01. Ni yepi maoni yako juu ya ambaye umebadilika ufahamu wake kiasi cha kwamba, mema yamekuwa maovu na maovu yamekuwa mema?

Swali 01: Ni yepi maoni yako juu ya ambaye umebadilika ufahamu wake kiasi cha kwamba, mema yamekuwa maovu na maovu yamekuwa mema?

Jibu: Maoni yangu juu ya watu hawa ambao umebadilika ufahamu wao kiasi cha kwamba, wakaona mema ni maovu na maovu ni mema na hatimaye wakawa hawakemei chochote katika maovu na hawatambui chochote katika dini, naona kuwa wametoka nje ya dini – na tunamuomba Allaah ulinzi. Hivyo ni kwa sababu ambaye anaona mema, ambayo ni sehemu katika Shari´ah ya Allaah, kuwa ni maovu basi ameikufuru Shari´ah. Vivyo hivyo yule mwenye kuona maovu kuwa ni mema basi ameamini waungu wa batili na ukafiri. Imani haikamiliki isipokuwa kwa kukufuru waungu wa batili na ukafiri na sambamba na hilo mtu akamwamini Allaah. Ni lazima kwa watu hawa wazirejee nafsi zao, wafikirie hali zao, watambue msingi wao na mwisho wa jambo lao. Mwisho wao ni kutokuwepo na mwisho wa jambo lao ni kutokomea duniani. Amesema (Ta´ala):

هَلْ أَتَىٰ عَلَى الْإِنسَانِ حِينٌ مِّنَ الدَّهْرِ لَمْ يَكُن شَيْئًا مَّذْكُورًا

”Je, mtu hakufikiwa na kipindi fulani katika dahari, hakuwa kitu kinachotajwa?”[1]

كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ

”Kila aliyekuwa humo [mbinguni na ardhini] atatoweka. Na utabakia uso wa Mola Wako wenye utukufu na wenye ukarimu.”[2]

كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ وَإِنَّمَا تُوَفَّوْنَ أُجُورَكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ

”Kila nafsi itaonja mauti na hakika si vyenginevyo mtatimiziwa malipo yenu siku ya Qiyaamah.”[3]

Ni lazima kwao wayafikirie hayo kwa kina. Lisiposaidia, basi wafikirie tena kwa kina. Wanaona watu namna wanavyoondoka na kuja, wanazaana na wanakufa, wanagonjweka, wanapata uzima na wanapewa mtihani katika mali zao na familia zao. Wanajua kuwa hakuna yeyote atakayebaki katika duniani. Hivyo basi, warejee kwa Allaah (Ta´ala), watambue yaliyo mema na wayakemee yaliyo maovu. Hakika Allaah anamsamehe yule mwenye kutubia Kwake.

[1] 76:01

[2] 55:26

[3] 03:185

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah Muhimmah, uk. 7-8
  • Imechapishwa: 23/02/2023