Swali 03: Ni ipi hukumu ya punyeto?

Jibu: Punyeto – ambako ni kule kujistarehesha kwa kutumia mkono au kitu kingine mfano wake – ni jambo la haramu kwa dalili ya Qur-aaan, Sunnah na utafiti sahihi. Kuhusu Qur-aan ni maneno Yake (Ta´ala):

وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ إِلَّا عَلَىٰ أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ فَمَنِ ابْتَغَىٰ وَرَاءَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْعَادُونَ

”Na wale ambao wanazihifadhi tupu zao, isipokuwa kwa wake zao au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, basi hao si wenye kulaumiwa. Basi yeyote yule atakayetaka kinyume ya hivo, basi hao ndio wavukao mipaka.”[1]

Yule ambaye anatafuta kukidhi matamanio yake kwa asiyekuwa mkewe au kijakazi wake, basi hakika ametaka kinyume na hivo na matokeo yake anakuwa amechupa mipaka kwa mujibu wa Aayah hii tukufu.

Kuhusu Sunnah, amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Enyi kongamano la barobaro! Yule atakayeweza miongoni mwenu kuoa basi na aoe. Hakika hilo linamfanya ainamishe macho na inahifadhi utupu wake. Yule asiyeweza basi ni juu yake afunge. Kwani kwake ni kinga.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwamrisha ambaye hana uwezo wa kuoa afunge. Endapo kufanya punyeto ingekuwa ni jambo linafaa, basi angelielekeza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Pale ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakulielekeza – pamoja na wepesi wake – ndipo ikatambulika kuwa haijuzu.

Kuhusu utafiti sahihi, ni yale madhara makubwa yanayopelekea katika kitendo hichi. Madaktari wametaja kuwa linapelekea katika madhara makubwa yanayouathiri mwili, msukumo wa kujamiiana, fikira na tabia. Pengine hata likamzuilia kuoa, kwa sababu pengine mtu akapuuzilia mbali kuoa pale anapokidhi matamanio yake kwa njia kama hizi.

[1] 23:05-07

[2] al-Bukhaariy na Muslim.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah Muhimmah, uk. 9
  • Imechapishwa: 23/02/2023