03. Salafiyyah ni nini na nani kiongozi wake?

Swali 03: Salafiyyah ni nini? Kiongozi wake ni nani?

Jibu: Salafiyyah ni unasibisho wa Salaf. Salaf ni Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wale waliowafuata kwa wema kuanzia wale watu waliokuwa katika karne tatu bora na waliokuja baada yao. Hii ndio Salafiyyah. Kujinasibisha kwao ina maana ya mtu kujinasibisha na yale waliyokuwemo Maswahabah wa Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na njia ya Ahl-ul-Hadiyth. Ahl-ul-Hadiyth ni wale wenye kufuata mfumo wa Salaf.

Salafiyyah inakuwa katika ´Aqiydah juu ya majina na sifa za Allaah, Qadar, Maswahabah n.k. Mtu Salafiy ni yule ambaye anamuamini Allaah (´Azza wa Jall), kwamba ana majina mazuri na sifa kuu Alizojisifu nazo na akamsifu kwazo Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtu Salafiy anaziamini kwa njia inayolingana na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Anafanya hivo pasi na kupotosha, kufananisha, kushabihisha, kukanusha wala kuzifasiri kimakosa. Vilevile wanaamini Qadar kheri na shari yake. Kwani haitimii imani ya mja mpaka aamini makadirio Aliyoyakadiria Allaah (´Azza wa Jall) juu ya waja Wake. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ

“Hakika sisi Tumekiumba kila kitu kwa makadirio.”[1]

Inapokuja kwa Maswahabah inatakiwa kuamini kuwa ni wajibu kuwatakia radhi Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kuamini kuwa wote ni waadilifu na kwamba wao ndio viumbe na karne bora. Hivi ni tofauti na wanavyoitakidi Shiy´ah na Khawaarij. Wanawakufurisha Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wala hawazitambui haki zao.

Salafiyyah hawana kiongozi mwengine asiyekuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio kiongozi wa Salafiyyah na kiigizo chao chema. Kadhalika Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio viigizo vyao vyema. Msingi wa hilo ni maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mayahudi wamefarikiana katika mapote sabini na moja, manaswara wamefarikiana katika mapote sabini na mbili na Ummah huu utakuja kufarikiana katika mapote sabini na tatu. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu.” Wakasema: “Ni kina nani hao, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Ni wale wataofuata yale ninayofuata mimi hii leo na Maswahabah zangu.”

al-´Irbaadhw bin Saariyah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwatolea Khutbah na kwamba baada ya hapo aliwausia yafuatayo:

“Ninakuusieni kumcha Allaah na kusikiliza na kutii hata kama mtatawaliwa na mtumwa.”

Baada ya hapo akawaamrisha kufuata Sunnah za makhaliyfah wake waongofu. Halafu akasema:

“Ziumeni kwa magego yenu. Tahadharini na mambo ya kuzua. Hakika kila kitachozushwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”

[1] 54:49

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fataawaa al-Jaliyyah
  • Imechapishwa: 16/07/2017