03. Kutoongeza wala kupunguza ili mtu aweze kuingia Peponi

5 – Shabaabah bin Sawwaar ametuhadithia: Sulaymaan bin al-Mughiyrah ametueleza, kutoka kwa Thaabit, kutoka kwa Anas ambaye amesema:

”Tulikuwa tumekatazwa kumuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kitu, na tulikuwa tukipendezwa ajiliwe na mtu mwenye busara katika mabedui na kumuuliza na sisi huku tunasikiza. Siku moja akaja mbedui mmoja na kusema: ”Ee Mtume wa Allaah! Amekuja mjumbe wako na kudai kuwa wewe unadai ya kwamba Allaah amekutuma.” Akasema: ”Amesema kweli.” Akasema: ”Ni nani aliyeziumba mbingu?” Akasema: ”Allaah.” Akasema: ”Ni nani ameziumba ardhi?” Akasema: ”Allaah.” Akasema: ”Ni nani aliyesimamisha milima hii?” Akasema: ”Allaah.” Akasema: ”Naapa kwa Ambaye ameziumba mbingu na ardhi na akasimamisha milima – Allaah ndiye amekutuma?” Akasema: ”Ndio.” Akasema: ”Mjumbe wako anadai kuwa tunalazimika kuswali swalah tano kwa siku.” Akasema: ”Amesema kweli.” Akasema: ”Naapa kwa Ambaye ameziumba mbingu na ardhi na akasimamisha milima – Allaah ndiye amekuamrisha mambo haya?” Akasema: ”Ndio.” Akasema: ”Mjumbe wako anadai kuwa tunalazimika kufunga mwezi mmoja kwa mwaka.” Akasema: ”Amesema kweli.” Akasema: ”Naapa kwa Ambaye ameziumba mbingu na ardhi na akasimamisha milima – Allaah ndiye amekuamrisha mambo haya?” Akasema: ”Ndio.”  Akasema: ”Mjumbe wako anadai kuwa tunalazimika kuhiji kwa yule mwenye kuweza kufanya hivo.” Akasema: ”Amesema kweli.” Akasema: ”Naapa kwa Ambaye ameziumba mbingu na ardhi na akasimamisha milima – Allaah ndiye amekuamrisha mambo haya?” Akasema: ”Ndio.” Akasema: ”Naapa kwa Ambaye amekutuma kwa haki kwamba sintozidisha wala kuongeza juu yake kitu.” Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Akiwa mweli, basi ataingia Peponi.”[1]

[1] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy na Muslim. Wote wawili wameipokea kupitia njia nyingine kutoka kwa Sulaymaan bin al-Mughiyrah.

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiy Shaybah al-Kuufiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 17-18
  • Imechapishwa: 05/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy