03. Imani sawa kama ya Malaika na Mitume?

Hata hivyo si katika ´Aqiydah ya wanazuoni kusema kwamba ni waumini na wakakusudia imani yenye nguvu kama Malaika na Mitume. Machukizo yao juu ya jambo hilo yamepokelewa kwa njia nyingi.

17 – Ima Hushaym ametuhadithia au nimehadithia kutoka kwake, kutoka kwa Juwaybir, kutoka kwa adh-Dhwahhaak kwamba alikuwa akichukia mtu kusema:

“Mimi nina imani kama ya Jibriyl na Mikaaiyl.”

18 – Sa´iyd bin Abiy Maryam al-Miswriy ametuhadithia, kutoka kwa Naafiy´, kutoka kwa ´Umar al-Jamhiy ambaye amesema:

“Nilimsikia bwana mmoja akimwambia Ibn Abiy Mulaykah: “Kuna mtu mmoja katika darsa zako anasema kuwa imani yake ni kama imani ya Jibriyl.” Akakaripia jambo hilo na kusema: “Allaah ametakasika kutokana na mapungufu! Allaah amemfadhilisha Jibriyl (´alayhis-Salaam) wakati alipomsifu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema:

إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ ذِي قُوَّةٍ عِندَ ذِي الْعَرْشِ مَكِينٍ مُّطَاعٍ ثَمَّ أَمِينٍ

“Hakika hii bila shaka ni kauli ya Mjumbe mtukufu. Mwenye nguvu na cheo kitukufu kwa Mwenye kumiliki ‘Arshi. Anayetiiwa mwaminifu.”[1]

19 – Tumehadithia kutoka kwa Maymuun bin Mihraan ambaye amesema kwamba:

“Alimuona kijakazi mmoja akiimba akasema: “Mwenye kudai kuwa huyu ana imani sawa kama Maryam bint ´Imraan amesema uwongo.”

Ni vipi mtu anaweza kuwafananisha watu na Malaika? Allaah katika maeneo mengi ndani ya Qur-aan amewatishia watu matishio makali, lakini haitambuliki kuwa amefanya hivo kwa Malaika:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَكُم بَيْنَكُم بِالْبَاطِلِ إِلَّا أَن تَكُونَ تِجَارَةً عَن تَرَاضٍ مِّنكُمْ ۚ وَلَا تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ عُدْوَانًا وَظُلْمًا فَسَوْفَ نُصْلِيهِ نَارًا ۚ وَكَانَ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرًا

“Enyi walioamini! Msiliane mali zenu kwa ubatilifu, isipokuwa iwe biashara kwa kuridhiana baina yenu. Wala msijiue. Hakika Allaah ni Mwenye kuwarehemuni. Na atakayefanya hivyo kwa uadui na dhuluma, basi tutamwingiza Motoni – na hilo kwa Allaah ni jepesi mno.”[2]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَذَرُوا مَا بَقِيَ مِنَ الرِّبَا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ فَإِن لَّمْ تَفْعَلُوا فَأْذَنُوا بِحَرْبٍ مِّنَ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ ۖ وَإِن تُبْتُمْ فَلَكُمْ رُءُوسُ أَمْوَالِكُمْ لَا تَظْلِمُونَ وَلَا تُظْلَمُونَ

 “Enyi walioamini! Mcheni Allaah na acheni yaliyobakia katika ribaa ikiwa kweli nyinyi ni waumini. Msipofanya, basi tangazeni vita kutoka kwa Allaah na Mtume wake na mkitubu basi mtapata rasilimali zenu – msidhulumu na wala msidhulumiwe.”[3]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لِمَ تَقُولُونَ مَا لَا تَفْعَلُونَ كَبُرَ مَقْتًا عِندَ اللَّـهِ أَن تَقُولُوا مَا لَا تَفْعَلُونَ

“Enyi walioamini!  Kwanini mnasema yale msiyoyafanya? Ni chukizo kubwa kabisa mbele ya Allaah kwamba mnasema yale msiyoyafanya.”[4]

أَلَمْ يَأْنِ لِلَّذِينَ آمَنُوا أَن تَخْشَعَ قُلُوبُهُمْ لِذِكْرِ اللَّـهِ وَمَا نَزَلَ مِنَ الْحَقِّ وَلَا يَكُونُوا كَالَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِن قَبْلُ فَطَالَ عَلَيْهِمُ الْأَمَدُ فَقَسَتْ قُلُوبُهُمْ ۖ وَكَثِيرٌ مِّنْهُمْ فَاسِقُونَ

“Je, haujafika wakati kwa walioamini zinyenyekee nyoyo zao kwa ukumbusho wa Allaah na yale yaliyoteremka ya haki, na wala wasiwe kama wale waliopewa Kitabu kabla, ukawarefukia muda, halafu zikawa ngumu nyoyo zao – na wengi miongoni mwao wakatumbukia katika madhambi na kuasi?”[5]

Katika Aayah ya kwanza amewatishia Moto, katika Aayah ya pili kupigana Naye vita, katika Aayah ya tatu amewakhofisha kwa chuki na katika Aayah ya nne kule kuchelewa kwao. Pamoja na yote haya amewaita waumini. Ni vipi basi watu hawa wanaweza kufanana na Jibriyl na Mikaaiyl pamoja na nafasi walizonazo mbele ya Allaah? Nachelea ´Aqiydah kama hiyo iwe ni kufanya ujasiri wa kipumbavu dhidi ya Allaah na kuwa mjinga juu ya Kitabu Chake.

[1] 81:19-21

[2] 4:29-30

[3] 2:278-279

[4] 61:2-3

[5] 57:16

  • Mhusika: Imaam Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 41-44
  • Imechapishwa: 25/06/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naawswir-ud-Diyn al-Albaaniy