03. Shikamana na Qur-aan na Sunnah na usiwe mzushi

Imaam Ibn Abiy Daawuud (Rahimahu Allaah) amesema:

تمسك بحبلِ الله واتبعِ الهُدى

01 – Shikamana na Kamba ya Allaah na ufuate uongofu

ولا تكُ بدعيا لعلك تُفلحُ

     usiwe mzushi huenda ukafaulu

MAELEZO

Mtunzi (Rahimahu Allaah) ameanza kwa kusema:

“Shikamana na Kamba ya Allaah na ufuate uongofu.”

Anamzungumzisha muislamu. Kamba ya Allaah ni Qur-aan na Sunnah. Amechukua haya kutoka katika maneno Yake (Ta´ala):

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

“Shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja wala msifarikiane.” (03:103)

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika yeyote atakayeishi kipindi kirefu katika nyinyi basi atakuja kuona tofauti nyingi. Hivyo basi, jilazimieni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu walioongozwa baada yangu. Shikamaneni nazo barabara na ziumeni kwa magego yenu. Tahadharini na mambo yaliyozuliwa. Hakika kila kilichozushwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”[1]

Shairi hili limechukuliwa kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Ndani yake mna maamrisho ya kushikamana barabara na Kamba ya Allaah ambayo ni Qur-aan na Sunnah. Kwa msemo mwingine unaweza vilevile kusema kuwa Kamba ya Allaah ni Uteremsho Wake aliomteremshia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni mamoja ikawa ni Qur-aan au Sunnah.

Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah):

“Shikamana na Kamba ya Allaah.”

Bi maana shikamana nayo barabara. Amesema (Ta´ala):

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ

“Shikamaneni kwa kamba ya Allaah.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah anaridhia kwenu mambo matatu; mumuabudu na wala msimshirikishe na chochote, mshikamane nyote na kamba ya Allaah na wala msifarikiane na mumnasihi yule ambaye Allaah amemfanya kuyatawalia mambo yenu.”[2]

Ameusia mambo haya matatu ambapo moja wapo ni kushikamana na kamba ya Allaah. Kufanya hivo kunamuepusha mtu na mfarakano na tofauti. Hakutokei tofauti na mfarakano isipokuwa ni kwa sababu ya kutokushikamana na Qur-aan na Sunnah. Hivyo ndivyo ilivyokuwa mfarakano na tofauti ya watu wa Kitabu pamoja na kuwa Allaah aliwateremshia Tawrat na Injiyl. Lakini ilipokuwa hawakushikamana na kamba ya Allaah ndio wakafarikiana na kutofautiana. Kwa ajili hii amesema:

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ تَفَرَّقُوا وَاخْتَلَفُوا مِن بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْبَيِّنَاتُ ۚوَأُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ

“Msiwe kama wale waliofarikiana na wakatofautiana baada ya kuwajia hoja zinazobainisha. Hakika hao watapata adhabu kuu.” (03:105)

Huu ndio mwenendo wa watu wa Kitabu. Waliacha Kitabu cha Mola wao na matokeo yake wakafarikiana.

[1] Abu Daawuud (4607), at-Tirmidhiy (2676) na wengine

[2] Muslim (10) na (1715)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 47-48
  • Imechapishwa: 16/12/2023