04. Hadiyth kuhusu kijakazi ni Swahiyh – na Radd kwa al-Kawthariy

Hadiyth hii imepokelewa kupitia njia nyingi. Pengine ndio maana mtunzi akasema kuwa ni miongoni mwa Hadiyth zilizopokelewa kwa mapokezi mengi. Lakini ni jambo linalotakiwa kutazamwa vyema. Katika baadhi ya mapokezi yamesema kuwa kijakazi huyo alikuwa si mwarabu na kwamba aliashiria juu mbinguni badala ya kusema kwake kuwa yuko juu ya mbingu, kama ilivyotajwa katika “al-Musnad”. Lakini katika mlolongo wa wapokezi wake yuko al-Mas´uudiy ambaye jina lake ni ´Abdur-Rahmaan bin ´Abdillaah bin ´Utbah bin Mas´uud al-Kuufiy ambaye muda ulivyokwenda alikuwa akichanganya mambo. Upokezi huu ameupokea katika michanganyiko hiyo, kwa sababu upo katika “al-Musnad”[1] na katika “as-Sunan”[2] ya al-Bayhaqiy kupitia kwa Yaziyd bin Haaruun. Ibn Numayr amesema:

“Alikuwa mwaminifu. Miaka ilivyoenda alianza kuchanganya mambo. ´Abdur-Rahmaan bin Mahdiy na Yaziyd bin Haaruun wamepokea kutoka kwake Hadiyth mchanganyiko.”

Kwa hivyo maneno ya adh-Dhahabiy katika asili ya kwamba cheni ya wapokezi wake ni nzuri, si nzuri. Kinachotilia nguvu ziada hii “asiyekuwa mwarabu” ni kwamba njia nyenginezo hazikulitaja. Mtunzi amezitaja katika asili. Baadhi yazo ni Swahiyh, nyenginezo hazina neno katika kutilia nguvu.

Nimetaja vyanzo vya Hadiyth na kuihukumu katika ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (862), ”al-Iymaan” (84) ya Ibn Abiy Shaybah na ”Dhwilaal-ul-Jannah” (489).

Hapana shaka kuwa Hadiyth hii ni Swahiyh na hakuna anayetilia shaka hilo isipokuwa tu mjinga au mwenye malengo mabaya na matamanio. Kila wanapofikiwa na andiko litokalo kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allahau ´alayhi wa sallam) linalopingana na ule upotofu waliyomo, basi wanajitahidi kulikwepa kwa kulipindisha maana na bali kulipinga kabisa. Wasipoweza kufanya hivo, basi wanajaribu kutilia kasoro kuthibiti kwake. Kama walivofanya katika Hadiyth hii. Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh na imesahihishwa na maimamu wa fani ya Hadiyth. Miongoni mwao ni Imaam Muslim ambaye ameitaja katika “as-Swahiyh” yake, Abu ´Awaanah katika ”al-Mustakhraj” yake na al-Bayhaqiy katika ”al-Asmaa’ was-Swifaat” yake ambaye amesema mwisho wake:

“Ni Swahiyh na ameipokea Muslim.”[3]

Licha ya hayo, tunamuona al-Kawthariy aliyeangamia kutokana na kasumba zake anafanya kila aliwezalo kutilia shaka juu ya usahihi wake na akadai kuwa Hadiyth ina msukosuko. Ameiwekea taaliki Hadiyth hii katika kitabu ”al-Asmaa’ was-Swifaat” na akasema:

“´Atwaa´ bin Yasaar ameipokea Hadiyth hiyo mwenyewe kutoka kwa Mu´aawiyah bin al-Hakam[4]. Imekuja katika tamko lake, kama ilivyo katika “al-Uluww” ya adh-Dhahabiy, ya kwamba Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pamoja na kijakazi haikuja isipokuwa kwa kuashiria peke yake. Ndipo mpokezi akatamka yale aliyoyafahamu kutokana na ishara hiyo. Kinachojulisha yale tunayosema ni tamko la ´Atwaa´:

“Amenihadithia mwenyewe bwana wa kijakazi.”

Humo imetajwa ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamnyooshea mkono kwa njia ya ishara ya kushangaza na akasema: “Ni nani aliye juu ya mbingu?” Akajibu: “Allaah.” Akasema: “Mimi ni nani?” Akajibu: “Mtume wa Allaah.” Ndipo akasema: “Mwache huru. Kwani hakika ni muislamu.” Hii ni dalili inayoonyesha kuwa swali la “Allaah yuko wapi?” halikuulizwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kama unavyoona usimulizi wa Hadiyth iliyosimuliwa imesababisha mtafaruku huu.”[5]

Hivi ndivo alivosema – Allaah amuhukumu kutokana na uadilifu Wake. Kama unakumbuka, utajua kuwa tumebainisha usahihi wa Hadiyth. Unajua pia kuwa Hadiyth ya ´Atwaa´, kutoka kwa bwana wa kijakazi, haisihi kutokana na cheni ya wapokezi wake. Kwa sababu ni kupitia kwa Sa´iyd bin Zayd. Hata kama yeye kama yeye ni mwaminifu, kumbukumbu yake haikuwa na nguvu. Kwa ajili hiyo wamemdhoofisha wengi. Bali Yahyaa bin Sa´iyd alikuwa akimdhoofisha sana. Haya yameashiriwa na Haafidhw katika “at-Taqriyb” wakati aliposema:

“Ni mwaminifu ambaye ana mawazo.”

Zaidi ya hayo unatakiwa kutambuwa “mkono” na “swali” vilivyotajwa katika upokezi wake. Yeye mwenyewe ndiye amepokea mambo hayo na hayapatikani kwa wale wasimulizi wote wenye kuhifadhi walioipokea Hadiyth hii hata wale walio chini yao. Kitendo cha yeye mwenyewe kuipokea Hadiyth hii, wanazuoni wa fani ya Hadiyth wanaizingatia kuwa ni Hadiyth dhaifu, inayopingana na zile Hadiyth Swahiyh. Hili ni jambo lisilokuwa na shaka yoyote.

Zingatia namna ambavyo al-Kawthariy huyu ametegemea upokezi huu ambao unaenda kinyume. Hakuishilia hapo tu! Bali ameigonganisha na upokezi uliyothibiti na ambao kuna maafikiano juu ya usahihi wake kwa mujibu wa wanazuoni wa fani ya Hadiyth. Sababu ya hilo ameegemea upokezi ambao ni dhaifu kuwa ni dalili juu ya udhaifu na kukanganyika kwa Hadiyth ambayo ni Swahiyh. Nini anachosema muumini juu ya bwana huyu ambaye anaitumia elimu yake katika kuwafanya waislamu waingiwe na mashaka juu ya Hadiyth za Mtume wao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Allaah amfanye kile anachostahiki!

Hakutosheka na upotofu huu. Bali akamshambulia mpokezi na kumtuhukumu kumsemea uwongo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – ilihali anajua kuwa ni mkweli. Kwa sababu wasimuliaji wote wa Hadiyth hii ni waaminifu, pasi na kujali ni nani. Kwa sababu maana ya maneno yake yaliyotangulia ni kwamba msimuliaji yeye mwenyewe ndiye aliweka swali hili mdomoni mwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah yuko wapi?”

al-Kawthariy anaona kuwa yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakusema hivo. Bali msimuliaji mwenyewe ndiye kajizulia jambo hilo badala ya upokezi wa Sa´iyd bin Zayd:

“Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamnyooshea mkono kwa njia ya kushangazwa: “Ni nani aliye juu ya mbingu?”

Kwa ajili hiyo naona kuwa ni wajibu kwangu kuwatadharisha waislamu kutokana na al-Kawthariy huyu na watu mfano wake ambao wanawatuhumu watu wasiokuwa na hatia mambo ambayo hawana. Aidha nawakumbusha maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن جَاءَكُمْ فَاسِقٌ بِنَبَإٍ فَتَبَيَّنُوا أَن تُصِيبُوا قَوْمًا بِجَهَالَةٍ فَتُصْبِحُوا عَلَىٰ مَا فَعَلْتُمْ نَادِمِينَ

“Enyi walioamini! Anapokujieni fasiki kwa habari yoyote, basi pelelezeni msije mkawasibu watu kwa ujinga, mkawa kuwa wenye kujuta juu ya ambayo mmeyafanya.”[6]

[1] al-Musnad (2/291).

[2] as-Sunan (7/388).

[3] Uk. 422

[4] Hivi ndivo alivosema. Allaah ampe kile anachostahiki.

[5] Uk. 421-422

[6] 49:06

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtasar-ul-´Uluww, uk 79-80
  • Imechapishwa: 12/04/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy