1 – Hadiyth ya Mu´aawiyah bin al-Hakam as-Sulamiy (Radhiya Allaahu ´anh). Amesimulia:

“Nilikuwa na kondoo kati ya Uhud na Jawaaniyyah[1] wanaochungwa na kijakazi wangu[2]. Siku moja akaja mbwa mwitu na akamchukua kondoo kutoka kwake. Mimi ni mwanaadamu wa kawaida ambaye hukasirika kama wanavyokasirika watu wengine. Nikaunyanyua mkono wangu na kumpiga kofi. Nikamwendea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumweleza yaliyopitika. Nikasikitika sana na kumwambia: “Ee Mtume wa Allaah! Si nimwache huru?” Akasema: “Mwite.” Nikamwita. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Allaah yuko wapi?” Akajibu: “Juu ya mbingu.” Akamuuliza: “Mimi ni nani?” Akajibu: “Wewe ni Mtume wa Allaah.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Mwache huru. Kwani hakika ni muumini.”[3]

Hadiyth hii ni Swahiyh. Kuna wengi ambao wameipokea kutoka kwa wapokezi waaminifu kutoka kwa Yahyaa bin Abiy Kathiyr, kutoka kwa Hilaal bin Abiy Maymuunah, kutoka kwa ´Atwaa’ bin Yasaar, kutoka kwa Mu´aawiyah as-Sulamiy. Ameipokea Muslim, Abu Daawuud, an-Nasaa’iy na maimamu wengineo katika tungo zao. Wanaipitisha kama ilivyokuja pasi na kupindisha tafsiri wala makengeusho.

*

[al-Albaaniy amesema:]

Tumewaona wale wote wanaoulizwa mahali alipo Allaah basi wanafanya haraka kutokana na maumbile yao na kujibu ya kwamba yuko juu ya mbingu. Hadiyth ina mambo mawili:

1 – Ni jambo limewekwa katika Shari´ah kwa muislamu kuuliza: “Allaah yuko wapi?”

2 – Muulizwaji kujibu: “Yuko juu ya mbingu.”

Yule mwenye kuyapinga mambo haya mawili basi anampinga mteule (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] Kaskazini mwa Madiynah.

[2] Kuna andiko lingine linalomweleza kwamba alikuwa kijakazi mweusi, ambalo amelipokea ad-Daarimiy katika ”ar-Radd ´alaa al-Mariysiy”, uk. 95, kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

[3] Ahmad, Abu Daawuud na wengineo. Imesahihishwa na wengi, ikiwemo “at-Talkhiysw” ambapo amekata moja kwa moja ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema hivo. Nimelibainisha katika “al-Mishkaat”.

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtasar-ul-´Uluww, uk 80-81
  • Imechapishwa: 12/04/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy