al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (Ta´ala) amesema: “Ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule ambaye anajaribu kuumba mfano wa viumbe Wangu? Hebu waumbe mdudu chungu, waumbe punje ya nafaka au waumbe chembe ya shayiri.”[1]

Tamko hili ni la Muslim.

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea tena kupitia kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu watakaokuwa na adhabu kali siku ya Qiyaamah ni wale wanaomuiga Allaah katika uumbaji Wake.”[2]

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea pia kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika watu wa picha hizi ni wenye kuadhibiwa siku ya Qiyaamah na wataambiwa: “Vipeni uhai vile mlivyoviumba!”[3]

Tamko ni la al-Bukhaariy.

al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Juhayfah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza:

“Ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameharamisha thamani ya damu, thamani ya mbwa, chumo la kahaba na amemlaani mwenye kula ribaa, wakala wake na mwenye kuchanja [tattoo], mwenye kuchanjwa na mwenye kutengeneza picha.”

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa ) ameeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Atakayetengeneza picha duniani atakalifishwa kuipulizia roho, jambo ambalo hatoweza.”[4]

Muslim amepokea kupitia kwa Sa´iyd bin Abiyl-Hassan ambaye ameeleza: “Bwana mmoja alikuja kwa Ibn ´Abbaas akasema: “Mimi ni mtu ninayetengeneza picha hizi. Nipe fatwa juu yake.” Akamwambia: “Sogea karibu nami” ambapo akasogea karibu naye. Kisha akamwambia tena: “Sogea karibu nami” ambapo akasogea karibu naye mpaka akaweka mkono wake juu ya kichwa chake na kusema: “Hebu wacha nikuzindue juu ya niliyosikia kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Kila mtengeneza picha ataingia Motoni. Ataiweka kila picha roho ambayo ataadhibiwa kwayo ndani ya Moto. Ikiwa huna budi ila kutengeneza, tengeneza picha za miti na visivokuwa na  nafsi.”[5]

al-Bukhaariy yeye amepokea maneno yake:

“Ikiwa huna budi ila kutengeneza, tengeneza picha za miti na visivokuwa na  nafsi.”

at-Tirmidhiy ameipokea katika “al-Jaamiy´” yake na akasema:

“Ni nzuri na Swahiyh kupitia kwa Abuz-Zubayr kupitia kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia:

“Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza mapicha nyumbani na amekataza kufanya hivo.”[6]

Muslim amepokea kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye ameeleza:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingia kwangu na mimi nilikuwa nimefunika kwa pazia chumba changu cha hazina ambacho kilikuwa na  masanamu. Aliponiona, basi alilichana na uso wake ukapiga wekundu na kusema: “Ee ´Aaishah! Hakika watu wataokuwa na adhabu kali siku ya Qiyaamah ni wale  wanaoigiza maumbile ya Allaah. Aaishah anaendelea kusimulia: “Basi tukalikata na kulifanya mto au mito miwili. Nilimuona akigemea mto mmoja wapo ilihali ulikuwa na picha.”[7]

 ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifika kutoka safarini na nilikuwa nimefunika kwa pazia chumba changu cha hazina ambacho kilikuwa na  masanamu. Wakati Mtume wa Allaah Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliponiona, basi aliliachana na akasema:

“Hakika watu wataokuwa na adhabu kali siku ya Qiyaamah ni wale  wanaoigiza maumbile ya Allaah. Aaishah anaendelea kusimulia: “Basi tukalikata na kulifanya mto au mito miwili.”[8]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim ambaye amezidisha baada ya maneno yake:

“… uso wake ukapiga wekundu… “

al-Bukhaariy amepokea kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye ameeleza:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifika kutoka safarini na nilikuwa nimefunika kwa pazia lililokuwa na picha. Akaniamrisha niiondoshe na nikafanya hivo.”[9]

Imekuja katika tamko la Muslim:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifika kutoka safarini na nilikuwa nimefunika mlango kwa pazia ambalo lilikuwa na picha zilizo na farasi wenye mbawa. Akaniamrisha ambapo nikaiondosha.”[10]

al-Qaasim bin Muhammad amepokea kupitia kwa ´Aaishah tena ambaye ameeleza:

“Nilinunua mto uliokuwa na picha. Wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipouona akasimama kwenye mlango na hakuingia ndani. Kukatambulika usoni mwake kuchukia. Nikasema: “Tuna nini, ee Mtume wa Allaah? Natubu kwa Allaah na kwa Mtume Wake. Nimefanya dhambi gani?” Akasema: “Vipi kuhusu mto huu?” Nikasema: “Ni mto nimeununua ili uweze kukaa juu yake na kuegemea.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Hakika watu wa picha hizi wataadhibiwa na wataambiwa: “Vipeni uhai vile mlivyoviumba.” Kisha akasema: “Hakika nyumba ilio na picha hawaingii Malaika.”[11]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim ambaye amezidisha kupitia kwa Ibn al-Maajishuwna ambapo ´Aaishah amesema:

“Nikaichukua na kuifanya mito miwili. Alikuwa akiiegemea nyumbani.”

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Malaika hawaingii ndani ya nyumba yenye mbwa na picha.”[12]

Muslim amepokea kupitia kwa Zayd bin Khaalid, kutoka kwa Abu Twalhah ambaye ameleeza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Malaika hawaingii ndani ya nyumba yenye mbwa na masanamu.”[13]

al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameleeza kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Sisi hatuingii nyumba yenye mbwa na picha.”[14]

Muslim amepokea kupitia kwa ´Aaishah na Maymuumah Hadiyth mfano wake.

Muslim amepokea kutoka kwa Abul-Hayyaaj ambaye ameeleza kwamba ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) alimwambia:

“Hivi nisikutume juu ya kazi aliyonituma kwayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Usiache picha hata moja isipokuwa umeiharibu wala kaburi lililoinuka isipokuwa umelisawazisha.”[15]

Abu Daawuud amepokea kwa cheni ya wapokezi nzuri kupitia kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwamrisha ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) kipindi cha Ufunguzi akiwa Batwhaa´ aiendee Ka´bah na afute kila picha iliokuwepo hapo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuingia ndani mpaka zilipofutwa picha zote zilizokuwepo hapo.

Abu Daawuud at-Twayaalisiy amepokea katika “Musnad” kupitia kwa Usaamah ambaye amesema:

“Niliingia kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Ka´bah na akaona picha. Akaniagiza ndoo ya maji na nikamletea ambapo akawa anaifuta na kusema: “Allaah awalaani watu wanaotengeneza picha ya vitu wasivoviumba.”

Haafidhw [Ibn Hajar] amesema:

“Cheni ya wapokezi ni nzuri.”

Amesema:

´Umar bin Shabh amepokea kupitia kwa ´Abdur-Rahmaan bin Mahraan kutoka kwa ´Umayr, mtumwa aliyeachwa huru na Ibn ´Abbaas, kutoka kwa Usaamah ambaye ameeleza:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingia katika Ka´bah na akaniamrisha ambapo nikamletea ndoo ya maji na akawa anazilowesha zile nguo na akizipiga picha na akisema: “Allaah awalaani watu wanaotengeneza picha ya vitu wasivoviumba.”

al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye ameeleza:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwa akiacha nyumbani kwake kitu kilicho na misalaba isipokuwa hukivunja.”[16]

al-Kashmihniy ameipokea kwa tamko lisemalo:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwa anaacha nyumbani kwake kitu kilicho na picha isipokuwa hukivunja.”

al-Bukhaariy ameitengenezea mlango unaosema: “Mlango kuhusu kuvunja picha” kisha akataja Hadiyth hii.

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Bisr bin Sa´iyd, kutoka kwa Zayd bin Khaalid, kutoka kwa Abu Twalhah ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Malaika hawaingii ndani ya nyumba yenye picha.”[17]

Bisr amesema:

“Zayd akalalamika ambapo tukarudi. Tahamaki mlangoni mwake kulikuwa na pazia lililokuwa na picha. Nikasema kumwambia ´Ubaydullaah al-Khawlaaniy, mtoto wa kambo wa Maymuunah ambaye ni mkewe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Je, Zayd si alitwambia kuhusu picha ile siku ya kwanza?” ´Ubaydullaah akasema: “Hukumsikia pindi aliposema: “Isipokuwa iliyotandazwa kwenye nguo.” Katika upokezi mwingine wa wawili hao kupitia katika njia ya ´Amr bin al-Haarith, kutoka kwa Bukayr al-Ashajj, kutoka kwa Bisr: “Nikasema kumwambia ´Ubaydullaah al-Khawlaaniy: “Je, hakutuzungumzia kuhusu picha?” Akasema: “Alisema isipokuwa iliyotandazwa kwenye nguo. Hukumsikia?” Nikasema: “Hapana.” Akasema: “Ndio, alisema hivo.”

Imekuja katika “al-Musnad” ya an-Nasaa´iy:

“Kutoka kwa ´Ubaydullaah bin ´Abdillaah ya kwamba aliingia kwa Abu Twalhah al-Answaariy kumtembelea ambapo akamkuta hapo kwake Sahl bin Abiy Haniyf. Abu Twalhah akamwamrisha mtu mmoja aondoshe mifumo ilioko chini yake. Sahl akamuuliza: “Ni kwa nini unaiondosha?” Akamjibu: “Kwa sababu ina na picha na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema yale uliyokwishajua.” Akasema: “Je, si alisema: “Isipokuwa iliyotandazwa kwenye nguo.” Akamjibu: “Ni kweli. Lakini ni vizuri zaidi kwa nafsi yangu.”[18]

Cheni ya wapokezi wake ni nzuri. Ameipokea at-Tirmidhiy kwa tamko hili na akasema:

“Nzuri na Swahiyh.”

Ameipokea Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa´iy kwa cheni nzuri kupitia kwa Abu Hurayrah ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Jibriyl alinijia akasema: ”Nilikuwa nimekujia jana usiku. Hakuna kilichonizuia kuingia ndani ya nyumba uliyokuwemo isipokuwa ni kwamba kulikuwa na kinyago cha sanamu cha mwanamme. Katika nyumba kulikuweko kinyago cha sanamu katika pazia. Amrisha kichwa cha kinyago hicho kikatwe kiwe na umbile kama la mti. Amrisha pazia ikatwe na kufanywe mito miwili inayokanyagwa chini. Amrisha mbwa atolewe nje.” Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akafanya hivo. Mbwa huyo alikuwa ni kilebu cha al-Hasan na al-Husayn kilichokuwa chini ya kitanda chao.”[19]

Hili ni tamko la Abu Daawuud na tamko la at-Tirmidhiy ni mfano wake. Tamko la an-Nasaa´iy ni kama ifuatavyo:

“Jibriyl alimwomba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) idhini ya kuingia ambapo akamwambia: “Ingia ndani.” Akasema: “Ni vipi nitaingia na nyumbani kwako kuna pazia lililo na picha? Ima ukate kichwa chake au uifanye zulia linalokanyagwa. Kwani hakika sisi Malaika hatuingii nyumba ilio na picha.”[20]

Zipo Hadiyth nyenginezo nyingi juu ya maudhui haya mbali na tulizotaja.

[1] al-Bukhaariy (5953) na (7559) na Muslim (2111).

[2] al-Bukhaariy (5954) na Muslim (2107).

[3] al-Bukhaariy (2105) na Muslim (2107).

[4] al-Bukhaariy (5963) na Muslim (2110).

[5] Muslim (2110) na Ahmad (01/308).

[6] at-Tirmidhiy (1749) na Muslim (03/335).

[7] Muslim (2107).

[8] al-Bukhaariy (5954).

[9] al-Bukhaariy (5956).

[10] Muslim (2107).

[11] al-Bukhaariy (2105), Muslim (2107), Ahmad (06/246) na Maalik (1803).

[12] al-Bukhaariy (3225), Muslim (2106), at-Tirmidhiy (2804), an-Nasaa´Iy (5348), Abu Daawuud (4153), Ibn Maajah (3649) na Ahmad (04/30).

[13] Muslim (2106).

[14] al-Bukhaariy (3227).

[15] Muslim (969).

[16] al-Bukhaariy (5952) na Abu Daawuud (4151).

[17] al-Bukhaariy (3226), Muslim (2106), Abu Daawuud (4155) na Ahmad (04/30).

[18] at-Tirmidhiy (1750), an-Nasaa´iy (5349) na Maalik (1802).

[19] at-Tirmidhiy (2806) na Abu Daawuud (4158).

[20] an-Nasaa´iy (5365).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Jawaab al-Mufiyd fiy Hukm-it-Taswwiyr kutoka katika Majmuu´-ul-Fataawaa (04/210-214)
  • Imechapishwa: 24/03/2022