Dalili ya masuala haya mane ni maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَالْعَصْرِ إِنَّ الْإِنسَانَ لَفِي خُسْرٍ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ

“Naapa kwa al-‘Aswr. Hakika ya mwanaadamu bila ya shaka yumo katika khasara. Isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema na wakausiana kwa kufuata ya haki na wakausiana kuwa na subira.”
(103:01-03)

Katika Suurah hii kubwa kuna dalili juu ya mambo haya. Hii ndio dini yote. Dini yote inahusiana na kuamini, kutenda kazi, kulingania na kusubiri. Haki inatakiwa kuaminiwa na kutendewa kazi. Baada ya hapo inatakiwa kulingania kwayo na kusubiri juu ya maudhi. Watu wote wamo katika khasara:

إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ

“… isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema na wakausiana kwa kufuata ya haki na wakausiana kuwa na subira.”

Allaah amewavua hao tu. Watu wote wamo khasarani na wameangamia isipokuwa wale walioamini, wakatenda wema, wakalingania katika haki na wakausiana kuwa na subira. Hawa ndio wenye kufuzu na wenye furaha. Allaah ameliapia hilo. Naye (Subhaanah) ni mkweli hata kama hakuapa. Hata hivyo ameapa ili kutilia nguvu nafasi hiyo. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) anaapa kwa kile anachokitaka katika viumbe Wake. Hakuna yeyote ana haki ya kumkataza. Ameapa kwa mbingu yenye buruji, mbingu, nyota, wakati wa asubuhi, jua na mwangaza wake, usiku unapofunika, wanaong´oa kwa nguvu na vyenginevyo. Viumbe wanaonyesha dalili ya ukubwa Wake na kwamba Yeye (Subhaanah) peke yake ndiye anayestahiki kuabudiwa. Anaapa vilevile kwa viumbe hivi ili kuonyesha ukubwa wake kwa sababu vinathibitisha umoja Wake na kwamba Yeye peke yake ndiye anayestahiki kuabudiwa.

Kuhusu viumbe haifai kwa wao wakaapa isipokuwa kwa Mola wao. Haifai kwake akaapa kwa mwengine asiyekuwa Allaah. Haijuzu kwake akaapa kwa Mitume, masanamu, waja wema, amana, Ka´bah wala kitu kingine. Huu ndio wajibu kwa waislamu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atayeapa kwa kitu asiyekuwa Allaah ameshirikisha.” Ahmad (1/47), ´Abdur-Razzaaq katika ”al-Muswannaf” (15926), Abu Daawuud (3251), at-Tirmidhiy (1535) na al-Haakim (7814).

Ameipokea Imaam Ahmad kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anayeapa basi na aape kwa Allaah au anyamaze.” al-Bukhaariy (6646) na Muslim (1646).

Ni wajibu kwa waislamu wote wahadhari kuapa kwa mwengine asiyekuwa Allaah na waape kwa Allaah peke yake (Subhaanahu wa Ta´ala).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 09-10
  • Imechapishwa: 15/10/2016