05. Hapa ndipo subira huzingatiwa

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Allaah hajampa mja kitu ambacho ni bora kwake na kunjufu zaidi kama subira.”[1]

Abud-Dardaa´ (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa amemsikia Abul-Qaasim (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

”Allaah (Ta´ala) amesema: ”Ee ´Iysaa! Hakika mimi nitaumba ummah baada yako, wakifikwa na yale wanayoyapenda, basi wanamshukuru Allaah, na wakifikwa na yale yanayowachukiza, wanataraji malipo kutoka kwa Allaah na kusubiri – pasi na upole wala ujuzi.” Akasema: ”Ee Mola! Hayo yanakuweje?”[2] Akasema: ”Nawapa katika upole na ujuzi Wangu.”

Ameipokea Imaam Ahmad, al-Bazzaar, at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Awsatw” na al-Haakim katika ”al-Mustadrak”  na ambaye pia ameisahihisha.

Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ukubwa wa malipo ni pamoja na ukubwa wa mitihani. Hakika Allaah (Ta´ala) anapowapenda watu basi huwajaribu. Yule mwenye kuridhia basi hupata radhi Zake na yule mwenye kuchukia basi hupata hasira Zake.”[3]

Ameipokea at-Tirmidhiy na Ibn Maajah.

Mahmuud bin Labiyb (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Allaah anapowapenda watu, basi huwapa majaribio.Yule mwenye kusubiri ana subira, na yule mwenye kukasirika anapata hasira.”[4]

Ameipokea Ahmad katika ”al-Musnad”yake.

Imesihi ya kwamba Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimpitia mwanamke mmoja anayemlilia mtoto wake ambapo akamwambia: ”Mche Allaah na kuwa na subira!” Akasema: ”Unajali nini juu ya msiba wangu?” Alipokwenda zake, mwanamke yule akaambiwa: ”Alikuwa ni Mtume wa Allaah.” Akawa utasema amefikwa na kifo. Akaenda kwenye mlango wake na hakukuta walinzi nje ya mlango. Akasema: ”Ee Mtume wa Allaah! Sikukujua.” Ndipo akasema: ”Hakika subira huzingatiwa katika pigo la mwanzo.”[5]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Kusema kwamba subira huzingatiwa katika pigo la mwanzo, au huzingatiwa katika pigo la kwanza, kama ilivyokuja katika upokezi mwingine, maana yake ni kuwa kila anayefikwa na msiba mwishoni tu hufanya subira, lakini anayesifiwa ni yule anayesubiri pale ambapo msiba unakuwa mkali na mgumu zaidi. Kwa sababu hata kidonda cha mtu aliyekata tamaa hupona muda utavyokuwa unaenda hata kama atasimama kwenye kaburi la ndugu yake kwa kipindi kirefu.

[1] al-Haakim (2/414).

[2] Ahmad (6/450), al-Bazzaar (2845), at-Twabaraaniy na al-Haakim (1/348) aliyesema kuwa Hadiyth ni Swahiyh kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[3] at-Tirmidhiy (2396) na Ibn Maajah (4031). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (2396).

[4] Ahmad (5/427) na (5/429).

[5] al-Bukhaariy (1283) na (1302), Muslim (626), Abu Daawuud (3124), at-Tirmidhiy (987-988), an-Nasaa’iy (4/22) na Ibn Maajah (1596).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 34-37
  • Imechapishwa: 09/08/2023