Himdi zote njema ni stahiki ya Allaah. Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wote.
Ama baada ya hayo;
Hakika umekufikieni mwezi mtukufu na msimu mtukufu. Nao si mwengine ni mwezi wa swadaqah na kisimamo, mwezi wa Ramadhaan ambao ndani yake ndio kumeteremshwa Qur-aan. Ni mwezi wa kusoma Qur-aan, mwezi wa swadaqah, mwezi wa wema, mwezi wa ihsani, mwezi wa kulisha chakula, mwezi wa kuwafajiri mafukara, masikini, wajane na mayatima. Ni mwezi mtukufu na uliobarikiwa. Allaah amejaalia ndani yake ´ibaadah mbalimbali zenye fadhilah na matendo matukufu yasiyokuwa katika miezi mingine. Mwezi wa Ramadhaan inang´aa nuru za Qur-aan na kuhisiwa harufu nzuri ya manukato ya Pepo. Ni mwezi wa utakatifu, baraka na rehema. Ni mwezi ambao kunasemwa makumi, mema yanalipwa maradufu na hupandishwa ngazi. Katika kila usiku kuna watu wanaachwa huru na Moto.
Ni lazima kwetu kufurahikia mwezi wa Ramadhaan na kuupokea kwa tawbah ya kweli na matendo mema. Hakika kufikiwa na mwezi wa Ramadhaan, kuweza kuufunga na matendo mema ndani yake ni neema kubwa kwa ambaye Allaah atamuwezesha juu yake. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwapongeza Maswahabah zake kwa kufikiwa na mwezi wa Ramadhaan. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:
“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwapa bishara njema Maswahabah zake kwa kufika mwezi wa Ramadhaan na akisema:
“Umekujieni mwezi wa Ramadhaan – ni mwezi wenye baraka. Allaah amekufaradhishieni kufunga. Ndani yake milango ya Pepo hufunguliwa, milango ya Moto hufungwa na mashaytwaan waovu hutiwa pingu. Humo Allaah ana usiku ambao ni bora kuliko miezi elfu moja. Mwenye kunyimwa kheri zake kwa kweli amenyimwa.”
Ameipokea Ahmad na an-Nasaa´iy[1].
Wanazuoni wamesema kuwa Hdiyth hii ndio msingi juu ya kitendo cha watu kupongezana kwa mwezi wa Ramadhaan.
´Ubaadah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:
“Imekujieni Ramadhaan – ni mwezi wa baraka na humo mna kheri. Allaah huwafunikeni, huteremsha rehema, hufuta madhambi na huitikia du´aa ndani yake. Allaah hutazama namna mnavyoshindana ndani yake na hujifakhari kwenu mbele ya Malaika Zake. Kwa hivyo muonyesheni Allaah yale mazuri yenu. Hakika mla khasara ni yule mwenye kunyimwa rehema za Allaah.”
Ameipokea at-Twabaraaniy na wapokezi wake ni waaminifu[2].
Kwa hivyo upokeeni mwezi wa Ramadhaan kwa nia njema na maazimio ya uongofu, matakwa na furaha. Aidha upokeeni kwa nafsi zilizotayarishwa kuupokea kwa tawbah ya kweli na iliyoenea na kukamilika. Vilevile upokeeni kwa kudhamiria kufanya mema na kujiepusha na mabaya. Upokeeni pia kwa kunuia kufunga swawm yenye kuhisiwa na swawm ya kimaana. Swawm yenye kuhisiwa kwa kujiepusha na vile vifunguzi na swawm ya kimaana ni kwa kujiepusha na madhambi na maovu. Mwigilize ndani yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye alikuwa mkarimu zaidi ya watu na ukarimu wake ulikuwa ukishamiri zaidi ndani ya Ramadhaan ambapo akikithirisha kufanya mema kukiwemo swawm, swadaqah, kusoma Qur-aan, Dhikr, du´aa, kufanya mema na kujiepusha na maovu.
Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wote.
[1] an-Nasaa´iy (2106) na Ahmad (7148).
[2] Katika ”Musnad-us-Shaamiyn” (03/271).
- Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
- Mfasiri: Firqatunnajia.com
- Marejeo: Duruus fiy Ramadhwaan, uk. 17-18
- Imechapishwa: 12/04/2023
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window)
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window)
- Click to print (Opens in new window)
- Click to email a link to a friend (Opens in new window)
- Click to share on Facebook (Opens in new window)
- Click to share on Twitter (Opens in new window)
- Click to share on Pocket (Opens in new window)