalah yake akapatwa na shaka kama ameswali Rak´ah tatu au nne. Katika hali hii asizingatie shaka hii isipokuwa ikiwa atakuwa na yakini kuwa kweli ameswali Rak´ah tatu. Katika hali hiyo ataikamilisha swalah yake ikiwa hakujapita kitambo kirefu, kisha atatoa salamu, halafu atasujudu Sujuud ya kusahau na kutoa salamu. Endapo hakukumbuka isipokuwa baada ya kupita muda mrefu, basi atarudi kuswali swalah yake upya.

Kuhusu kutilia shaka mahali pengine mbali na hizi hali tatu, basi shaka hiyo itakuwa ni yenye kuzingatiwa.

Shaka ndani ya swalah inaweza kuwa katika hali mbili:

1 – Ikambainikia yeye moja katika mambo mawili. Hapa atafanyia kazi lile ambalo limembainikia. Atatakiwa kujengea swalah yake juu ya hilo, halafu atatoa salamu, kisha atasujudu Sujuud ya kusahau na kutoa salamu.

Mfano wa hilo:

Mtu anaswali Dhuhr na akatilia shaka juu ya Rak´ah aliyomo kama ni Rak´ah ya pili au ni ya tatu. Lakini akawa na dhana yenye nguvu ya kwamba ile Rak´ah ni ya tatu, basi ataifanya kuwa ni ya tatu. Baada ya hapo ataswali Rak´ah nyingine moja – ambayo inatimiza nne –akamilishe swalah yake halafu atasujudu Sujuud ya kusahau kisha ndio atoe salamu.

Dalili ya hilo:

Ni yale yaliyothibiti katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy na ya Muslim kutoka katika Hadiyth ya ´Abdullaah Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakapokuwa na shaka mmoja wenu katika swalah yake, basi ajitahidi lililo la sawa na aendelee kwa hilo. Baadaye atoe salamu kisha asujudu sijda mbili.”

Tamko hili ni la al-Bukhaariy.

2 – Isibainike kwake moja kati ya mambo mawili. Atafanyia kazi lile ambalo ni yakini, nalo ni kuchukua ile idadi ya chini. Atakamilisha swalah yake kujengea kwa hilo halafu atasujudu Sujuud ya kusahau kabla ya kutoa salamu kisha ndio atoe salamu.

Mfano wa hilo:

Mtu anaswali ´Aswr na akawa na shaka ni Rak´ah ngapi ameswali; ni mbili au tatu. Isibainike kitu kwake ya kwamba hii ni Rak´ah ya pili au ya tatu, basi atajaalia kuwa ni Rak´ah ya pili. Hivyo basi, atakaa Tashahhud ya kwanza kisha baada ya hapo aswali Rak´ah zingine mbili, halafu atasujudu Sujuud ya kusahau kisha atoe salamu.

Dalili ya hilo:

Ni yale aliyopokea Muslim kutoka kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakapokuwa na shaka mmoja wenu katika swalah yake na asijue [ni Rak´ah] ngapi ameswali, tatu au nne, basi atupilie mbali ile shaka na ajengee kwa lile aliloyakinisha katika moyo wake kisha asujudu Sujuud mbili kabla ya kutoa salamu. Ikiwa atakuwa ameswali Rak´ah tano, basi swalah yake itamfanyia uombezi. Na ikiwa atakuwa ameswali swalah kikamilifu nne, basi hio itakuwa ni fedheha kwa shaytwaan.”

Mfano wa shaka:

Mtu anapokuja na imamu amerukuu. Mtu huyo atapiga Takbiyrat-ul-Ihraam hali ya kuwa amesimama wima na kunyooka kisha arukuu. Na wakati atakapofanya hivyo, hatotoka nje ya hali tatu:

1 – Awe na yakini ya kwamba amemuwahi imamu kwenye Rukuu´ kabla ya kuinuka mahali hapo. Hapo atakuwa amewahi ile Rak´ah na kutadondoka kwake usomaji wa al-Faatihah.

2 –  Awe na yakini ya kwamba imamu aliinuka kutoka kwenye Rukuu´ kabla ya kumuwahi katika Rukuu´ hiyo. Hapo atakuwa amekosa ile Rak´ah.

3 – Awe na shaka kama alimuwahi imamu kwenye Rukuu´ akawa ni mwenye kuwahi ile Rak´ah au yule imamu aliinuka kutoka kwenye Rukuu´ kabla ya kumuwahi akawa ni mwenye kukosa ile Rak´ah. Iwapo itambainikia yeye moja kati ya hayo mawili, basi atafanyia kazi lile lililombainikia halafu atakamilisha swalah yake kisha atatoa salamu, halafu atasujudu Sujuud ya kusahau na kutoa salamu. Ikiwa hakupitwa na kitu chochote katika swalah, hapo hatakiwi kuleta Sujuud ya kusahau. Lakini ikiwa haitombainikia yeye moja kati ya mambo mawili, basi atatakiwa kutendea kazi lililo na yakini ambalo ni kwamba aliikosa ile Rak´ah. Hivyo basi, atatakiwa kukamilisha swalah yake na kusujudu Sujuud ya kusahau kabla ya kutoa salamu kisha atoe salamu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sujuud-us-Sahw, uk. 146-148
  • Imechapishwa: 07/04/2022