04. Kulingania kwa Allaah juu ya utambuzi wa mambo matatu

Enyi ndugu! Kulingania kwa Allaah pasi na elimu ni kinyume na yale aliyokuwemo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wale waliomfuata. Sikiza maneno ya Allaah hali ya kumwamrisha Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale aliposema:

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي ۖ وَسُبْحَانَ اللَّـهِ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ

“Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah, juu ya ujuzi na umaizi – mimi na anayenifuata. Utakasifu ni wa Allaah na mimi si miongoni mwa washirikina.”[1]

Maneno Yake:

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي ۖ وَسُبْحَانَ اللَّـهِ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ

“Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah, juu ya ujuzi na umaizi – mimi na anayenifuata.”[2]

maana yake ni kwamba atakayemfuata yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni lazima alinganie kwa Allaah kutokana na utambuzi na si kutokana na ujinga.

Ee ambaye unalingania kwa Allaah, tafakari maneno ya Allaah (Ta´ala):

عَلَىٰ بَصِيرَةٍ

“… juu ya ujuzi na umaizi.”

maana yake ni utambuzi juu ya mambo matatu:

1 – Awe na utambuzi juu ya kile anacholingania. Awe ni mjuzi wa hukumu ya Shari´ah kwa yale anayolingania. Kwa sababu anaweza kulingania katika jambo ambalo anafikiri kuwa ni wajibu ilihali kwa mujibu wa Shari´ah ya Allaah sio wajibu. Matokeo yake akawalazimisha waja wa Allaah mambo ambayo Allaah hakuwalazimisha. Pia anaweza kulingania kuacha jambo ambalo anadhani kuwa ni haramu ilihali kwa mujibu wa dini Allaah sio haramu. Matokeo yake anakuwa mwenye kuwaharamishia waja wa Allaah yale ambayo Allaah amewahalalishia.

2 – Awe na utambuzi wa hali ya mlinganiwa. Ndio maana wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomtuma Mu´aadh kwenda Yemen alimwambia:

“Hakika wewe unawaendea watu wa Kitabu.”[3]

Anamwambia hivi ili ajue hali yao na ajiandae nao. Kwa hivyo ni lazima utambue hali ya huyu anayelinganiwa na kiwango alichonacho cha elimu na mahojiano. Lengo ni ili upate kujiandaa na hivyo ujadiliane naye. Ukianza kubishana na mfano wa mtu kama huyu na yeye akawa na nguvu ya kujadili kukushinda basi inakuwa ni balaa kubwa dhidi ya haki ilihali wewe ndiye umesababisha. Usidhanie kwamba mtu wa batili anashindwa vyovyote vile. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika nyinyi mnazozana kwangu na pengine baadhi yenu wakawa ni mafaswaha zaidi kwa hoja zake kuliko wengine. Nikamuhukumia yeye kwa mujibu wa kile nilichosikia.”[4]

Hii inajulisha kwamba huyu mtesi, ijapo atakuwa katika batili, anaweza kuwa mfaswaha zaidi katika hoja yake kuliko yule mwingine na matokeo yake akahukumiwa kwa mujibu wa kile alichokizungumza huyu mtesi. Kwa hivyo ni lazima uwe mtambuzi wa hali ya yule mlinganiwa.

3 – Awe na ujuzi namna ya kulingania. Allaah (Ta´ala) amesema:

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ

“Lingania katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi.”[5]

Baadhi ya watu wanaweza kupata maovu na hivyo wakayashambulia. Mtu huyu hazingatii matokeo yanayotokana na jambo hilo na si kwa upande wake yeye mwenyewe, lakini kwa upande wake yeye na wenzake katika wanaolingania katika haki.

Kwa hivyo ni lazima kwa mlinganizi kabla ya kufanya hatua yoyote atazame matokeo na ayapime. Pengine katika wakati huo ukawa ni mwenye kuzima miale ya ghera kwa kile unachokifanya. Lakini kitendo hichi kitazima moto wa ghera yake na ghera ya wengine huko mbele. Pengine mustakabali wake uko karibu na hauko mbali. Kwa ajili hii nawahimiza ndugu zangu kutumia hekima na utaratibu. Jambo pengine likachelewa kidogo lakini mwisho wake ukawa wenye kusifiwa kwa matakwa ya Allaah (Ta´ala).

Mambo yakiwa hivo – kujipamba mlingajizi kwa elimu sahihi – inayojengeka juu ya Qur-aan na Sunnah Swahiyh ambavyo ndivo vinavyojulishwa na maandiko yaliyowekwa katika Shari´ah na aidha ndio vinavyojulishwa na akili ya wazi ambayo ndani yake haina shubuha wala matamanio, kwa sababu ni vipi utalingania kwa Allaah (´Azza wa Jall) na wewe hujui njia inayokufikisha Kwake na Shari´ah Yake. Ni vipi utafaa kuwa mlinganizi? Mtu akiwa hana elimu basi bora kwake ni yeye kusoma kwanza kisha baada ya hapo ndio alinganie.

[1] 12:108

[2] 12:108

[3] al-Bukhaariy (1496) na Muslim (31).

[4] al-Bukhaariy (2680) na Muslim (1713).

[5] 16:125

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Zaad Daa´iyah ila Allaah, uk. 11-13
  • Imechapishwa: 01/11/2021