Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

ujuzi wa kumjua Mtume Wake

MAELEZO

Miongoni mwa mambo ya wajibu ambayo hapewi udhuru wowote kwa kutoyajua ni kumtambua Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuyajua yale ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekuja nayo. Haitoshi kwa muislamu wa kike na wa kiume kusema kwamba wanamjua Mtume wa Allaah kwamba ni Muhamamd bin ´Abdillaah. Haitoshi jambo hili. Anatakiwa kutambua kuwa ametumilizwa kutoka kwa Allaah, Allaah amemteremshia Kitabu, ambayo ni Upambanuzi, na akamwamrisha kuipambanua, akamwamrisha kuwalingania Ummah kushikamana barabara na Kitabu hichi na yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Sunnah zake tukufu. Kutokana na hilo kumtambua Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumefupika katika mambo yafuatayo:

1 – Kujua utu wake. Yeye ni Muhammad bin ´Abdillaah bin ´Abdil-Muttwalib bin Haashim. Haashim wanatokana na Quraysh, Quraysh wanatokana na waarabu, waarabu wanatokana na kizazi cha Ismaa´iyl bin Ibraahiym kipenzi wa hali ya juu wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

2 – Kumepnda zaidi ya jinsi mtu anavoipenda nafsi yake, mali zake, watoto na wazazi wake.

3 – Kuyapenda yale aliyokuja nayo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa ujumla na kwa upambanuzi.

4 – Kuyatendea kazi kwa kutarajia rehema za Allaah na kwa kuogopa adhabu Zake.

Wanachuoni wametaja baada ya tafiti za kisomi kwamba “kushuhudia kuwa Muhammad ni Mtume wa Allaah” kuna sharti sita:

Ya kwanza: Kutambua ujumbe Wake na kuuamini ndani ya moyo.

Ya pili: Kuitamka na kuitambua kwa mdomo.

Ya tatu: Kumfuata katika kutendea kazi yale aliyokuja nayo hali ya kuyaamrisha na kukataza na kuyahalalisha na kuharamisha.

Ya nne: Kumsadikisha katika yale yote aliyokhabarisha katika mambo yaliyojifichikana yaliyotangulia na yanayokuja huko mbele.

Ya tano: Kumpenda zaidi kuliko mtu anavyoipenda nafsi yake, mali yake, watoto wake, wazazi wake na watu wengine wote.

Ya tano: Kutanguliza maneno yake mbele kabla ya maneno ya mwengine yeyote na kutendea kazi Sunnah zake.

Allaah (´Azza wa Jall) amemteremshia Wahy Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) awafikishie Ummah ueneaji wa ujumbe wake na kwamba hauwahusu waarabu peke yao. Bali ni ujumbe wenye kuenea na unaomuhusu kila yule ambaye Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametumilizwa akiwa ardhini. Ni mamoja mtu huyo ni mwarabu au si mwarabu, mwanamume au mwanamke, muungwana au mtumwa, mtukufu au asiye mtukufu, bali majina na watu. Amesema (Ta´ala):

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا

“Sema: “Hakika mimi ni Rasuli wa Allaah kwenu nyinyi nyote.”[1]

Maneno Yake:

 جَمِيعًا

“… nyote.”

yamewakusanya viumbe wote.

Allaah akasisitiza maana hii katika maneno Yake:

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا كَافَّةً لِّلنَّاسِ بَشِيرًا وَنَذِيرًا

”Hatukukutuma isipokuwa kwa watu wote na uwe mbashiriaji na muonyaji.”[2]

Maneno Yake:

كَافَّةً

“… wote… “

yanafidisha ujumla. Kwa hivyo hatoki nje ya ujumbe wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yeyote ambaye Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametumilizwa na yeye yuko ulimwenguni. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisisitiza ujumla na ueneaji huu pale aliposema:

“Ninaapa kwa Ambaye nafsi ya Muhammad iko mikononi Mwake. Hatosikia kuhusu mimi yeyote kutoka katika Ummah huu – awe myahudi au mkristo – kisha akafa hali ya kuwa si mwenye kuamini yale niliyokuja nayo isipokuwa atakuwa ni miongoni mwa watu wa Motoni.”[3]

Madai ya mayahudi, madai ya wakristo na madai ya wanaodai kwamba wanamwabudu Allaah kwa vitabu vilivyoitangulia Qur-aan – baada ya kuwa Qur-aan imeshateremshwa na yule ambaye ameteremshiwa Qur-aan hiyo – ni madai batili. Isitoshe ni mwongo katika madai hayo. Kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameifanya Qur-aan ni yenye kuvihukumu vitabu vyengine vyote. Pia amemfanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye mwenye kumalizia Mitume na Manabii wote. Hivyo haijuzu kwa yeyote kuabudu isipokuwa kwa Shari´ah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye hazungumzi kwa matamanio yake mwenyewe.

[1] 07:158

[2] 34:28

[3] Muslim (01/134).

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Twariyqal-Usuwl ilaa idhwaah-ith-Thalaat-il-Usuwl, uk. 18-20
  • Imechapishwa: 18/11/2021