Kufuata (التقليد) kilugha ni kuweka mkufu shingoni. Maana yake kiistilahi ni kufuata maoni ya wengine pasi na hoja. Ni kitu kinachofaa kwa ambaye hawezi kufikia elimu yeye mwenyewe. Amesema (Ta´ala):

فَاسْأَلُواْ أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لاَ تَعْلَمُونَ

“Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui.”[1]

Madhehebu yanayotambulika ni manne:

1 – Madhehebu ya Hanafiyyah. Imamu wake ni Abu Haniyfah an-Nu´maan bin Thaabit. Huyu ni imamu wa watu wa ´Iraaq. Amezaliwa mwaka wa 80 baada ya kuhajiri na akafa mwaka wa 150 baada ya kuhajiri.

2 – Madhehebu ya Maalikiyyah. Imamu wake ni Abu ´Abdillaah Maalik bin Anas. Ni imamu wa watu wa al-Madiynah. Alizaliwa mwaka wa 93 baada ya kuhajiri na akafa mwaka wa 179 baada ya kuhajiri.

3 – Madhehebu ya ash-Shaafi´iyyah. Imamu wake ni Abu ´Abdillaah Muhammad bin Idriys ash-Shaafi´iy. Alizaliwa mwaka wa 150 baada ya kuhajiri na akafa mwaka wa 204 baada ya kuhajiri.

4 – Madhehebu ya Hanbaliyyah. Imamu wake ni Abu ´Abdillaah Ahmad bin Muhammad bin Hanbal. Alizaliwa mwaka wa 164 baada ya kuhajiri na akafa mwaka wa 241 baada ya kuhajiri.

Kuna madhehebu mengine kama vile madhehebu ya Dhwaahiriyyah, Zaydiyyah, Sufyaaniyyah na mengineyo. Kila mmoja yanachukuliwa maneno yake yaliyokuwa ya sawa na yanaachwa maneno yake yaliyo ya kimakosa. Hakuna kukingwa na makosa isipokuwa katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Tunamuomba Allaah atujaalie miongoni mwa wale wenye kushikamana na Kitabu Chake na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa nje na kwa ndani, atufishe juu ya hilo, atulinde duniani na Aakhirah, asizipotoshe nyoyo zetu baada ya kutuongoza, atutunuku rehema kutoka Kwake. Kwani hakika Yeye ndiye Mwenye kutunuku.

Himdi zote njema ni Zake kama anavopenda na kuridhia Mola wetu na kama inavyopaswa kuwa kwa ukarimu wa uso Wake (´Azza Jalaaluh). Sifa njema ni za Allaah ambaye kwa neema yake yanatimia mambo mema. Swalah na amani ziwe juu ya Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

Imetimia siku ya ijumaa sawa na tarehe 10/01/1392 kwa kalamu ya mtunzi ambaye ni fakiri kwa Allaah; Muhammad Swaalih al-´Uthaymiyn

[1] 16:43

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 165-167
  • Imechapishwa: 23/02/2023