Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah akurehemu

MAELEZO

Wewe ambaye ni msomaji na msikilizaji mwenye kufaidika. Kisha baada ya hapo akaanza makusudio ambayo ni kubainisha kwamba ni lazima kwa kila muislamu wa kike na wa kiume masuala haya ambayo ameyataja kwa kusema:

“… ya kwamba ni wajibu juu yetu kujifunza masuala mane:”

 Ameyaanza kwa njia ya ujumla mambo manne ili msomaji na msikilizaji waweze kutafuta upambanuzi wake mambo haya manne. Kwani watu wana haja kubwa kuyafahamu na khaswakhaswa wanafunzi wajifunze nayo na wawafunze nayo wengine ili wapate thawabu nyingi. Mwandishi (Rahimahu Allaah) amesema:

”Suala la kwanza: Ujuzi”

Makusudio ya elimu ni elimu ya Kishari´ah. Ni yale yaliyotajwa katika Qur-aan na Sunnah na yakabainishwa na wanachuoni walezi ambao wanafuata ´Aqiydah Salafiyyah[1] na mfumo uliosalimika katika kila mlango wa elimu.

Maneno haya ya kijumla upambanuzi wake umekuja baada yake. Kama kwamba muulizaji anauliza ni yepi makusudio ya elimu ambayo ni lazima? Kwa sababu elimu kuna ambayo ni wajibu na hapewi udhuru mtu kwa kutoijua. Sehemu nyingine ya elimu ni faradhi kwa baadhi ya watu. Sehemu nyingine ya elimu ni faradhi kwa kila mmoja. Mambo haya manne – ambapo jambo la kwanza ni elimu – ni wajibu na lazima kwa kila muislamu mwanaume na mwanamke. Maneno Yake (Rahimahu Allaah):

”… nao ni ujuzi wa kumjua Allaah”

Amefasiri elimu kwamba ni ujuzi wa kumjua Allaah. Kwa msemo mwingine ni lazima kwa kila muislamu wa kiume na wa kike kila mmoja kumtambua Mola Wake kwa dhati Yake, sifa Zake, matendo Yake na kwamba:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[2]

Vilevile mja anatakiwa kutambua kuwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ndiye Muumbaji na Mruzukaji Wake. Yeye ndiye anayaendesha mambo Yake na ulimwengu mzima. Yeye pekee ndiye anastahiki kuabudiwa pasi na mwengine. Kila ´ibaadah anayofanyiwa mwengine basi hiyo ni ´ibaadah batili na mwenye kufanya hivo kamshirikisha Allaah.

Vilevile mtu anapaswa kuamini kwamba Allaah ana majina mazuri mno na sifa kuu zilizotajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah. Allaah (´Azza wa Jall) ametuamrisha majina na sifa viwe ni njia katika kumuomba na kumdhalilikia. Amesema:

وَلِلّهِ الأَسْمَاء الْحُسْنَى فَادْعُوهُ بِهَا وَذَرُواْ الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَآئِهِ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُواْ يَعْمَلُونَ

”Allaah ana majina mazuri mno; hivyo basi muombeni kwayo na waacheni wale wanaopotoa katika majina Yake. Watalipwa yale waliokuwa wakifanya.”[3]

Kwa hivyo yule mwenye kumtambu Allaah (´Azza wa Jall) ipasavyo basi atamtukuza ukweli wa kumtukuza. Matokeo yake atatekeleza faradhi Zake, mambo ya wajibu, atafanya yale yaliyoamrishwa, atajiepusha na yale yaliyokatazwa, ayahalalisha ya halali hali ya kuona kuwa ni halali na ataharamisha ya haramu hali ya kuona kuwa ni haramu. Anafanya yote hayo na wakati huohuo anataraji rehema za Mola Wake na anachelea adhabu Zake katika maisha yake yote. Huyu ndiye muumini wa kweli. Huyu atapata kutoka kwa Mola Wake msamaha na ujira mkubwa.

[1] Maana ya ”Salafiyyah” ni nisba ya wema waliotangulia (as-Salaf as-Swaalih). Nao si wengine ni Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Taabi´uun na wale wenye kufuata mwenendo wao hadi siku ya Qiyaamah.

[2] 42:11

[3] 07:180

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Twariyqal-Usuwl ilaa idhwaah-ith-Thalaat-il-Usuwl, uk. 16-18
  • Imechapishwa: 18/11/2021