05. Kipi afanye mtu akiwaamrisha familia yake kuswali lakini wasimuitikie?

Swali 05: Kipi afanye mtu akiwaamrisha familia yake kuswali lakini wasimuitikie? Je, aishi pamoja nao na kuchanganyika nao au atoke ndani ya nyumba?

Jibu: Ikiwa wanafamilia hawa hawaswali kabisa, basi ni makafiri na wenye kuritadi. Wametoka nje ya Uislamu na haijuzu kuishi pamoja nao. Lakini ni lazima kwake kuwalingania, kuwang´ang´ania na akariri pengine Allaah akawaongoza. Kwa sababu mwenye kuacha swalah ni kafiri – na naomba ulinzi kwa Allaah. Hilo lina dalili ya Qur-aan, Sunnah, maneno ya Maswahabah na utafiti sahihi. Kuhusu ndani ya Qur-aan Tukufu Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu washirikina:

فَإِن تَابُوا وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ فَإِخْوَانُكُمْ فِي الدِّينِ

“Wakitubu na wakasimamisha swalah na wakatoa zakaah, basi ni ndugu zenu katika dini.”[1]

Kwa maana nyingine Aayah inasema wasipotekeleza swalah basi sio ndugu zenu. Udugu haukatiki kwa maasi, hata yakiwa makubwa kiasi gani, lakini udugu unakatika wakati mtu anapotoka katika Uislamu.

Kuhusiana na Sunnah Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Baina ya mtu na kufuru na shirki ni kuacha swalah.”[2]

Amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth ya Buraydah:

“Ahadi iliopo kati yetu sisi na wao ni swalah. Hivyo basi, yeyote atakayeiacha amekufuru.”[3]

Ama maneno ya Maswahabah, amesema Kiongozi wa waumini ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh):

“Hana fungu katika Uislamu kwa yule mwenye kuacha swalah.”

Kwa sababu makanusho yamekuja kwa njia ya uhakika, basi ni yenye kuenea; si fungu kubwa wala dogo. ´Abdullaah bin Shaqiyq amesema:

“Hakuna kitu katika matendo Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakiona kukiacha ni ukafiri isipokuwa swalah.”

Kuhusu mtazamo sahihi kunasemwa: je, inaingia akilini kwa mtu ambaye moyoni mwake mna imani sawa na mbegu ya haradali, anajua utukufu wa swalah, namna Allaah alivyoitilia umuhimu, kisha asiichunge? Nimezingatia dalili za wale ambao hawaonelei mwenye kuacha swalah hakufuru, na nikaona kuwa hazitoki nje ya maoni manne:

1 – Hakuna dalili katika msingi wake.

2 – Zimefungamanishwa na sifa zinazokanusha kuacha swalah.

3 – Zimefungamanishwa na hali ya kumpa udhuru mwenye kuacha swalah.

4 – Zimekuja kwa njia ya kuenea na hivyo zikafanywa maalum na Hadiyth kuhusu ukafiri wa mwenye kuacha swalah.

Ikishabainika kuwa ambaye anaacha swalah ni kafiri, basi anafuatiwa na hukumu zifuatazo:

1 – Si sahihi kumuozesha. Akiozeshwa ilihali haswali, basi ndoa inazingatiwa ni batili na mwanamke huyo si halali kwake. Hilo ni kutokana na maneno Yake (Ta´ala) kuhusu wale wanawake waliohama:

لَا هُنَّ حِلٌّ لَّهُمْ وَلَا هُمْ يَحِلُّونَ لَهُنَّ

“Wao [wanawake wa kiislamu] si halali kwao [hao makafiri] na wala wao [waume] si halali kwao.”[4]

Akiacha swalah baada ya kuozeshwa, basi ndoa yake inafutika na mwanamke huyo si halali kwake. Dalili ya hilo ni Aayah ambayo tumeitaja punde.

2 – Mtu huyu ambaye haswali akichinja basi hakitoliwa kichinjwa chake. Kwa nini? Kwa sababu ni haramu. Hata hivyo endapo myahudi au mkristo atachinja basi vichinjwa vyao ni halali kwetu kuvila. Kwa hivyo kichinjwa chake kinakuwa kibaya zaidi kuliko kichinjwa cha myahudi na mkristo.

3 – Si halali kwake kuingia Makkah au mipaka yake mitakatifu. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْمُشْرِكُونَ نَجَسٌ فَلَا يَقْرَبُوا الْمَسْجِدَ الْحَرَامَ بَعْدَ عَامِهِمْ هَـٰذَا

”Enyi walioamini! Hakika washirikiana ni najisi, hivyo basi wasikaribie al-Masjid al-Haraam baada ya mwaka wao huu.”[5]

4 – Akifariki mmoja katika ndugu zake, basi hana haki ya kumrithi. Ni nani anayemrithi muislamu aliyekufa, hata hivyo anaye mtoto ambaye haswali na anaye binamu wa mbali anayeswali? Atamrithi huyo binamu yake wa  mbali. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika Hadiyth ya Usaamah:

“Muislamu hamrithi kafiri wala kafiri hamrithi muislamu.”[6]

5 – Akifa, basi hatooshwa wala hatovikwa sanda. Aidha hatoswaliwa wala hatozikwa na waislamu. Tumfanye nini sasa? Tutatoka naye jangwani na kumchimbia shimo na kumzika akiwa na nguo yake, kwa sababu hana heshima yoyote. Kujengea juu ya hili haifai kwa mtu ambaye amefiwa na ndugu na yeye anatambua kuwa mtu huyo haswali, akamleta kwa waislamu wamswalie.

6 – Atafufuliwa siku ya Qiyaamah akiwa na Fir´awn, Haamaan, Qaaruun na Ubayy bin Khalaf[7] – na naomba ulinzi kwa Allaah. Aidha hatoingia Peponi na si halali kwa yeyote katika familia yake kumuombea du´aa ya rehema na msamaha, kwa sababu ni kafiri na hastahiki kuombewa hivo.

Enyi ndugu! Suala hili ni la khatari sana. Kwa masikitiko tunaona baadhi ya watu wanachukulia wepesi suala hili na wanawakubali wanafamilia wasioswali. Kitendo hichi hakijuzu na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

[1] 09:11

[2] at-Tirmidhiy ambaye amesema:

”Hadiyth hii ni nzuri na Swahiyh.”

[3] an-Nawawiy amesema:

”Ameipokea at-Tirmidhiy katika “Kitaab-ul-Iymaan” kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.”

[4] 60:10

[5] 09:28

[6] al-Bukhaariy na Muslim.

[7] Ahmad (6288) na ad-Daarimiy (2605).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah Muhimmah, uk. 10-14
  • Imechapishwa: 26/02/2023