02. Ni ipi hukumu ya kuwadhihaki wale wenye kushikamana na maamrisho ya Allaah na Mtume Wake?

Swali 02: Ni ipi hukumu ya kuwachezea shere wale wenye kushikamana na maamrisho ya Allaah na Mtume Wake?

Jibu: Kuwafanyia istihzai wale wenye kushikamana na maamrisho ya Allaah na Mtume Wake kwa sababu wamelazimiana na mambo hayo, ni jambo la haramu na la khatari sana kwa mtu. Kwa sababu kunakhofiwa kule kuwachukia kwake ni kuichukia ile hali waliyomo ambayo ni kunyooka juu ya dini ya Allaah. Hivyo inakuwa maana yake, ni kuchezea shere ile njia waliyomo na hivyo wanakuwa wamefanana na wale ambao Allaah amesema juu yao:

قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Sema:  Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?”  Msitoe udhuru; mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.”[1]

Aayah hii imeteremka juu ya wanafiki waliosema:

”Hatujaona mfano wa wasomaji wetu hawa ambao wana matumbo makubwa, wanasema uwongo sana na ni waoga vitani.”

Wakimkusudia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake. Hapo ndipo Allaah akateremsha Aayah hii. Hivyo basi watahadhari wale wanaowafanyia dhihaka watu wa haki, kwa sababu wameshikamana na dini. Kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

إِنَّ الَّذِينَ أَجْرَمُوا كَانُوا مِنَ الَّذِينَ آمَنُوا يَضْحَكُونَ وَإِذَا انقَلَبُوا إِلَىٰ أَهْلِهِمُ انقَلَبُوا فَكِهِينَ وَإِذَا مَرُّوا بِهِمْ يَتَغَامَزُونَ وَإِذَا رَأَوْهُمْ قَالُوا إِنَّ هَـٰؤُلَاءِ لَضَالُّونَ وَمَا أُرْسِلُوا عَلَيْهِمْ حَافِظِينَ فَالْيَوْمَ الَّذِينَ آمَنُوا مِنَ الْكُفَّارِ يَضْحَكُونَ عَلَى الْأَرَائِكِ يَنظُرُونَ هَلْ ثُوِّبَ الْكُفَّارُ مَا كَانُوا يَفْعَلُونَ 

“Hakika wale waliofanya ukhalifu walikuwa [duniani] wakiwacheka wale walioamini. Na wanapowapitia [karibu yao], basi wanakonyezana, na wanaporudi kwa familia zao, hurudi hali ya kuwa ni wenye kufurahika kwa kejeli, na wanapowaona, husema: “Hakika hawa bila shaka ndio waliopotea.” Hawakutumwa kuwa ni walinzi juu yao. Basi hii leo wale walioamini watawacheka makafiri. Kwenye makochi ya fakhari wakitazama. Je, basi makafiri wamelipwa yale waliyokuwa wakiyafanya?”[2] 

[1] 09:65-66

[2] 83:29-36

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah Muhimmah, uk. 8
  • Imechapishwa: 23/02/2023