04. Mnaonaje kuhusu Allaah kuwa juu ya waja na kulingana juu ya ´Arshi?

´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy (rahimahullaah) amesema:

Swali 4: Mnaonaje kuhusu Allaah kuwa juu ya waja na kulingana juu ya ´Arshi?

Jibu: Tunamtambua Mola wetu kuwa juu kwa njia zote:

1 – Kuwa juu kwa dhati.

2 – Kuwa juu kwa hadhi na sifa.

3 – Kuwa juu kwa nguvu.

Ametengana na viumbe Wake na amelingana juu ya ´Arshi.

MAELEZO

Allaah kuwa juu ya viumbe Wake ni jambo linalotambulika kimaumbile. Pindi mja anapomuomba Allaah basi huelekea kwa moyo wake na roho yake kwa Allaah (´Azza wa Jall) hali ya kuwa ni mwenye kunyanyua kichwa chake kukielekeza mbinguni. Sambamba na hilo anamuomba msaada Yule aliyeko juu ya ´Arshi. Ahl-us-Sunnah wanaona kuwa Allaah amelingana juu ya ´Arshi na ni Mwenye kujitenga na viumbe Wake na wakati huohuo elimu Yake imeenea kila mahali.

Kulingama maana yake ni kuwa juu na kuthibiti. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

لِتَسْتَوُوا عَلَىٰ ظُهُورِهِ ثُمَّ تَذْكُرُوا نِعْمَةَ رَبِّكُمْ إِذَا اسْتَوَيْتُمْ عَلَيْهِ وَتَقُولُوا سُبْحَانَ الَّذِي سَخَّرَ لَنَا هَـٰذَا وَمَا كُنَّا لَهُ مُقْرِنِينَ وَإِنَّا إِلَىٰ رَبِّنَا لَمُنقَلِبُونَ

“Ili mlingamane sawasawa juu ya mgongo wake, kisha mkumbuke neema ya Mola wenu mtakapolingamana sawasawa juu yao na mseme: “Utakasifu ni wa Yule ambaye ametutiishia haya na tusingeliweza wenyewe kumdhibiti na hakika kwa Mola wetu bila shaka ni wenye kurejea.”[1]

Kulingana hapa maana yake ni kuthibiti. Kadhalika maneno Yake (Ta´ala):

وَاسْتَوَتْ عَلَى الْجُودِيِّ ۖ وَقِيلَ بُعْدًا لِّلْقَوْمِ الظَّالِمِينَ

“… na [jahazi] likatua juu ya [mlima wa] al-Juwdiyy na pakasemwa: “Wametokomelea mbali watu madhalimu!”[2]

Bi maana kuthibiti juu ya mlima.

Yule mwenye kutaka kulifasiri kwa maana nyingine anazingatiwa ni mpotevu. Ashaa´irah wanaikengeusha sifa hii ya kwamba ni kutawala. Tafsiri hii ni batili. Wanatumia dalili mashairi ya al-Akhtwal:

“ Bishr amelingana (Istawaa) juu ya ´Iraaq bila ya upanga wala kumwaga damu.”

 al-Akhtwal alikuwa mkrito na haiwezekani mashairi yake yakatuiwa kama tafsiri ya Qur-an.

Isitoshe kutawala kunakuwa juu ya kitu ambacho kabla ya hapo mtu hakuwa mwenye kukitawala. Kwa ajili hiyo Maalik bin Anas (Rahimahu Allaah) alimkemea bwana mmoja aliyemuuliza namna Allaah alivyolingana juu ya ´Arshi. Akainamisha kichwa chake chini na akaanza kutokwa na majasho. Kisha akainua kichwa chake na kusema:

“Kulingana kunatambulika. Namna haijulikani. Kuamini hilo ni jambo la lazima. Kuuliza juu ya hilo ni jambo la Bid´ah. Wewe ni mtu muovu. Mtoeni nje.”[3]

Ndipo akatolewa nje.

Kufasiri kulingana kwa maana ya uangalizi ina maana hiyohiyo ya kutawala. Yote hayo ni ujinga na upotevu. Ni nani ambaye alikuwa akiiangalia ´Arshi kabla ya Muumba wa ´Arshi (Subhaanahu wa Ta´ala)?

Kulingana juu ya ´Arshi ni sehemu ya ujuu na inahusiana na ujuu wa dhati. Aina zingine za ujuu ni ujuu wa dhati na ujuu wa sifa. Ikiwa Allaah (´Azza wa Jall) ana dhati isiyofanana na dhati zengine, basi tunapaswa tutambue kuwa yuko na sifa zisizofanana na sifa nyenginezo. Je, uwezo wa Allaah ni kama uwezo wa mtu kwa sababu tu wote wawili wanao uwezo? Hapana. Uwezo wa Allaah si wenye kushindwa na chochote ilihali uwezo wa viumbe ni wa viwango. Vivyo hivyo inapokuja kuhusu ujuzi wa Allaah na sifa Zake zengine zote. Ujuzi wa Allaah ni wenye kukienea kila kitu ilihali ujuzi wa mtu ni wenye mipaka. Kwa hiyo ujuu wa Allaah wa uwezo unapelekea vilevile ujuu wa sifa Zake. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[4]

وَأُوحِيَ إِلَيَّ هَـٰذَا الْقُرْآنُ لِأُنذِرَكُم بِهِ وَمَن بَلَغَ

“Nimeteremshiwa Wahy hii Qur-aan ili nikuonyeni kwayo na kila itakayomfikia.”[5]

Ama kuhusu kuwa juu kwa nguvu, tunatakiwa kuamini ya kwamba Allaah ni Mwenye kudhibiti juu ya viumbe Wake wote. Wote wako chini ya ufalme Wake. Ni Mwenye kuwafanya atakacho. Anawafanya akitakacho. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ ۚ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ

“Naye hapingiki Aliye Mkuu kabisa juu ya waja Wake Naye ni Mwenye hekima wa yote, Mwenye khabari zote.”[6]

وَاللَّـهُ غَالِبٌ عَلَىٰ أَمْرِهِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ

“Allaah ni Mwenye kushinda juu ya jambo Lake, lakini watu wengi hawajui.”[7]

Kwa ajili hiyo ndio maana Allaah alimpasulia bahari Muusa (´alayhis-Salaam) na akamzamisha ndani yake Fir´awn na watu wake.

Vilevile aliufanya moto kuwa baridi na salama kwa Ibraahiym (´alayhis-Salaam).

Aliitikia du´aa ya Nuuh na akawazamisha wote waliokuwemo ardhini isipokuwa Nuuh na wale waliokuwa pamoja naye ndani ya safina.

Akawaangamiza ´Aad kwa upepo mkali.

Akawaangamiza watu wa Swaalih (´alayhis-Salaam) kwa ukelele.

Akamnyanyua ´Iysaa (´alayhis-Salaam) juu mbinguni na akamwokoa kutokamana na vitimbi ya mayahudi.

Akampandisha Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mpaka akafika katika mbingu ya saba.

Yote haya yanaonyesha nguvu za Mola (Subhaanahu wa Ta´ala) na kuwadhibiti Kwake waja Wake.

Kwa kufupiza ni kwamba ujuu umegawanyika aina tatu: ujuu wa dhati, ujuu wa hadhi na ujuu wa nguvu. Tunalazimika kuamini aina zote hizo na kwamba Allaah amelingana juu ya ´Arshi Yake na kwamba ametengana na viumbe Wake na wakati huohuo elimu Yake imetapakaa kila mahali. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ ۖ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ

“Hakika Tumemuumba mwanaadamu na tunajua yale  yanayomshawishi nafsi yake na Sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wa shingo.”[8]

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۖ مَا يَكُونُ مِن نَّجْوَىٰ ثَلَاثَةٍ إِلَّا هُوَ رَابِعُهُمْ وَلَا خَمْسَةٍ إِلَّا هُوَ سَادِسُهُمْ وَلَا أَدْنَىٰ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْثَرَ إِلَّا هُوَ مَعَهُمْ أَيْنَ مَا كَانُوا ۖ ثُمَّ يُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Je, huoni kwamba Allaah Anajua yale yote yaliyomo mbinguni na yale yote yaliyomo ardhini? Hauwi mnong’ono wa watatu isipokuwa Yeye ni wa nne wao, na wala watano isipokuwa Yeye ni wa sita wao, na wala [hauwi mnong’ono wa] chini kuliko ya hivyo, na wala wa wengi zaidi isipokuwa Yeye Yu pamoja nao popote watakapokuwa, kisha siku ya Qiyaamah atawajuza yale waliyoyafanya. Hakika Allaah kwa kila jambo ni Mjuzi.”[9]

Allaah hakutuamrisha kumwelekea mwombezi wakati tunamwomba Yeye kitu. Bali ametukhabarisha na akatubainishia kwa kusema:

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ

“Watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi [wajuze kwamba] Mimi Niko karibu Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Hivyo basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi wapate kuongoka.”[10]

Enyi watu! Mwombeni Mola wenu kwa siri na kwa dhahiri. Mwelekee Yeye katika kila jambo lako muhimu. Yeye ndiye muweza wa kuyaondosha matatizo. Yeye ndiye mwenye kuzijibu du´aa. Nakutahadharisheni kumwelekea mwengine asiyekuwa Yeye mkaja kupotea na kukata mafungamano yako Naye. Matokeo yake akakupuuza vile utakavyoangamia.

[1] 43:13-14

[2] 11:44

[3] Sharh Usuul I´tiqaad Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah (644), Abu Nu´aym katika ”Hilyat-ul-Awliyaa’” (6/325) na adh-Dhahabiy katika ”al-´Uluww”, uk. 139, aliyesema: ”Haya yamethibiti kutoka kwa Maalik.” Ibn Hajar ameitaja katika ”Fath-ul-Baariy” (13/406) na akasema kuwa cheni ya wapokezi wake ni nzuri.

[4] 42:11

[5] 06:19

[6] 6:18

[7] 12:21

[8] 50:16

[9] 58:07

[10] 02:186

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyaat ´alaa Kitaab Ahamm-il-Muhimmaat, uk. 28-32
  • Imechapishwa: 23/09/2021