Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Sharti ya pili ni kuwa na akili na kinyume chake ni wendawazimu. Mwendawazimu kalamu yake imesimamishwa mpaka anapopata akili. Dalili ni Hadiyth:

“Kalamu imenyanyuliwa kwa watu aina tatu; aliyelala mpaka anapoamka, mtoto mpaka anapobaleghe na mwendawazimu mpaka anapopata akili.”[1]

MAELEZO

Sharti ya pili… – Miongoni mwa sharti za kusihi kwa swalah ni kuwa na akili. Ni lazima kwa mswaliji awe na akili. Amesema:

“… na kinyume chake ni wendawazimu.”

Swalah ya mwendawazimu haisihi mpaka awe na fahamu na irudi akili yake. Maneno yake:

“Mwendawazimu kalamu yake imesimamishwa mpaka anapopata akili.”

Wala siku ya Qiyaamah hatoadhibiwa kwa sababu ´ibaadah si yenye kumuwajibikia. Kuwajibishiwa ´ibaadah ni lazima ziwepo akili. Akili zikiweko basi ´ibaadah inakuwa yenye kumuwajibikia mtu. Akili ikiondoka kunaondoka jukumu la kuwajibishiwa ´ibaadah. Mwendawazimu ni yule ambaye ameondokwa na akili. Huyu kalamu yake imenyanyuliwa.

Vivyo hivyo kikongwe mchanganyikiwa ambaye ameshakuwa mtumzima sana. Huyu pia kalamu imenyanyuliwa kwake. Huyu ana hukumu moja kama mwendawazimu. Hakuna ´ibaadah yoyote inayomuwajibikia; si kuswali wala kufunga. Kwa ajili hiyo yule ambaye ana ndugu mtumzima kikongwe anabwabwaja swalah wala funga havimuwajibikii. Hafungiwi katika Ramadhaan wala hatolewi chakula. Kwa sababu kalamu yake imenyanyuliwa na hivyo ´ibaadah si yenye kumuwajibikia. Mtumzima kikongwe mchanganyikiwa mara nyingi akili yake hairudi mwishoni mwa uhai wake. Huu ndio umri dhalili ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliomba kukingwa nao. al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Sa´d bin Abiy Waqqaas (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema: “Takeni ulinzi kwa matamshi ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiomba ulinzi kwayo:

اللهم إني أعوذ بك من الجبن وأعوذ بك من البخل وأعوذ بك من أن أرد إلى أرذل العمر وأعوذ بك من فتنة الدنيا وعذاب القبر

“Ee Allaah! Hakika naomba ulinzi Kwako kutokamana na woga, naomba ulinzi Kwako kutokamana na ubakhili, naomba ulinzi Kwako kutokamana na kurudishwa katika umri dhalili, naomba ulinzi Kwako kutokamana na na fitina ya dunia na adhabu ya kaburi.”

Umri dhalili ni ule utuuzima unaompelekea mwenye nao katika kuchanganyikiwa na kuondokwa na akili. Hivyo yule mjuzi anarudi kuwa mjinga na anakuwa katika hali ya kutokuweza kupambanua, hawezi kutekeleza zile haki za Allaah zinazomlazimu na haja zake mwenyewe[2].

Hivyo yule ambaye amezimia. Ikiwa mtu amezimia kwa kipindi cha siku moja, siku mbili, siku tatu au chini ya hapo maoni sahihi ni kwamba akiamka baada ya hapo basi anatakiwa kulipa zile swalah zinazomlazimu. Yaziyd, ambaye ni mtumwa aliyeachwa huru wa ´Ammaar bin Yaasir, ameeleza:

“´Ammaar bin Yaasir mrumi alizimia katika Dhuhr, ´Aswr, Maghrib na ´Ishaa. Akaamka wakati wa nusu ya usiku ambapo akaswali Dhuhr, kisha Maghrib halafu ´Ishaa.”[3]

Siku zenye kuzidi siku tatu hazilipwi. Huyu kalamu yake imenyanyuliwa ambaye amelazwa kwenye koma/icu. Kulazimishiwa mtu ´ibaadah ni lazima ziwepo akili. Maneno yake:

“Dalili… “

juu ya kwamba akili ni sharti ya kusihi kwa swalah na kwamba mwendawazimu ´ibaabah hazimuwajibikii ni Hadiyth:

“Kalamu imenyanyuliwa kwa watu aina tatu; aliyelala mpaka anapoamka, mtoto mpaka anapobaleghe na mwendawazimu mpaka anapopata akili.”

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kalamu imenyanyuliwa kwa watu aina tatu… “

kunakusudiwa kalamu ya yule mtu ambaye ´ibaadah ni yenye kumuwajibikia.

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… aliyelala mpaka anapoamka, mtoto mpaka anapobaleghe na mwendawazimu mpaka anapopata akili.”

Watu sampuli hii tatu ´ibaadah si yenye kuwawajibikia. Kwa msemo mwingine ni kwamba endapo watafanya hivo hawapati dhambi. Lakini ni lazima kuwajibishwe juu ya kile watachoharibu. Kwa sababu dhamana imefungamana na kile kilichoharibiwa.

Ambaye amelala kalamu imenyanyuliwa kwake mpaka atakapoamka. Endapo mwanamke atamlalia mwanae mchanga ambapo akafa mwanamke huyo hapati dhambi. Lakini ni lazima kwake kutoa diya. Kadhalika mwendawazimu na mtoto mdogo wakiharibu kitu hawapati dhambi. Lakini hata hivyo ni lazima kuwajibishwe juu ya kile walichoharibu. Hiyo ina maana kwamba kama wako na mali basi kutachukuliwa kutoka katika mali yao. Vinginevyo walezi na wasimamizi wao ndio watawajibika.

[1] Abu Daawuud (4405) na Ahmad (1362). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (2/5).

[2] Sharh ”Swahiyh-ul-Bukhaariy” (10/120) ya Ibn Battwaal.

[3] Ameipokea ´Abdur-Razzaaq katika ”al-Muswannaf” (02/479).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 11-14
  • Imechapishwa: 06/12/2021