Ulazima wa kufunga Ramadhaan unaanza pale kutapojulikana kuingia kwake. Zipo njia tatu za kujua kuwa Ramadhaan imeingia:

1- Kuonekana mwezi mwandamo. Amesema (Ta´ala):

فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ

“Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi mpya na afunge.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Fungeni kwa kuuona… “[2]

Ambaye atauona mwezi mwandamo yeye mwenyewe basi atalazimika kufunga.

2- Ushahidi wa kuuona au taarifa juu yake. Watu watafunga kwa ushahidi wa mtu mwadilifu ambaye ´ibaadah ni yenye kumuwajibikia ambaye ataelezea juu ya jambo hilo. Ibn ´Umar amesema:

“Watu waliona mwezi mwandamo. Nikamweleza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba nimeuona ambapo akafunga na akawaamrisha watu kufunga.”

Ameipokea Abu Daawuud na wengineo. Imesahihishwa na Ibn Hibbaan na al-Haakim[3].

3- Kukamilisha idadi ya Sha´baan siku thelathini. Hapo ni pale ambapo hautoonekana mwezi mwandamo usiku wa kuamkia tarehe thelathini za Sha´baan kwa kuwepo vitu vinavyozuia maono kama mfano wa mawingu, vipandikizi na mfano wake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika mwezi ni siku ishirini na tisa. Hivyo basi msifunge mpaka mtakapoona mwezi mwandamo na wala msifungue mpaka mtakapouona. Mkifunikwa na mawingu basi ikadirieni.”[4]

Maana ya maneno:

“… ikadirieni.”

kamilisheni mwezi wa Sha´baan siku thelathini. Hayo ni kutokanaa na yale yaliyothibiti katika Hadiyth ya Abu Hurayrah:

“Mkifunikwa na mawingu, basi ikadirieni siku thelathini.”[5]

[1] 02:185

[2] al-Bukhaariy (1909) na Muslim (19/1081).

[3] Abu Daawuud (2342), Ibn Hibbaan (3447), al-Haakim (1541) na ad-Daaraqutwniy (2127).

[4] al-Bukhaariy (1907) na Muslim (2499).

[5] al-Bukhaariy (1909) na Muslim (2516).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mulakhasw al-Fiqh (01/374-375)
  • Imechapishwa: 24/03/2021