Himdi zote njema anastahiki Allaah. Amma baada ya hayo;

Huu ni muktasari mfupi wa namna ya kutekeleza ´ibaada ya ´Umrah:

Ambaye anataka kufanya ´Umrah atakapofika katika kituo basi inapendeza kwake kuoga na kujisafisha. Vivyo hivyo ndivo anavotakiwa kufanya mwanamke hata kama atakuwa mwenye hedhi au damu ya uzazi licha ya kwamba haifai kwake kutufu Ka´bah mpaka atwahirike na kuoga. Mwanamme atajitia manukato kwenye mwili wake na si katika yale mavazi ya Ihraam yake. Haina neno asipoweza kuoga kwenye kituo. Inapendeza pia kuoga atakapofika Makkah kabla ya Twawaaf ikiwepesika kufanya hivo.

Mwanamme anatakiwa kuepuka mavazi yote yaliyoshonwa na avae shuka ya juu na shuka ya chini. Inapendeza mavazi hayo yawe meupe na masafi. Kuhusu mwanamke atafanya Ihraam ndani ya mavazi yake ya kawaida yasiyokuwa na mapambo wala yenye kushuhurika. Kisha anuie kwa moyo wake kuingia katika ´ibaadah ya ´umrah na atamke kwa ulimi wake hali ya kusema:

لبيك عُمْرَةً

”Nakuitikia ´Umrah.”

au aseme:

اللَّهُمَّ لَبَيْكَ عُمْرَةً

”Ee Allaah, nakuitikia ´Umrah.”

Muhrim akiogopa kutotekeleza ´ibaadah yake kwa sababu ya mgonjwa, anaogopa n.k, basi imewekwa katika Shari´ah akaweka sharti katika kuhirimia kwake. Atasema:

فإِنْ حَبَسنِي حابسٌ فَمَحِلِّي حَيْثُ حَبَسْتَنِي

”Nikizuiwa na kizuizi, basi nitatoka Ihraam pale nilipozuilika.”

Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Dhwabaah bint az-Zubayr (Radhiya Allaahu ´anhaa).

Kisha ataleta Talbiyah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambayo ni:

لَبَّيْكَ اللَّهُمَّ لَبَّيْكَ، لَبَّيْكَ لا شَرِيكَ لَكَ لَبَّيْكَ، إنَّ الْحَمْدَ، وَالنِّعْمَةَ ،لَكَ وَالْمُلْكُ، لا شَرِيكَ لَكَ

”Nimekuitikia, ee Allaah, nimekuitikia. Nimekuitikia, huna mshirika, nimekuitikia. Hakika himdi zote njema, neema na ufalme ni Vyako. Huna mshirika.”

Ailete Talbiyah hii kwa wingi na kumtaja Allaah na kumuomba du´aa mpaka pale atakapofika katika Ka´bah.

Atakapofika katika msikiti Mkatatifu basi ataanza kuingia kwa mguu wake wa kulia kabla ya mguu wake wa kushoto na atasema:

بِسْمِ اللهِ وَالصَّلَاةِ وَالسَّلَامِ عَلَى رَسُولِ

”Naanza kwa jina la Allaah na swalah na amani zimwendee Mtume.”

أَعُوذُ بِاللَّهِ العَظِيمِ، وَبِوَجْهِهِ الْكَرِيمِ، وَسُلْطَانِهِ الْقَدِيمِ، مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ [بِسْمِ اللَّهِ، وَالصَّلَاةُ] [وَالسَّلَامُ عَلَى رَسُولِ اللَّهِ] اللَّهُمَّ افْتَحْ لِي أَبْوَابَ رَحْمَتِكَ

“Najilinda na Allaah mtukufu, kwa uso Wake mtukufu kutokamana na shaytwaan aliyefukuzwa mbali na rehema za Allaah. Kwa jina la Allaah, swalah na amani zimwendee Mtume wa Allaah. Ee Allaah! Nifungulie mimi milango ya rehema Zako.”

Atakapofika katika Ka´bah atasitisha Talbiyah kisha atakusudia jiwe jeusi, atalielekea kisha ataligusa kwa mkono wake wa kulia na kulibusu ikimsahilikia kufanya hivo. Asiwaudhi watu kwa msongamano. Atasema wakati wa kuligusa:

بسم الله والله أكبر

”Kwa jina Allaah, Allaah ni mkubwa.”

Ikiwa kuna ugumu kuibusu basi ataashiria kwa mkono wake, sehemu yake au mfano wa hayo mawili. Ikiwa kuna ugumu kuligusa basi ataashiria kwa mkono wake na kusema:

والله أكبر

”Allaah ni mkubwa.”

Asibusu kile anachokiashiria.

Ili Twawaaf iweze kusihi ni sharti mwenye kutufu awe na twahara kutokamana na hadathi kubwa na hadathi ndogo. Kwa sababu Twawaaf ni kama swalah ingawa tu mtu ameruhusiwa kuzungumza. Aifanye Ka´bah upande wa kushotoni mwake na azunguke mara saba. Anapokuwa sambamba na kona ya upande wa yemeni basi ataigusa kwa mkono wake wa kuume ikimsahilikia kufanya hivo na atasema:

بسم الله والله أكبر

”Kwa jina Allaah, Allaah ni mkubwa.”

na asiibusu. Ikiwa ni vigumu kwake kuigusa basi ataiacha na ataendelea na Twawaaf yake na wala asiiashirie na wala asilete Takbiyr. Kwa sababu mambo hayo hayakunakiliwa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuhusu jiwe jeusi kila ambapo atapokuwa sambamba nalo ataligusa na kulibusu, kama tulivyotangulia kusema mwanzoni. Vinginevyo ataliashiria na kuleta Takbiyr.

Inapendeza kuchapuka – nako ni kule kutembea haraka na kukaribiana hatua za miguu – katika ile mizunguko mitatu ya mwanzo ya Twawaaf ya kufika. Hili ni kwa wanamme peke yao. Katika Twawaaf ya kufika inapendeza pia kwa mwanamme kuweka katikati shuka yake ya juu chini ya bega lake la kulia na ncha zake juu ya bega lake la kushoto katika mizunguko yote.

Inapendeza kufanya Dhikr na kuomba du´aa kwa wingi katika mizunguko yote kwa yale yatakayomsahilikia mtu. Hakuna du´aa wala Dhikr maalum ya Twawaaf. Bali aombe na amtaje Allaah kwa yale yatayomkuwia mepesi katika Adhkaar na du´aa. Atasema baina ya upande wa nguzo ya yemeni na jiwe jeusi:

ربنا آتنا في الدنيا حسنة وفي الآخرة حسنة وقنا عذاب النار

“Ee Mola wetu! Tupe duniani wema na Tupe Aakhirah wema na tukinge na adhabu ya Moto.”[1]

Atasema hivo katika kila mzunguko. Hilo limethibiti kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Atakamilisha mzunguko wa saba kwa kuligusa jiwe jeusi na kulibusu ikimuwepesikia, au kuliashiria kwa mkono pamoja na kuleta Takbiyr kutokana na ule ufafanulizi tuliotaja punde kidogo. Baada ya kumaliza kwake Twawaaf hii, atavaa shuka yake ya juu na kuiweka juu ya mabega yake na ncha yake juu ya kifua chake.

Kisha ataswali Rak´ah mbili nyuma ya nafasi aliposimama Ibraahiym ikimsahilikia kufanya hivo. Lisipomuwezekania hilo basi ataziswali maeneo yoyote ya msikiti na baada ya al-Faatihah katika Rak´ah ya kwanza atasoma ”al-Kaafiruun” na katika Rak´ah ya pili atasoma ”al-Ikhlaasw”. Kufanya hivi ndio bora zaidi. Hapana ubaya akisoma nyenginezo. Kisha baada ya kumaliza hizo Rak´ah mbili atalikusudia jiwe jeusi ikimuwepesikia kufanya hivo.

Kisha atatoka kwenda kupanda mlima wa Swafaa au kusimama pembezoni mwake. Akiweza kupanda ndio bora zaidi na atasoma maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَآئِرِ اللّهِ

“Hakika vilima vya Swafaa na Marwah ni katika alama za Allaah.”[2]

Inapendeza aelekee Qiblah, amuhimidi Allaah, kumtukuza na aseme:

الله أكبر لا إله إلا الله وحده لا شريك له له الملك وله الحمد يحيي ويميت وهو على كل شيء قدير

لا إله إلا الله وحده لا شريك له أنجز وعده ونصر عبده وهزم الأحزاب وحده

“Allaah ni mkubwa. Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa peke yake hana mshirika. Ufalme ni Wake Yeye na himdi zote ni Zake Yeye. Anahuisha na Anafisha. Naye juu ya kila jambo ni muweza. Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa peke yake hana mshirika. Ameitimiza ahadi Yake, amemnusuru mja Wake na amevishinda vikosi hali ya kuwa peke yake.”

Kisha ataomba kwa yale yenye kumsahilikia hali ya kunyanyua mikono yake, aikariri Dhikr na du´aa hii mara tatu.

Kisha atashuka na kutembea kwenda Marwah mpaka pale atakapofika sehemu yenye alama ya kwanza [mataa ya kijani]. Imesuniwa kwa mwanamme kutembea kwa haraka mpaka pale atakapofika katika alama ya pili. Kuhusu mwanamke haikusuniwa kwake kutembea kwa haraka. Kwa sababu mwanamke ni uchi. Kisha atatembea na kupanda mlima wa Marwah au kusimama karibu nao ingawa bora ni kupanda ikisahilika kufanya hivo. Atasema na kufanya  hapo Marwah yale aliyosema na kuyafanya Swafaa. Kisha atashuka na kutembea mahali pa kutembea na kutembea kwa haraka mahali pa kutembea kwa haraka mpaka atakapofika Swafaa. Atafanya hivo kwenda na kurudi mara saba. Akifanya Say´ kwa kupanda kipando hapana vibaya na khaswa ikiwa mtu anahitaji kufanya hivo. Inapendeza wakati wa kufanya kwake Say´ kufanya Dhikr na kuomba du´aa kwa wingi kwa yale yatayomkuwia mepesi. Anatakiwa awe ametwahirika kutokana na hadathi kubwa na hadathi ndogo. Itasihi endapo atafanya Say´ pasi na twahara.

Akikamilisha Say´ yake mwanamme ima atanyoa au atapunguza nywele zake ingawa kunyoa ndio bora zaidi. Ikiwa amefika Makkah karibu na wakati wa kufanya hajj, basi kupunguza ndio bora ili baadaye kipindi cha hajj anyoe kichwa kizima. Kuhusu mwanamke atazikusanya nywele zake na kukata kiasi cha kidole na chini ya hapo.

Muislamu akifanya yaliyotajwa basi ´Umrah yake itakuwa imetimia na itafaa kwake kufanya kila kitu ambacho kilikuwa ni haramu kwake wakati wa Ihraam.

[1] 02:201

[2] 02:158

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min A´maal Ramadhwaan, uk. 09-13
  • Imechapishwa: 02/04/2023