02. Kuvua au kuthibitisha imani? Makinzano ya Salaf

Kwa ajili hiyo Sufyaan na wale waliokuwa wakiafikiana naye walikuwa wakifanya uvuaji katika imani. Kama tulivyotangulia kusema katika mlango wa kwanza, naona kuwa walikuwa wanachukia kushuhudia imani zao kwa ajili ya kuogopa kujitakasa nafsi zao na kuonyesha kuwa ni yenye kukamilika mbele ya Allaah. Lakini inapokuja katika hukumu za kidunia, walikuwa wakiwaita waislamu wote kuwa ni waumini, kwa sababu urafiki, vichinjwa, ushahidi, kuoana kwao na mambo yao mengine yote yalikuwa yanatokana na imani. Ndio maana al-Awzaa´iy alikuwa anaona kuwa jambo hilo ni lenye wasaa na alikuwa akiruhusu yote mawili kufanya uvuaji na kuithibitisha imani.

16 – Muhammad bin Kathiyr ametuhadithia, kutoka kwa al-Awzaa´iy ambaye amesema:

“Mwenye kusema kuwa yeye ni muumini, ni vyema, na mwenye kusema kuwa yeye ni muumini Allaah akitaka, ni vyema pia. Kwa sababu Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

لَتَدْخُلُنَّ الْمَسْجِدَ الْحَرَامَ إِن شَاءَ اللَّـهُ آمِنِينَ مُحَلِّقِينَ رُءُوسَكُمْ وَمُقَصِّرِينَ لَا تَخَافُونَ

”… bila shaka mtaingia al-Masjid al-Haraam ­– Allaah akitaka – hali ya kuwa ni wenye amani, wenye kunyoa vichwa vyenu na wenye kupunguza, hamtakuwa na khofu.”[1]

Alijua kuwa wataingia.”

Naona kuwa hilo linafasiri upokezi wa ´Abdullaah[2] wakati alipomjilia swahiba yake Mu´aadh akamwambia:

“Hujui kuwa watu katika zama za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa makundi matatu: waumini, wanafiki na makafiri? Wewe ulikuwa katika wepi?” Akasema: “Katika waumini.”

Naona kwamba alichokusudia ni yeye kusema kwamba alikuwa miongoni mwa watu wa dini hii na si wengineo. Yeye alikuwa mtambuzi na mwenye kumcha Allaah zaidi kusema kwamba alikusudia kuwa ni muumini mbele ya Allaah. Ni vipi atakusudia kitu kama hicho ilihali Allaah anasema:

فَلَا تُزَكُّوا أَنفُسَكُمْ ۖ هُوَ أَعْلَمُ بِمَنِ اتَّقَىٰ

“Hivyo basi msizitakase nafsi zenu. Yeye anamjua zaidi ni nani mwenye kumcha Allaah.”[3]?

Sidhani kama kabla ya hapo alikuwa akisema kuwa ni muumini kwa lengo la kujitakasa wala lengo lingine. Wala sidhani kuwa alikuwa akimkemea kwa hali yoyote anayesema kuwa ni muumini. Alikuwa akisema kuwa anamwamini Allaah, Vitabu Vyake na Mitume Yake na hazidishi juu ya hayo. Hayo pia baadaye ndio yaliyokuwa yakisemwa na Ibraahiym, Twaawuus na Ibn Siyriyn. Kisha baada ya hapo akajibu ´Abdullaah kwamba ni muumini. Ikiwa upokezi huo umesihi, basi unafasiriwa kama ambavyo punde nilivyokujuza. Hata hivyo nimemuona Yahyaa bin Sa´iyd akiikataa na kuikosoa cheni ya wapokezi wake kwa sababu maswahiba zake ´Abdullaah wanaonelea kinyume chake.

Isitoshe tunaona jopo la wanazuoni ambao walikuwa wakijiita waumini bila kufanya uvuaji katika imani zao. Wakisema kuwa ni waumini. Miongoni mwao ni ´Abdur-Rahmaan as-Sulamiy, Ibraahiym at-Taymiy, ´Awn bin ´Abdillaah na waliokuja baada yao kama vile ´Umar bin Dharr, as-Swalt bin Bahraam na Mis´ar bin Kidaam. Naona kuwa walisema hivo kwa ajili ya kubainisha kuwa wameingia katika imani, na si kwamba imani zao zimekamilika. Huoni kuwa tofauti kati yao na Ibraahiym, Ibn Siyriyn na Twaawuus ilikuwa kwamba hawa walikuwa…[4] kabisa ilihali wengine walikuwa wakijiita kwa jambo hilo.

[1] 48:27

[2] Bi maana Ibn Mas´uud. Hadiyth inayoashiriwa iko katika ”Kitaab-ul-Iymaan” (73) ya Ibn Abiy Shaybah. Katika cheni ya wapokezi wake kuna mtu ambaye hakutajwa jina. Yahyaa bin Sa´iyd pia ameikataa, lakini atavyotaja mtunzi hivi karibu.

[3] 53:32

[4] Imekuja namna hiyo katika asili. Kinachodhihiri ni kwamba kuna kitu kinakosekana. Pengine kulikuwa ”hawa walikuwa hawajiiti kwa jambo hilo kabisa… ”

  • Mhusika: Imaam Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 38-41
  • Imechapishwa: 25/06/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naawswir-ud-Diyn al-Albaaniy