Zipo Hadiyth nyingi za kinabii zinazotilia nguvu fadhilah za kuwa na subira na malipo yake na kuihimiza kwa yule ambaye amefikwa na majanga. Miongoni mwazo ni yale aliyosimulia Abu Maalik al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Usafi ni nusu ya imani. Kusema “Himdi zote njema anastahiki Allaah (الحمد لله) kunajaza mizani, na kusema “Allaah ametakasika na mapungufu, na himdi zote njema anastahiki Allaah (سبحان الله والحمد لله) kunajaza yaliyomo kati ya mbingu na ardhi. Swalah ni nuru, swadaqah ni hoja, subira ni mwanga na Qur-aan ni ima hoja yako au dhidi yako. Kila mmoja ni mwenye kujipinda na kuiuza nafsi yake; ima akaiacha huru au akaiangamiza.”[1]

Ameipokea Muslim katika ”as-Swahiyh” yake, Imaam Ahmad katika ”al-Musnad”, Ibn Maajah katika ”as-Sunan” na an-Nasaa’iy kwa kifupi katika ”´Amal-ul-Yawm wal-Laylah”. Ni Hadiyth iliyo na faida kubwa na ni moja katika misingi ya Uislamu. Inafahamisha kuwa mwenye subira ni mwenye kuendelea kuangaziwa mwanga wa uongofu na usawa sambamba na hayo analipwa ujira na thawabu.

Muslim amepokea kutoka kwa Suhayb (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ajabu iliyoje juu ya jambo la muumini. Hakika mambo yake yote huwa ni kheri. Na hilo haliwi kwa mwingine isipokuwa tu muumini. Akifikwa na kitu cha kufurahisha basi hushukuru na ikawa ni kheri kwake. Na akifikwa na kitu cha kusononesha basi husubiri na ikawa ni kheri kwake.”[2]

Sa´iyd (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hamshangazwi na muumini? Akifikwa na jambo la kumfurahisha, basi humhimidi na kumshukuru Allaah. Na akifikwa na msiba, anamhimidi Allaah na kusubiri. Muumini analipwa thawabu juu ya kila kitu – mpaka tonge analoliweka ndani ya mdomo wake.”

Ameipokea an-Nasaa´iy.

Nasema:

Makadirio yanapita na ndani yake kuna kheri ya ziada

kwa muumini anayemtegemea Allaah – na si kwa mwenye mbwembwe

Ni mamoja amefikwa na faraja au msiba

yeye husema ´namshukuru Allaah´

al-Mubaarak bin Fadhwaalah al-´Adawiy al-Baswriy amesimulia kwamba amemsikia al-Hasan (Rahimahu Allaah) akisema:

”Kila wakati ambapo Ayyuub alikuwa anafikwa na msiba basi husema: ”Ee Allaah, Wewe ndiye Umetwaa na Wewe ndiye Uliyetoa kwa muda wa kuwa Umeibakiza nafsi yangu. Nakushukuru kwa majaribio Yako mazuri.”

Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yule mwenye kujibidisha kusubiri, basi Allaah atamsubirisha. Hakuna yeyote aliyepewa zawadi bora na kunjufu zaidi kama subira.”[3]

Ameipokea al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy.

[1] Muslim (223), Ahmad (5/342), at-Tirmidhiy (3517) aliyesema kuwa Hadiyth ni nzuri na Swahiyh, an-Nasaa’iy (5/5-6) na Ibn Maajah (280).

[2] Muslim (2999) na Ahmad (4/332).

[3] al-Bukhaariy (1469) na Muslim (1053).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 31-33
  • Imechapishwa: 09/08/2023