Miongoni mwa majanga ni watu kupuuza duara za kielimu na kutofaidika kutoka katika Khutbah za ijumaa. Matokeo yake mjinga anazidi kuwa mjinga na watu wanaghafilika zaidi. Hivyo mioyo inagonjweka, inapuuza utajo wa Allaah na kujiepusha na haki kwa sababu ya kukusanyikiwa juu yake na madhambi.  Mtu anapotenda dhambi yoyote, basi kunaota juu ya moyo wake doa nyeusi. Hivo ndivo alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akitunu na akarudi basi linaondoka. Akiendelea katika madhambi basi doa linazidi kuwa kubwa na dhambi juu ya dhambi nyingine mpaka moyo unakuwa mweusi na inatawaliwa na kutu. Hii ndio maana ya maneno Yake (Jalla wa ´Alaa):

كَلَّاۖ بَلْۜ رَانَ عَلَىٰ قُلُوبِهِم مَّا كَانُوا يَكْسِبُونَ

“Sivo hivyo! Bali imefanya kutu juu ya nyoyo zao yale waliyokuwa wakiyachuma.”[1]

Bi maana kutokana na madhambi na maasi.

Mtu akichukulia wepesi maasi na madhambi yakawa mengi juu ya moyo wake moyo wake huwa mweusi na ukapinduliwa juu chini kiasi cha kwamba hatambui mema na hakatazi maovu. Kwa hivyo ni lazima kutahadhari na shari ya madhambi. Ni lazima daima kulazimiana na tawbah.

Mtu anatakiwa kupupia duara za elimu, kusikiliza Khutbah zenye faida, ndugu kukumbushana na kusoma vitabu yenye manufaa akiwa ni mwenye kujua kusoma ili afaidike kheri juu ya kheri, nuru juu ya nuru na elimu juu ya elimu. Muhimu zaidi kuliko hayo ni kutilia umuhimu Qur-aan tukufu na kuisoma kwa wingi na kumsikiliza anayeisoma. Kwa sababu Allaah (Subhaanah) ameifanya kuwa nuru, mwongozo na shifaa ya maradhi. Amesema (Subhaanah):

إِنَّ هَـٰذَا الْقُرْآنَ يَهْدِي لِلَّتِي هِيَ أَقْوَمُ

“Hakika hii Qur-aan inaongoza katika yaliyonyooka kabisa.”[2]

قُلْ هُوَ لِلَّذِينَ آمَنُوا هُدًى وَشِفَاءٌ

“Sema: “Hiyo ni kwa walioamini ni mwongozo na shifaa.””[3]

كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ لِّيَدَّبَّرُوا آيَاتِهِ وَلِيَتَذَكَّرَ أُوْلُوا الْأَلْبَابِ

“Kitabu Tumekiteremsha kwako chenye baraka ili wapate kuzingatia kwa makini Aayah zake na ili wapate kukumbuka wale wenye akili.”[4]

Zipo Aayah nyingi zenye maana kama hii.

Katika Hadiyth Swahiyh imepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Isomeni Qur-aan hii. Hakika itakuja hali ya kumfanyia uombezi wenye nayo siku ya Qiyaamah.”[5]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Maana yake ni kwamba itawafanyia uombezi wenye nayo ambao walikuwa wakiitendea kazi duniani. Hivo ndivo alivobainisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth nyingine:

“Qur-aan italetwa siku ya Qiyaamah na watu wake ambao walikuwa wakiitendea kazi duniani. Wakitangulizwa mbele na Suurah “al-Baqarah” na “Aal ´Imraan” kama vile mawingu mawili, pazia mbili au makundi mawili ya ndege wakikunjua [mbawa zao] zitawatetea watu wao.”[6]

Ameipokea Muslim pia katika “as-Swahiyh” yake.

Amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yeyote atakayesoma herufi moja ndani ya Qur-aan, basi anapata kwayo jema moja. Jema moja linalipwa kwa kumi mfano wake. Sisemi kuwa “Alif Laam Miym” (الم) ni heruf moja. Lakini “Alif” ni harufi moja, “Laam” ni herufi na “Laam” ni herufi nyingine.”[7]

Zipo Aayah nyingi zenye maana kama hii.

[1] 83:14

[2] 17:09

[3] 41:44

[4] 38:29

[5] Muslim (1337) na Ahmad (21186).

[6] Muslim (1338) na Ahmad (21126).

[7] at-Tirmidhiy (2835).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 48-50
  • Imechapishwa: 30/11/2021