03. Picha ni dhambi kubwa na matishio ya adhabu

Hadiyth zilizotangulia na nyenginezo zilizopokelewa zenye maana kama hii zinafahamisha mafahamisho ya wazi kabisa juu ya uharamu wa picha ya kila chenye roho na kwamba kitendo hicho ni katika madhambi makubwa yaliyotishiwa Moto. Hadiyth ni zenye kuenea aina mbalimbali ya picha. Ni mamoja picha hizo ni zile za kisasa zenye kivuli au nyenginezo. Ni mamoja picha hizo ziko ukutani, kwenye pazia, katika nguo, kio, karatasi au kwenginepo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakupambanua kati ya zile zenye kivuli na nyenginezo au zinazowekwa kwenye pazia au kwenginepo. Bali amemlaani mwenye kutengeneza picha na akakhabarisha kuwa wanaotengeneza picha ndio wenye adhabu kali siku ya Qiyaamah na kwamba kila mtengeneza picha ataingia Motoni. Ameyasema hayo kwa njia isiyofungamana na wala hakubagua kitu.

Ueneaji unapewa nguvu pale alipoona picha iliokuwa katika pazia ya ´Aaishah alilichana na uso wake ukapiga wekundu na kusema:

“Hakika watu wataokuwa na adhabu kali siku ya Qiyaamah ni wale  wanaoigiza maumbile ya Allaah.”[1]

Katika tamko jengine amesema pindi alipoona pazia:

“Hakika watu wa picha hizi ni wenye kuadhibiwa siku ya Qiyaamah na wataambiwa: “Vipeni uhai vile mlivyoviumba!”[2]

Tamko hili na mengine yanaonyesha wazi namna ambavo mtengeneza picha kwenye mapazia na kwenginepo anaingia katika ueneaji wa matishio.

[1] Muslim (2107).

[2] al-Bukhaariy (2105) na Muslim (2107).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Jawaab al-Mufiyd fiy Hukm-it-Taswwiyr kutoka katika Majmuu´-ul-Fataawaa (04/214-215)
  • Imechapishwa: 24/03/2022