03. Yote ni yenye kutoka kwa Allaah

Qadar, ni mamoja ya kheri na ya shari yake, ndogo na kubwa yake, inayoonekana na iliyojificha, tamu na chungu yake, inayopendeza na inayochukiza, nzuri na mbaya yake, ya mwanzo na ya mwisho wake ni yenye kutoka kwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Amewakadiria na kuwapangia waja Wake. Hakuna yeyote katika wao anayetoka nje ya matakwa ya Allaah (´Azza wa Jall). Hakuna anayevuka mipango Yake. Wote wanafanya yale Aliyowaumbia, wote wanatumbukia kwa yale waliyokadiriwa. Ni jambo lisiloepukika na ni uadilifu kutoka kwa Mola wetu (´Azza wa Jall).

Uzinzi, wizi, unywaji pombe, kuiua nafsi iliyoharamishwa, ushirikina, madhambi na mengine yote yanatokea ni kwa mipango na Qadar ya Allaah. Hakuna kiumbe yeyote aliye na hoja dhidi ya Allaah; bali Allaah ndiye mwenye hoja timilifu juu ya viumbe Wake:

لَا يُسْأَلُ عَمَّا يَفْعَلُ وَهُمْ يُسْأَلُونَ

“Haulizwi [Allaah] kwa yale anayoyafanya, lakini wao wataulizwa.”[1]

Ujuzi wa Allaah (´Azza wa Jall) ni wenye kutendeka juu ya viumbe Wake kwa utashi Wake. Alijua kutoka kwa Ibliys na wengine waliomuasi, tangu wakati Mola wetu (Tabaarak wa Ta´ala) alipoasiwa mpaka kusimama kwa Saa. Amewaumba kwa ajili ya hilo.

Alijua utiifu kutoka kwa wale wenye kumtii. Amewaumba kwa ajili ya hilo. Kila mmoja anatenda kwa kile alichoumbiwa. Kila mmoja ni mwenye kukiendelea kile alichohukumiwa. Hakuna yeyote katika wao anayetoka nje ya makadirio na matakwa ya Allaah. Allaah ni mwenye kufanya kile anachokitaka.

Yule atakayedai kuwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amewataka waja Wake ambao wamemuasi kumtii, lakini waja wao wenyewe ndio wametaka shari na maasi ambapo wakatenda kwa mujibu wa utashi wao, basi amedai kuwa matakwa ya waja ni yenye kushinda matakwa ya Allaah (Tabarak wa Ta´ala). Ni uwongo upi wa kumsemea Allaah mkubwa kuliko huu?

Yule atakayedai kuwa kuna kiumbe ambaye hakiendei kile ambacho alipangiwa, basi amepinga uwezo wa Allaah juu ya viumbe. Huu ni uzushi na kumsemea uwongo Allaah.

Ambaye atadai kuwa uzinzi hautokani na makadirio ataulizwa ikiwa mwanamke huyu ambaye amebeba ujauzito unaotokana na uzinzi na baadaye akazaa – Allaah (´Azza wa Jall) ametaka azaliwe mtoto huyu? Je, Allaah alijua kuwa mtoto huyu atazaliwa? Akisema hapana, basi atakuwa amedai kuwa kuna waumba wengine pamoja na Allaah. Maoni haya hayafanani na shirki peke yake – bali ndio shirki yenyewe.

Ambaye atadai kuwa wizi, unywaji pombe na kula mali ya haramu hakutokani na mipango na makadirio ya Allaah, basi atakuwa amedai kuwa mtu huyu ni muweza wa kula riziki ya mwingine. Maoni haya yanafanana na maoni ya waabudia moto na maoni ya manaswara. Bali huyu amekula riziki Yake. Allaah amempangia aile kwa ile njia aliyoila.

Yule mwenye kudai kuwa kuua hakutokani na mipango ya Allaah (´Azza wa Jall) na kwamba jambo hilo halitokani na kutaka Kwake kwa kiumbe, basi amedai kuwa muuliwa amekufa kabla ya kufika wakati wake. Kuna kumkufuru Allaah kubaya kushinda huku?

Bali yote hayo yanatokana na mipango na makadirio ya Allaah. Yote hayo yanatokana na matakwa na kuwaendesha Kwake viumbe. Yote yanayopitika yametangulia utambuzi Wake juu yao. Allaah ni mwadilifu wa Haki ambaye anafanya Akitakacho.

Yule anayetambua ujuzi wa Allaah basi analazimika vilevile kutambua Qadar na matakwa Yake, kukiwemo kila kidogo na kisichokuwa kizuri kilichopo. Allaah ni mwenye kudhuru na mwenye kunufaisha, mwenye kupotosha na mwenye kuongoza. Amebarikika Allaah, Mbora wa wenye kuumba!

[1] 21:23

  • Mhusika: Imaam Harb bin Ismaa´iyl al-Kirmaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-us-Sunnah, uk. 39-44
  • Imechapishwa: 23/05/2022