02. Hatuna kasumba; Qur-aan, Sunnah na Salaf

Ee mja wa Allaah! Ukipenda inswafu, basi lazimiana na maandiko ya Qur-aan na Sunnah. Baada ya hapo soma yale yaliyosemwa na Maswahabah, wanafunzi wa Maswahabah na maimamu wa tafsiri juu ya Aayah hizi na ´Aqiydah ya Salaf. Ima uzungumze kwa elimu au unyamaze kwa upole. Acha mabishano na mivutano. Kubishana juu ya Qur-aan ni kufuru, kama ilivyotajwa katika Hadiyth Swahiyh. Baada ya kutajwa Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) utayaona maneno ya maimamu juu ya suala hilo.

Allaah azikusanye nyoyo zetu juu ya kumcha na atulinde na mabishano na mivutano. Hakika tumesimama juu ya msingi sahihi na tunayo ´Aqiydah imara juu ya kwamba hakuna chochote kinachoweza kuwa mfano wa Allaah na tunaamini juu ya zile sifa Zake zilizothibiti kama tunavyoamini dhati Yake. Kwani sifa ni zenye kuifuatia dhati. Tunaelewa uwepo wa Muumba na tunaona kuwa hauna mfano, pasi na kutokujua namna yake. Vivyo hivyo ndivo tunavyoamini juu ya sifa Zake. Tunaziamini na tunaelewa uwepo Wake. Tunazitambua kwa ujumla pasi na kuzielewa, kuzishabihisha, kuzifanyia namna au kuzilinganisha na sifa za viumbe Wake. Imaam Maalik na wengineo wamesema kuwa kulingana juu kunatambulika na namna haitambuliki.

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtasar-ul-´Uluww, uk 80
  • Imechapishwa: 12/04/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy