2 – Kupunguka

1 – Kupunguza nguzo:

Mwenye kuswali pale ambapo atapunguza nguzo katika swalah yake, ikiwa ni Takbiyrat-ul-Ihraam, basi swalah si sahihi. Ni mamoja ikiwa ameiacha kwa kusahau au kwa kukusudia. Kwa sababu swalah yake haikufungika. Ikiwa ni kitu kingine kisichokuwa Takbiyrat-ul-Ihraam na akawa amekiacha kwa kukusudia, basi swalah yake inabatilika. Endapo atakuwa ameiacha kwa kusahau, akifika mahali pake katika Rak´ah ile ya pili, basi itafutika ile Rak´ah ya kwanza [ambayo kulikosekana nguzo] na ile Rak´ah aliyomo sasa itasimama mahali pa ile ya kwanza. Endapo atakuwa hajafika mahali pale alipoacha ile nguzo, basi itamuwajibikia kurudi katika ile nguzo alioacha na ailete tena na kuendelea kuanzia hapo. Katika hali zote mbili ni wajibu kwake yeye kusujudu Sujuud ya kusahau baada ya salamu.

Mfano wa hilo:

Mtu amesahau sijda ya pili katika Rak´ah ya kwanza. Akakumbuka hilo wakati amekaa baina ya sijda mbili katika Rak´ah ya pili, ataifuta ile Rak´ah ya kwanza na ile Rak´ah ya pili itasimama mahali pa ile ya kwanza na ataizingatia kuwa ndio Rak´ah ya kwanza. Atakamilisha swalah yake halafu atatoa salamu kisha atasujudu Sujuud ya kusahau na kutoa salamu.

Mfano mwingine:

Mtu amesahau sijda ya pili na kukaa kabla yake katika ile Rak´ah ya kwanza. Akakumbuka hilo baada ya kuinuka kutoka katika Rukuu´ katika Rak´ah ya pili. Katika hali hii anatakiwa kurudi na kukaa, kisha asujudu halafu aendelee swalah yake kwa kujengea hapo. Baadaye atatoa salamu, halafu atasujudu Sujuud ya kusahau na kutoa salamu.

2 – Kupunguka jambo la wajibu katika swalah:

Mwenye kuswali akiacha jambo la wajibu katika mambo ya wajibu ya swalah kwa kukusudia, basi swalah yake inabatilika. Endapo itakuwa ni kwa kusahau na akakumbuka hilo kabla ya kuondoka mahali pake katika swalah, hivyo ataileta na wala hakuna kingine kinachomlazimu. Na endapo atakumbuka baada ya kuondoka mahali pake, lakini kabla ya kufika kwenye nguzo inayofuata, basi anatakiwa kurudi. Ataleta jambo hilo la wajibu, kisha atakamilisha swalah yake, halafu atatoa salamu, kisha atasujudu Sujuud ya kusahau na kutoa salamu. Na endapo atakumbuka baada ya kufika katika nguzo inayofuata, basi itakuwa imedondoka na wala hatorejea kwayo, isipokuwa ataendelea swalah yake. Atasujudu Sujuud ya kusahau kabla ya kutoa salamu.

Mfano wa hilo:

Mtu ameinuka kutoka katika sijda ya pili katika Rak´ah ya pili ili asimame kwenda katika Rak´ah ya tatu hali ya kuwa amesahau Tashahhud ya kwanza. Akakumbuka hilo kabla ya kuinuka, anatakiwa kubaki hapo na kuleta Tashahhud kisha ataendelea swalah yake na wala hakuna kingine kinachomlazimu. Ikiwa atakumbuka hilo baada ya kuinuka kabla ya kusimama wima, basi atarudi na kukaa na kuleta Tashahhud. Kisha ataendelea na swalah yake na kutoa salamu kisha asujudu Sujuud ya kusahau halafu atatoa salamu. Endapo atakumbuka hilo baada ya kusimama wima, basi Tashahhud itadondoka na wala hatorejea kwayo, isipokuwa atakamilisha swalah yake na kusujudu Sujuud ya kusahau kabla ya kutoa salamu.

Dalili ya hilo:

Ni yale aliyopokea al-Bukhaariy na wengineo kutoka kwa ´Abdullaah bin Buhaynah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaswalisha Dhuhr na akasimama katika Rak´ah mbili za kwanza na hakukaa katika ile Tashahhud ya kwanza na watu wakawa wamesimama pamoja naye. Wakati alipomaliza swalah na watu wakawa wanamsubiri Mtume atoe salamu, akapiga Takbiyr hali ya kuwa amekaa na akasujudu sijda mbili kabla ya kutoa salamu, kisha ndio akatoa salamu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sujuud-us-Sahw, uk. 144-146
  • Imechapishwa: 07/04/2022