04. Je, inafaa kwa mtu kutoka kwenda kuswali msikitini na akawaacha watoto wake nyumbani?

Swali 04: Je, inafaa kwa mtu kutoka kwenda kuswali msikitini na akawaacha watoto wake nyumbani?

Jibu: Ni lazima kwa mtu kutekeleza amri ya Allaah (´Azza wa Jall) pale aliposema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَائِكَةٌ غِلَاظٌ شِدَادٌ لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ

“Enyi mlioamini! Jikingeni nafsi zenu na familia zenu na Moto ambao mafutayake ni watu na mawe; juu yake wako Malaika wakali, shadidi hawamuasi Allaah kwa yale anayowaamrisha na wanafanya yale wanayoamrishwa.”[1]

Ni lazima kwa mtu kuwaamrisha familia yake kuswali. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanya hivo pale aliposema:

“Waamrisheni watoto wenu kuswali wanapokuwa na miaka saba na wapigeni kwayo wanapokuwa na miaka kumi na watenganisheni kwenye malazi.”[2]

Kadhalika Allaah (Ta´ala) ametaja kuwa Ismaa´iyl, ambaye ndiye baba wa waarabu:

وَكَانَ يَأْمُرُ أَهْلَهُ بِالصَّلَاةِ وَالزَّكَاةِ وَكَانَ عِندَ رَبِّهِ مَرْضِيًّا

”Na alikuwa akiwaamrisha ahli zake swalah na zakaah na alikuwa mridhiwa mbele ya Mola wake.”[3]

Haifai kwake kuwaacha watoto wake wanalala pasi na kuwaamsha kuswali na akawachunga. Haitoshi kuwaamsha peke yake, bali ni lazima kuwafuatilia. Pengine akawaamsha kisha wakarudi kulala. Ama kitendo cha yeye kutoka kwenda msikitini akawaacha nyumbani kwa sababu anachelea asipitwe na swalah ikiwa atabaki nyumbani na kuwachunga, anatakiwa kutoka kwenda kuswali kisha awarudilie. Hata hivyo akiwa ni mwenye kupuuza na anawaamsha pale anapotaka kutoka na hazumgumzi isipokuwa mara moja au mara mbili na anasema kuwa anachelea asije kupitwa na swalah, hakika kitendo hicho kinazingatiwa ni uzembe anaofanya. Bali analazimika kuwaamsha kutegemea na hali zao; kama wana uzito wa kuamka basi anapaswa kuwaamsha mapema na kinyume chake.

[1] 66:06

[2] Ahmad na Abu Daawuud.

[3] 19:55

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah Muhimmah, uk. 10
  • Imechapishwa: 26/02/2023