Nasema – na tawfiyq yote iko kwa Allaah:

Ahl-ul-Hadiyth wanaoshikamana barabara na Qur-aan na Hadiyth – Allaah awahifadhi wale waliohai katika wao na awarehemu wale waliokwishakufa – wanamshuhudia Allaah (Ta´ala) umoja na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ujumbe na unabii. Wanamtambua Mola Wao (´Azza wa Jall) kwa sifa Zake ambazo zimezungumzwa na wahy na uteremsho wake au ambazo amezishuhudia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika zile khabari Swahiyh zilizothibiti na wakazinukuu wasimulizi waadilifu na wenye kuaminika kutoka kwake. Wanamthibitishia (Jalla wa ´Alaa) yale aliyojithibitishia Mwenyewe na yale aliyomthibitishia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Vivyo hivyo wanasema juu ya sifa zote zilizotajwa na Qur-aan na khabari Swahiyh, kukiwemo kusikia, kuona, jicho, uso, ujuzi, uwezo, utukufu, ukubwa, matakwa, utashi, neno, maneno, kuridhia, kuchukia, uhai, kuwa macho, mapenzi na kucheka, pasi na kufananisha sifa yoyote na sifa za viumbe wenye kuendeshwa na walioumbwa. Bali wanakomeka na yale aliyosema Allaah (Ta´ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), bila kupunguza wala kuongeza kitu juu yake, kuzifanyia namna wala kuzishabihisha, wala kuzipotosha, kuzibadilisha wala kuzigeuza. Hawaondoshi matamshi ya mapokezi kutoka nje ya ile maana wanayoijua waarabu kwenda katika tasiri zilizosimangwa. Wanazipitisha juu ya udhahiri wake na kumtegemezea ujuzi Wake Allaah (Ta´ala). Wanakiri ya kwamba hakuna yeyote anayejua tafsiri yake isipokuwa Allaah pekee, kama ambavo Allaah ameeleza juu ya wale waliobobea katika elimu ya kwamba wanasema pale Aliposema (Ta´ala):

وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ يَقُولُونَ آمَنَّا بِهِ كُلٌّ مِّنْ عِندِ رَبِّنَا ۗ وَمَا يَذَّكَّرُ إِلَّا أُولُو الْأَلْبَابِ

“Ama wale waliobobea katika elimu husema: “Tumeziamini; zote ni kutoka kwa Mola wetu”, na hawakumbuki isipokuwa wale wenye akili.”[1]

[1] 03:07

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 9
  • Imechapishwa: 29/11/2023