Kufunga Ramadhaan kunamlazimu kila muislamu, ambaye ´ibaadah ni yenye kumuwajibikia na muweza. Hiyo ina maana kwamba haimlazimu kafiri na wala haishi kutoka kwake. Akisilimu katikati ya mwezi basi atafunga siku zilizosalia. Hatolazimika kulipa siku zilizotangulia kipindi cha ukafiri wake.

Si lazima kwa mtoto mdogo kufunga ijapo mtoto mwenye uwezo wa kupambanua akifunga ni sahihi. Kwa haki yake itazingatiwa kuwa ni funga iliyopendekezwa.

Si lazima kwa mwendawazimu kufunga. Akifunga kipindi cha wendawazimu wake haitosihi kutoka kwake kwa kutokuwa na manuizi.

Si lazima kwa mgonjwa asiyeweza kufunga na msafiri kufunga. Watailipa wakati ambapo wataondokwa na udhuru wa ugonjwa na safari. Amesema (Ta´ala):

فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Basi atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu au yuko safarini, hivyo basi akamilishe idadi katika siku nyinginezo.”[1]

[1] 02:184-185

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mulakhasw al-Fiqh (01/376)
  • Imechapishwa: 24/03/2021