05 – Sharti ya tano ya shaahadah – Ukweli

Sharti ya tano ni ukweli ambao kinyume chake ni uwongo. Maana yake ni kwamba aitamke shahaadah akiwa ni mkweli moyoni mwake na baadaye uafikiana na ulimi wake. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

أَحَسِبَ النَّاسُ أَن يُتْرَكُوا أَن يَقُولُوا آمَنَّا وَهُمْ لَا يُفْتَنُونَ وَلَقَدْ فَتَنَّا الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۖ فَلَيَعْلَمَنَّ اللَّـهُ الَّذِينَ صَدَقُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْكَاذِبِينَ

“Je, wanadhani watu kuwa wataachwa kwa kuwa wanasema “Tumeamini”, nao ndio wasijaribiwe? Hakika tuliwajaribu wale waliokuwa kabla yao na kwa yakini Allaah atawajulisha wale walio wakweli na kwa hakika atawajulisha waongo.”[1]

 Vilevile Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu wanafiki ambao waliisema kwa uwongo:

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَقُولُ آمَنَّا بِاللَّـهِ وَبِالْيَوْمِ الْآخِرِ وَمَا هُم بِمُؤْمِنِينَ يُخَادِعُونَ اللَّـهَ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَمَا يَخْدَعُونَ إِلَّا أَنفُسَهُمْ وَمَا يَشْعُرُونَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ فَزَادَهُمُ اللَّـهُ مَرَضًا ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ بِمَا كَانُوا يَكْذِبُونَ

“Miongoni mwa watu wako wasemao: “Tumemwamini Allaah na siku ya Mwisho hali ya kuwa si wenye kuamini. [Wanadhani kuwa] wanamhadaa Allaah na wale walioamini lakini hawahadai isipokuwa nafsi zao na wala hawahisi. Ndani ya nyoyo zao mna maradhi na Allaah akawazidishia maradhi na watapata adhabu iumizayo kwa waliyokuwa wakiyakadhibisha.”[2]

Mara nyingi Allaah anazitaja hali zao na kuwafichua. Allaah (Ta´ala) amefanya hivo kwa mfano katika Suurah al-Baqarah, Aal ´Imraan, an-Nisaa’, al-Anfaal, at-Tawbah na Suurah kamili juu yao na kadhalika.

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwa Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anh) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Hakuna yeyote anayeshuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kuwa Muhammad ni mja na Mtume Wake hali ya kuwa mkweli kutoka moyo wake, isipokuwa Allaah atamuharamishia Moto.”[3]

Ili shahaadah hii iweze kumuokoa mtu kutokana na Moto ameshurutisha mtu aitamke kikweli kutoka moyoni mwake. Kwa ajili hiyo ni upuuzi kuitamka peke yake pasi na kuafikiana na moyo.

[1] 29:2-3

[2] 2:8-10

[3] al-Bukhaariy (1/44) na Muslim (94).

  • Muhusika: ´Allaamah Haafidhw bin Ahmad al-Hakamiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ma´aarij-ul-Qabuul (1/336-337)
  • Imechapishwa: 27/01/2025