04. Mfano wa namna ambavo Ibn ´Abdil-Wahhaab hataji kitu isipokuwa kwa dalili

Mtunzi amesema:

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

مَا كَانَ لِلْمُشْرِكِينَ أَن يَعْمُرُواْ مَسَاجِدَ الله شَاهِدِينَ عَلَى أَنفُسِهِمْ بِالْكُفْرِ أُوْلَئِكَ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ وَفِي النَّارِ هُمْ خَالِدُونَ

“Si haki kwa washirikina kuamirisha misikiti ya Allaah hali ya kuwa wanajishuhudia nafsi zao kwa ukafiri. Hao yamebatilika matendo yao na katika Moto wao ni wenye kudumu.”[1]

Mtunzi (Rahimahu Allaah) ametumia dalili kwa Aayah hii ya kwamba matendo yake yote ni yenye kuharibika. Hiyo ina maana kwamba matendo yake yote ni batili na hayalipwi thawabu wala ujira. Miongoni mwa matendo ni swalah. Swalah yake haisihi mpaka ampwekeshe Allaah. Mtunzi amesema:

وَقَدِمْنَا إِلَى مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاء مَّنثُورًا

”Na Tutayaendea yale waliyoyatenda ya matendo yoyote yale na Tutayafanya kuwa ni mavumbi yaliyotawanyika.”[2]

Dhamiri katika:

إِلَى مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ

“… yale waliyoyatenda ya matendo yoyote yale… “

inarudi kwa makafiri. Amesema (Ta´ala):

فَجَعَلْنَاهُ هَبَاء مَّنثُورًا

“… na Tutayafanya kuwa ni mavumbi yaliyotawanyika.”

Bi maana tutayafanya hayana hukumu wala nafasi yoyote.

Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amepambanuka kwa njia ya kwamba hataji kitu isipokuwa kwa dalili. Dalili ima ikawa ni Aayah kutoka ndani ya Qur-aan au Hadiyth kutoka katika Sunnah takasifu. Madai hayakubaliwi isipokuwa kwa dalili. Pindi mayahudi waliposema:

لَن يَدْخُلَ الْجَنَّةَ إِلَّا مَن كَانَ هُودًا

 “Hatoingia Peponi isipokuwa aliyekuwa myahudi.”

Manaswara nao wakasema:

لَن يَدْخُلَ الْجَنَّةَ إِلَّا مَن كَانَ هُودًا أَوْ نَصَارَىٰ

“Hatoingia Peponi isipokuwa aliyekuwa myahudi au mnaswara.”

Allaah (Ta´ala) akasema:

قُلْ هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

“Sema: “Leteni ushahidi wenu, mkiwa ni wasema kweli.”[3]

[1] 09:17

[2] 25:23

[3] 02:111

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 10-11
  • Imechapishwa: 06/12/2021