Ni kuamini kwa kukata na kusadikisha kuwepo kwa Malaika, kwamba ni viumbe vilivyo na dhati zinazohisiwa ambavyo vinakwenda na kurudi, kupanda na kushuka, vinaona na kumzungumzisha Mtume wa Allaah. Sio maumbo yenye kung´aa wala mambo ya kimaana, kama wanavosema wanafalsafa. Aidha ni lazima kuamini fadhilah na nafasi yao mbele ya Allaah, kwamba ni waja watukufu wasiomuasi Allaah kwa yale anayowaamrisha na wanafanya yale wanayoamrishwa. Vilevile ni lazima kuamini kazi zao na sampuli zao kutegemea na vile Allaah alivyowapa na kwamba miongoni mwao kuna wabebaji wa ´Arshi. Amesema (Ta´ala):

الَّذِينَ يَحْمِلُونَ الْعَرْشَ وَمَنْ حَوْلَهُ

“Ambao wanabeba ‘Arshi na walio pembezoni mwake.”[1]

وَيَحْمِلُ عَرْشَ رَبِّكَ فَوْقَهُمْ يَوْمَئِذٍ ثَمَانِيَةٌ

“Watabeba ‘Arshi ya Mola wako juu yao siku hiyo [Malaika] wanane.”[2]

Miongoni mwao kuna waliokurubishwa. Miongoni mwao kuna waliopewa kazi ya jua,  wengine wamepewa kazi ya mwezi. Wengine wamepewa kazi ya nyota. Wengine wamepewa kazi ya nyota. Wengine wamepewa kazi ya mvua ambayo ndio uhai wa wanaadamu, wanyama na mimea. Wengine wamepewa kazi ya Pepo na kuwaandalia neema wakazi wake. Wengine wamepewa kazi ya Moto, kuuwasha na kuwaandalia adhabu wenye nayo. Wengine wamepewa kazi ya tone la manii na kusimamia jambo lake mpaka likamilike umbile lake. Wako ambao wamepewa kazi ya kumuhifadhi mwanadamu. Amesema (Ta´ala):

لَهُ مُعَقِّبَاتٌ مِّن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ يَحْفَظُونَهُ مِنْ أَمْرِ اللَّـهِ

“Ana Malaika wanaofuatana kwa zamu mbele yake na nyuma yake wanamhifadhi kwa amri ya Allaah.”[3]

وَإِنَّ عَلَيْكُمْ لَحَافِظِينَ

“Hakika juu yenu bila shaka kuna wenye kuhifadhi.”[4]

Wako ambao wamepewa kazi ya kuandika matendo ya viumbe mema na maovu. Amesema (Ta´ala):

إِذْ يَتَلَقَّى الْمُتَلَقِّيَانِ عَنِ الْيَمِينِ وَعَنِ الشِّمَالِ قَعِيدٌ مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ

“Pale wanapopokea wapokeaji wawili wanaokaa kuliani na kushotoni. Hatamki maneno yoyote isipokuwa anaye mchungaji aliyejitayarisha [kurekodi].”[5]

Wengine wamepewa kazi ya kuzitoa roho kutoka kwenye viwiliwivili vyake. Amesema (Ta´ala):

حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ تَوَفَّتْهُ رُسُلُنَا

“… mpaka kinapomfikia mmoja wenu kifo, basi wajumbe Wetu.”[6]

قُلْ يَتَوَفَّاكُم مَّلَكُ الْمَوْتِ الَّذِي وُكِّلَ بِكُمْ

“Sema: “Atakufisheni Malaika wa mauti ambaye amewakilishwa kwenu.”[7]

Wengine wamepewa kazi ya kupuliza baragumu ambaye ni Israafiyl (´alayhis-Swalaatu was-Salaam). Akipuliza kwa mara ya pili basi roho zitarudi kwenye viwiliwili vyake, viwiliwili vitafufuliwa na kutolewa kwenye makaburi kwa ajili ya hesabu na malipo. Wengine wamepewa kazi ya kuwaletea Mitume Wahy ambao ndio unazihuisha nyoyo na roho.

Viongozi wa Malaika ni watatu; Jibriyl, Mikaaiyl na Israafiyl. Ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaomba kwa uola wa Allaah kupitia Malaika hawa watatu katika du´aa yake ya kufungulia swalah katika Hadiyth Swahiyh ambayo ameipokea Imaam Muslim ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anaposimama usiku husema baada ya kuleta Takbiyr:

اللَّهُمَّ رَبَّ جِبْرِيلَ وَمِيكَالَ وَإِسْرَافِيلَ فَاطِرَ السَّمَواتِ والأَرْضِ عَالِمَ الْغَيْبِ والشَّهَادَةِ أَنْتَ تَحْكُمُ بَيْنَ عِبَادك فِيما كانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ اهْدِنِي لِمَا اخْتُلِفَ فِيهِ مِنَ الْحَقِّ بإِذْنِكَ إِنَّكَ تَهْدِي مَنْ تَشَاءُ إِلى صِرَاطٍ مُسْتَقِيم

“Ee Allaah! Mola wa Jibriyl, Mikaaiyl na Israafiyl! Muumba wa mbingu na ardhi! Wewe ambaye ni Mjuzi wa mambo yenye kujificha na yalio ya wazi! [Siku moja] utahukumu baina ya waja Wako katika mambo ambayo walikuwa wakitafautiana! Niongoze mimi katika haki katika yale waliotafautiana kwa idhini Yako – Hakika Wewe unamuongoza umtakaye katika njia ilionyoka.”[8]

[1] 40:07

[2] 69:17

[3] 13:11

[4] 82:10

[5] 50:17-18

[6] 06:61

[7] 32:11

[8] Muslim (770).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Iymaan – Haqiyqatuhu wa Nawaaqidhwuh, uk. 10-12
  • Imechapishwa: 20/03/2023