05. Sharti ya nne ya swalah ni kuondoa hadathi

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Sharti ya nne ni mtu kuondosha hadathi, nako ni kule kutia wudhuu´ unaojulikana.

MAELEZO

Hadathi ni kila chenye kutoka katika njia mbili na kila kinachochengua wudhuu´. Hadathi ni ile hali inayowajibisha mtu kutia wudhuu´. Hadathi hugawanyika mara mbili:

1 – Hadathi kubwa: Ni ile inayowajibisha kuoga kama vile hali ya kuwa na janaba, hedhi na nifasi.

2 – Hadathi ndogo: Ni ile inayowajibisha wudhuu´.

Kuondoa hadathi kunafanyika kwa kuoga na kutia wudhuu´ kwa yule aliyepata maji au mwenye uwezo wa kuyatumia. Iwapo maji hayapo au yapo lakini mtu hana uwezo wa kuyatumia, basi atahamia kwenye kuondoa hadathi kubwa na ndogo kwa kufanya Tayammum.

Mtu akifanya Tayammum kwa ajili ya hadathi kubwa, kisha baadaye akapata maji, basi ataoga. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika udongo msafi ni twahara ya muislamu, hata kama hakupata maji kwa miaka kumi. Anapopata maji basi ayaweke kwenye ngozi yake, kwa kuwa kufanya hivyo ni bora zaidi.”

Ameipokea at-Tirmidhiy (124) na wengine kutoka kwa Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh). at-Tirmidhiy amesema:

”Hadiyth hii ni nzuri na Swahiyh.” Tazama pia ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (153).

Ikiwa mtu mwenye hadathi kubwa ataoga na akanuia kuondoa hadathi kubwa na ndogo, basi zote huondoka. Lakini akimimina maji mwilini katika kuoga ijumaa au kupata baridi kidogo na wakati huohuo akanuia kuondoa hadathi ndogo, basi hadathi hiyo haiondoki, kwa sababu kuoga huku hakuhusiani na kuondoa hadathi.

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 7-8
  • Imechapishwa: 30/04/2026