04. Mwanafunzi kuwa nia nzuri ya kujifunza elimu

Jambo kubwa na muhimu zaidi katika kujifunza elimu ni mwanafunzi anatakiwa amtakasie nia Allaah (´Azza wa Jall) katika kutafuta kwake elimu. Asikusudie jengine isipokuwa Uso wa Allaah (´Azza wa Jall). Awe na nia ya kujinufaisha mwenyewe, awanufaishe watu na ajifunze kheri na kuieneza. Akifanya yote hayo huku akikusudia Uso wa Allaah (´Azza wa Jall). Atayefanya hivo, basi atapata ujira mkubwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anasema:

“Hakika kila kitendo kinategemea na nia na kila mmoja atalipwa kutegemea na vile alivyonuia. Yule aliyehajiri kwa ajili ya Allaah na Mtume Wake, basi kuhajiri kwake kutakuwa kwa ajili ya Allaah na Mtume Wake, na yule aliyehajiri kwa ajili ya dunia ataipata au kwa ajili ya kumuoa mwanamke, basi kuhajiri kwake ni kwa lile alilohajiri kwalo.”[1]

Hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametahadharisha vikali kujifunza elimu kwa ajili ya kupata pato la kidunia na akabainisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba kuwa na nia nzuri katika kujifunza elimu ni jambo kubwa na khatari yake ni kubwa. Imesihi kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Watu wa kwanza wataoshikwa siku ya Qiyaamah… ” halafu akataja watu watatu. Miongoni mwao “… mtu ambaye amejifunza elimu na akaifunza na akasoma Qur-aan. Ataletwa na kujuzwa neema yake. Aseme: “Nimezitambua.” Aulizwe: “Ulifanya nini kwayo?” Aseme: “Nilijifunza elimu na mimi nikaifunza na nikasoma Qur-aan kwa ajili Yako.” Ataambiwa: “Umesema uongo. Hakika wewe ulijifunza ili uitwe ‘mwanachuoni’ na umesoma Qur-aan ili isemwe ‘msomaji’ na kumeshasemwa. Baada ya hapo kuamrishwe atupwe kwa uso wake ndani ya Moto.”[2]

Ndugu waheshimiwa! Hakika miongoni mwa fitina ilio kubwa kabisa ni mwanafunzi akusudie katika kujifunza kwake elimu kupata jina la kidunia na kusifiwa kwa wasifu wa kidunia. Kwa mfano aambiwe “Kiongozi wetu mwanachuoni!”, “Kiongozi wetu msomaji!”, “Muheshimiwa Shaykh msomaji!”, “Daktari!”, “Mwalimu!”, na majina mengineyo ya kidunia. Khatari kubwa kwa mwanafunzi ni pale malengo yake ya kujifunza elimu yatakuwa ni kama haya. Mfano wa mtu kama huyu ndiye wa kwanza atayevugumizwa Motoni siku ya Qiyaamah. Allaah atulinde na mfano wa mambo kama haya.

[1] al-Bukhaariy (54) na Muslim (1907)

[2] Muslim (1905)

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliymillaah ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Ilm wa Wasaaailuh wa Thimaaruh
  • Imechapishwa: 22/10/2016