03. Mtazamo wa Ahl-ul-Hadiyth juu ya mikono ya Allaah

Hawaoni kuwa sifa Zake zinafanana na sifa za viumbe Wake. Kwa mfano wanasema kuwa Amemuumba Aadam kwa mikono Yake, kama alivoyasema hayo waziwazi:

مَا مَنَعَكَ أَن تَسْجُدَ لِمَا خَلَقْتُ بِيَدَيَّ

”Kipi kilichokuzuia usimsujudie Niliyemuumba kwa mikono Yangu?”[1]

Hawayakengeushi maneno kuyaondoa mahala pake kwa njia ya kwamba wakapindisha maana mikono miwili kuwa ni neema mbili au nguvu mbili, kama wanavopindisha Mu´tazilah na Jahmiyyah. Wala hawaziwekei namna wala kuzifananisha na mikono ya viumbe, kama wanavofanya Mushabbihah. Allaah (Ta´ala) amewakinga Ahl-us-Sunnah kutokana na upotoshaji, kufananisha na kufanya namna, na akawatunuku utambuzi na uelewa. Hivyo wakawa wamepita juu ya njia ya Tawhiyd na matakosa kutokana na mapungufu, na wakajiepusha na ukanushaji na ushabihishaji. Hivyo wakafuata maneno Yake Allaah (´Azza wa Jall):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote.”[2]

Kama ambavo Qur-aan imetaja mikono miwili pale aliposema:

مَا مَنَعَكَ أَن تَسْجُدَ لِمَا خَلَقْتُ بِيَدَيَّ

”Kipi kilichokuzuia usimsujudie Niliyemuumba kwa mikono Yangu?”

بَلْ يَدَاهُ مَبْسُوطَتَانِ يُنفِقُ كَيْفَ يَشَاءُ

”Bali mikono Yake imekunjuliwa hutoa atakavyo.”[3]

Khabari Swahiyh kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´aalyhi wa sallam) zimetamka waziwazi mkono, ikiwa ni pamoja na maneno ya Muusa kumwambia Aadam:

”Allaah amekuumba kwa mkono Wake na Malaika Wake wakakusujudia.”[4]

Vilevile maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Sintofanya dhuriya njema ya ambaye Nimemuumba kwa mkono Wangu kuwa kama ambaye Nimemuumba kwa kusema ”Kuwa!” na akawa.”[5]

na:

”… na Allaah ameiumba Firdaws kwa mkono Wake.”[6]

[1] 38:75

[2] 42:11

[3] 5:64

[4] Ibn Mandah katika ”Kitaab-ul-Iymaan” (11) na (13) na ad-Daaraqutwniy (207).

[5] al-Bayhaqiy katika ”al-Asmaa’ was-Swifaat” (688). Cheni yake ya wapokezi ni salama kwa mujibu wa adh-Dhahabiy katika “al-´Uluww”, uk. 66.

[6] al-Bayhaqiy amesema:

”Kuna Swahabah aliyekosekana katika cheni ya wapokezi, Mursal.” (al-Asmaa’ was-Swifaat (2/125))

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 161-164
  • Imechapishwa: 29/11/2023